The House of Favourite Newspapers

Rage Awapa Ushindi Simba Dhidi ya Merrikh

0

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, amesema kuwa Simba wanayo nafasi kubwa ya kushinda rufaa dhidi ya Klabu ya AL Merrikh juu ya timu hiyo kuwachezesha wachezaji wasiostahili kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa wiki iliyopita nchini Sudan.

 

Rage alisema Simba inaweza kunufaika baada ya Klabu ya Al Merrikh kuwatumia wachezaji waliofungiwa kwenye mchezo huo kwani mchezaji hawezi kushiriki mashindano ya Caf kama hana leseni ya kushiriki ligi ya nchi anapochezea na mchezaji kama huyo anakuwa hana nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa.

Akizungumzia ishu hiyo Rage alisema: “Simba ina nafasi kubwa ya kupata pointi tatu kwa Al Merrikh, kama kweli wachezaji watatu wa timu hiyo wamefungiwa na Chama cha Mpira cha Sudan baada ya kufanya kosa la kusaini klabu mbili tofauti, makosa ambayo Caf na Fifa ni wakali sana.

 

“Barua ambayo Chama cha Soka cha Sudan kimeziandikia klabu kuwajulisha wamewafungia wachezaji hao, kwa mujibu wa kanuni za Caf na Fifa moja kwa moja wachezaji hao wanakosa sifa kucheza mashindano ya kimataifa.

 

“Hivyo kama wale wachezaji waliruhusiwa na Caf au Fifa kushiriki mashindano hayo, basi Simba wanatakiwa kulalamikia kuomba au kulalamikia kadi au leseni ambazo ziliwaruhusu, kwa sasabu zile za mwanzo zilishafutwa kwa hiyo hawakuwa na uhalali wa kucheza tena.“

Lakini kwa mambo yanavyoonekana ni kwamba wale wachezaji hawakuwa halali hivyo Simba watashinda rufaa hiyo kisha mambo mengine yataendelea kama kawaida,” alisema Rage.

 

Klabu ya Simba ilitoa taarifa kuwa imeandika barua kwenda Fifa kuomba uchunguzi juu ya wachezaji wawili Ramadan Ajab na Bakhiet Khamis, ambao inatajwa walicheza dhidi ya Simba wakiwa wamefungiwa na Chama cha Soka cha Sudan.Iwapo Al Merrikh itakutwa na hatia, Simba wanaweza kupewa pointi zote tatu katika mchezo waliotoka sare na timu hiyo nchini Sudan, Jumamosi iliyopita.

Stori: Issa Liponda, Dar es Salaam

Leave A Reply