The House of Favourite Newspapers
gunners X

CAG: ATCL Haina Ndege

0

ACHANA na hasara ya Sh 60 bilioni iliyopata Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema ndege za shirika hilo hazitotengenezeka zikiharibika hivyo kujiweka kwenye hatari ya kutumika kwa muda mfupi.

 

 

Uwezekano huo unatokana kile alichokibaini kwenye ukaguzi wake kwamba ATCL haijalipa Sh71.48 bilioni ya tozo za kukodisha ndege za Serikali na fedha ya akiba ya matengenezo.

 

 

Iko hivi, ATCL haina ndege ingawa inatoa huduma za usafiri. Ndege zote inazozitumia imezikodi kutoka kwa Wakala wa Ndege wa Serikali (TGFA).

 

 

Ukodishaji huo ulifanywa kwa mkataba ulioingiwa Oktoba 2016 na, Julai na Desemba 2018. Katika mikataba hiyo, ATCL ilikodi serikalini ndege nne aina ya Bombardier Dash 8 – Q400, Airbus mbili aina ya A220-300 na Boeing mbili aina ya B787-8.

 

 

Makubaliano hayo yanamtaka mkodishaji kulipa tozo ya kodi kila mwezi na fedha ya akiba ya matengenezo katika kiwango maalumu kilichoainishwa.

 

 

“Katika ukaguzi wa makubaliano haya nilibaini TGFA ilimtoza ATCL kiasi cha Sh79.62 bilioni ambazo ni gharama za kukodi ndege na fedha ya akiba ya matengenezo. Hata hivyo, TGFA ilipokea Sh8.14 bilioni kutoka ATCL na Sh71.48 bilioni hazijalipwa mpaka mwishoni mwa Juni 2020,” anasema CAG.

 

 

Kiasi ambacho hakijalipwa Cag anasema kinajumisha Sh28.39 bilioni za tozo ya kodi na Sh43.08 bilioni ya fedha za akiba za matengenezo.

 

 

Licha ya juhudi za TGFA kufuatilia tozo ambazo hazijalipwa, ATCL ilieleza kuwa “mazingira ya biashara sasa hivi yamesababisha kampuni kupata changamoto ya kulipa viwango vilivyowekwa na mkataba.”

 

 

Kutokana na ugumu huo wa kulipwa, Cag amesema iliilazimu TGFA kuliwasilisha suala hilo kwa bodi ya kumshauri waziri ambayo ilielekeza TGFA, ATCL na wawakilishi wa katibu mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi) wakae pamoja na kuzipitia tozo hizo.

 

 

Kwa maoni yake, CAG anasema “kutokulipwa kwa gharama hizo zenye thamani ya Sh71.48 bilioni kunaiweka TGFA katika hatari ya kushindwa kutekeleza matengenezo ya ndege husika kama miongozo ya ndege inavyotaka hivyo kupunguza muda wa maisha ya ndege husika na utendaji kazi wake.”

 

 

Ili kuondokana na hali hiyo, Charles Kichere (CAG) ameshauri Serikali ihakikishe ATCL inakuwa na mkakati utakaosaidia kulipa gharama iliyobakia na kufanya tathmini ya viwango vya tozo vilivyopo kwenye mkataba ili kupata viwango sahihi.

 

 

Leave A Reply