The House of Favourite Newspapers

TBC kikaangoni kwa kurusha harusi ‘live’

0

tbc.
Watu waliokuwa kwenye sherehe ya harusi iliyorushwa moja kwa moja na TBC juzi. Picha na Mtandao
Kwa ufupi

Serikali imeliagiza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutoa maelezo ya kina baada ya kurusha matangazo ya moja kwa moja sherehe za harusi kwa zaidi ya saa mbili, jambo lilihojiwa na wananchi maeneo mbalimbali hasa katika mitandao ya jamii.
Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kupata malalamiko mengi kwa kile kilichokuwa kinarushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC1 cha shirika hilo linaloendeshwa kwa ruzuku kutoka Serikalini.
Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye alibainisha kuwa amepokea simu za watu wengi waliokuwa wanahoji juu ya kipindi hicho, hivyo kulazimika kuchukua hatua mara moja za kutaka maelezo kutoka kwa watendaji wa shirika hilo.
Miongoni mwa programu za burudani na masuala ya kijamii, kituo cha TBC1 kinacho kipindi cha Chereko ambacho hurushwa kila Jumapili kwa matukio ambayo yamerekodiwa, lakini hali ilikuwa tofauti juzi usiku baada ya sherehe za harusi hiyo kurushwa moja kwa moja.
Kwa urefu wa muda uliotumika kurusha sherehe hizo, watazamaji wengi walishikwa na butwaa hivyo kuzua mijadala kwenye mitandao ya kijamii wakihoji inawezekanaje kwa TBC1 kutoa muda mrefu kwa mtu mmoja kwa ajili ya shughuli yake binafsi.
“Mtu hawezi kuitumia Televisheni ya Taifa kwa matakwa yake. Hii ni mali ya umma. kama kila mwenye pesa atakuwa na uwezo wa kulipia muda wa matangazo, si muda wote tutakuwa tunawaona watu wenye hela tu badala ya vipindi muhimu?” alihoji mwananchi mmoja katika mtandao wa kijamii.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana alisema kwa kifupi kuwa kipindi hicho ni sehemu ya vipindi vya kituo hicho cha televisheni.
“Kile ni kipindi cha Chereko ambacho tunacho kwenye programu zetu,” alisema Mshana.
Alipoulizwa ilikuwaje ratiba ya kipindi hicho ikabadilishwa kutoka Jumapili mpaka Jumamosi, alisema: “Kile ni kipindi cha wikiendi na kama mtu sherehe yake inafanyika siku hiyo, inakuwa haina shida yoyote.”
TBC ni shirika linalomilikiwa na Serikali likiwa na televisheni na redio.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, kituo hicho kilikuwa kikilalamikiwa kwa kuendesha kwa upendeleo kipindi cha Jambo Tanzania ambacho hupitia na kusoma magazeti makubwa ya kila siku. Katika moja ya vipindi hivyo, habari zilizokuwa zikihusu wagombea wa upinzani zilikuwa hazisomwi licha ya kuwamo kwenye magazeti yaliyokuwa yakichambuliwa.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene amewahi kukaririwa akisema kuwa ameshaliandikia barua za onyo shirika hilo juu ya kukiuka kanuni za utangazaji ambazo hazitaki upendeleo wa aina yoyote.

 

CHANZO: MWANANCHI

Leave A Reply