The House of Favourite Newspapers

Wahujumu Yanga wakamatwa Manzese

0

Jerry Muro (38)-001Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro.

Wilbert Molandi na Nicodemus Jonas
YANGA imewakamata watu wanne waliokuwa wakiihujumu timu hiyo kwa kutengeneza tiketi bandia kisha kuziuza ambazo ni za mchezo wa leo wa timu hiyo dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius.
Watu hao walikamatwa jana eneo la Manzese jijini Dar es Salaam wakiwa na tiketi hizo bandia ambapo wengine walikimbia baada ya kuwaona wenzao wakikamatwa.
Yanga leo inacheza na Cercle de Joachim mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya awali kushinda bao 1-0 wiki mbili zilizopita huko Mauritius.

SIMBA-YANGA-2.jpgMashabiki wa timu ya Yanga wakifanya yao.

Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, katika oparesheni yao jana walifanikiwa kukamata watu wanne Manzese waliopanga kuuza tiketi bandia na tayari wamewafikisha katika vyombo vya dola.
“Mashabiki wanatakiwa kuwa makini katika ununuaji wa tiketi kwani baada ya kuwakamata watu hao, tulisitisha mauzo katika baadhi ya vituo na kubakisha vituo viwili tu, klabuni na Uwanja wa Karume,” alisema Muro.
“Kwa kesho Jumapili tiketi zitauzwa Uwanja wa Taifa tu na mtu anatakiwa kununua katika magari yatakayokuwa na polisi na nembo maalum.”

PLUIJM ATAMBA
Wakati hayo yakitokea, bila straika Donald Ngoma, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm amesema kikosi chake kitaifunga Cercle de Joachim leo Jumamosi na kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pluijm ameliambia Championi Jumamosi kuwa, hakuna kitakachowazuia ushindi katika mechi hiyo kutokana na maandalizi mazuri aliyoyafanya ya wiki nzima.

YANGA (1)Wachezaji wa timu ya Yanga wakifanya mazoezi.

Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema hawatawadharau wapinzani wao, badala yake amepanga kuingia bila ya kufikiria matokeo ya ushindi ya mechi ya kwanza na kutafuta mabao mapema.
“Kikosi changu hakitakuwa na mabadiliko makubwa kwenye mechi ya kesho (leo) ambapo Ngoma hatakuwepo wala Haruna (Niyonzima) ambaye ni majeruhi wa kifundo cha mguu ‘enka’.
“Wapinzani wetu ni wazuri siyo wabaya, lakini ninaamini sisi pia wazuri, hivyo utakuwa mchezo mzuri,” alisema Pluijm.
Katika nafasi ya Ngoma, Pluijm anaonekana atamtumia Malimi Busungu ambaye alimfanyisha mazoezi ya kucheza pamoja na Amissi Tambwe katika mazoezi ya jana asubuhi.
Kikosi cha Yanga leo kinatarajiwa kupangwa hivi; Ali Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Pato Ngonyani, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Tambwe, Busungu, Deus Kaseke.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Cercle de Joachim, Abdel Ben Kacem, ametamba kuwa wataibuka na ushindi na kusonga mbele katika michuano hiyo.
“Tumekuja kupambana kuhakikisha tunapata ushindi katika mechi hii, hivyo Yanga wajiandee kwa hilo,” alisema Kacem. Katika mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kesho Jumapili Mafunzo ya Zanzibar itacheza na AS Vita ya DR Congo nchini DR Congo.

Leave A Reply