Waziri Mkuu Mwigulu Aagiza Upanuzi wa Nafasi kwa Wachezaji Wazawa Kujiandaa AFCON 2027 – Video

Waziri Mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa agizo kwa wizara za michezo na mashirikisho ya soka nchini (TFF na ZFA) kuangalia upya kanuni za mashindano ili kuwapa nafasi zaidi wachezaji wazawa, ikiwa ni mkakati wa kuandaa kikosi imara kuelekea mashindano ya AFCON 2027 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.
Akizungumza leo Januari 5, 2026, visiwani Unguja, Zanzibar, Waziri Mkuu amependekeza kuwa mashindano kama ya Kombe la Shirikisho na Ligi ya Muungano yatumie wachezaji wazawa pekee. Amesema hatua hiyo itasaidia kupanua wigo wa wachezaji wa ndani kupata uzoefu wa mashindano mengi na kuwaandaa vyema kabla ya kuungana na wachezaji wanaocheza nje ya nchi.
Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza kwa dhati Timu ya Taifa, Taifa Stars, kwa kiwango walichokionesha katika mashindano ya AFCON nchini Morocco. Amesema kuwa ingawa timu hiyo imeyaaga mashindano, haikutoka bali “imetolewa” kutokana na mazingira ya mchezo, hasa katika dakika za mwisho za mchezo wao wa mwisho.
Kufuatia ushujaa huo, Waziri Mkuu amewaelekeza Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, pamoja na Wizara ya Michezo, kuandaa mapokezi ya kishujaa kwa vijana hao watakaporejea nchini.

