Wachina Wakamatwa Dar Wakiwa Na Bilioni 6 Ndani Ya Nyumba – Video

Taarifa zilizosambaa mapema leo, Januari 6, 2026, kwenye mitandao ya kijamii zimeeleza kuwa raia kadhaa wa China wamekamatwa katika eneo la Oysterbay, jijini Dar es Salaam, wakiwa na fedha taslimu zinazodaiwa kuwa na thamani ya shilingi bilioni 6 za Kitanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, tukio hilo lilitokea majira ya saa 5:30 asubuhi, ambapo uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, ulifanikiwa kuwakamata raia hao wa kigeni wakiwa na kiasi kikubwa cha fedha taslimu, zikiwemo fedha za Kitanzania na Dola za Kimarekani.
Fedha hizo zilidaiwa kukutwa zimefichwa katika ghorofa ya tatu, Apartment namba 317, katika Jengo la Phoenix, Mtaa wa Mazengo.
Hatua hiyo ilielezwa kuwa ilifuatia ufuatiliaji wa muda mrefu uliohusisha vyombo vya ulinzi na usalama, baada ya kuibuka kwa shaka juu ya mwenendo wa maisha ya watuhumiwa hao, ikiwemo matumizi makubwa ya fedha na mienendo isiyo ya kawaida, hususan nyakati za usiku kuanzia saa 7:30 usiku hadi saa 10:00 alfajiri.
Baada ya kupata taarifa hizo, GLOBAL TV ilizungumza na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay, Mololo Abel Mwaisumo, ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa atatoa ufafanuzi zaidi baadaye.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Doreen Kapwani, amesema kuwa ufafanuzi kamili kuhusu tukio hilo utatolewa kesho, Januari 7, 2026, kupitia Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni.
“TAKUKURU tulikuwepo na tumeshiriki katika tukio hilo, lakini ufafanuzi wa kina zaidi utatolewa kesho, Januari 7, 2026,” amesema Kapwani.

