The House of Favourite Newspapers

Magufuli okoa hiki kizazi

0

Magufuli amalizia Baraza la Mawaziri-001Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

John Joseph, Dar es Salaam

SIJAWAHI kuwa muumini wa siasa za chama chochote hapa nchini lakini ni mfuatiliaji wa tasnia hiyo kwa kuwa najua siasa ndiyo inaendesha dunia, huo ndiyo ukweli, niseme wazi kuwa nimevutiwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani miezi minne iliyopita.

Magufuli amekuwa kiongozi mtendaji na kuniaminisha kuwa kumbe inawezekana ila basi tu, kuna vitu vingi ambavyo vinaonekana kurejea kwenye mstari, amefanya mengi yeye na uongozi wake ndani ya muda mfupi, nawapa heko kwa yote yaliyotokea, Mungu awazidishie afya njema na maisha marefu ili Watanzania tutembee kifua mbele tunapovuka mipaka.

Wakati yote hayo yakiendelea kuna jambo kuhusu madawa ya kulevya yanavyoa-ngamiza kizazi cha vijana, natamani kumu-eleza na kumfa-fanulia Rais Mafuguli hisia zangu kuhusu janga hili lakini najua ni vigumu kumfikia ‘live’.

Nilitamani kumuandikia barua lakini kizazi hiki cha digital naona nitakuwa napoteza muda tu, nikapata wazo la kumpigia simu nako najua itakuwa mchakato mrefu mpaka kumpata.
Sasa nimeamua kuandika barua hii ya wazi kwenda kwa rais wetu, haya ambayo nitayaeleza hapa ndiyo hayo ambayo ningeweza kumueleza kama ningempigia simu Rais Magufuli na kisha ningempata yeye mwenyewe na siyo wasaidizi wake.

(Simu inaita)…rrrrring…rrring
Magufuli: Haloo!
John: Shikamoo mheshimiwa, naitwa John Joseph Haramba ni mwandishi na mhariri wa Gazeti la Championi Ijumaa, nashukuru kwa kunipa muda wako japo dakika chache kukueleza kilicho ndani ya ubongo wangu.

Magufuli: Marahaba, nakusikiliza mwanangu, endelea…
John: Asante sana mzee ni hivi…

Lengo la kupiga simu
Mzee wangu nataka kukueleza juu ya madawa ya kulevya jinsi ambavyo yamekuwa ni janga la kitaifa japokuwa suala hili linachukuliwa poa kwa kuwa linahusisha mitandao mingi ya siri na ninaamini kuna wenye nguvu wengi wanahusika, mifano ipo mingi ya watu waliowahi kuhusishwa na kukamatwa lakini kesi zao au madai hayo yakapotea kimyakimya.

Vijana wanateketea
Juzijuzi nimekusikia ukisema kama vijana hawataki kufanya kazi basi wachukuliwe kwa nguvu wakafanye kazi ikiwemo kulima ili wakitoka huko wawe wamejifunza, pia ukasema hutaki kuona wakicheza pool asubuhi kwa kuwa unahisi nguvu kazi zao hazitumiki vizuri, nakuunga mkono katika hilo lakini kuna kitu nyuma ya pazia.

Kila kukicha katika vyombo vya habari madawa ya kulevya yanapokamatwa yamekuwa yakitajwa kuwa thamani yake ni mamilioni na mabilioni ya fedha, kutokana na ugumu wa maisha kuna baadhi ya vijana wameingia tamaa na kutaka kujaribu biashara hiyo kwa kuwa thamani ya fedha zinazotajwa ni sehemu ya ushawishi kwao kujitosa kwenye biashara hiyo.

Wasanii & wanamichezo ni mifano
Awali, kuvuta na kuuza bangi ndiyo ilikuwa ‘fasheni’ lakini leo bangi haina ‘dili’ tena kwani kama ni kuvuta wanavuta sana tu tena wakati mwingine hadi hadharani na hakuna anayejali.

Kuna wasanii wengi maarufu na wanamichezo wenye majina ambao wamewahi kukiri kutumia au kuhusishwa katika biashara ya madawa ya kulevya ambayo pia yanatambulika kwa majina mengi kama vile unga na poda, wingi wa wasanii hao hasa vijana ni mfano hai kwa kuwa kuna maelfu ya vijana ambao nao wanahusika ama kwa kuuza au kutumia.

Msanii ni kioo cha jamii, kama kuna wasanii wengi wanatumia au kuuza maana yake ni kuwa jamii yao nayo inahusika kwa kiwango cha juu.Orodha ya wale waliowahi kukiri au kukamatwa au kutajwa kwenye matumizi au biashara ya unga ni ndefu, baadhi yao wameshajiondoa katika matumizi ya unga na wamekuwa mabalozi wazuri.

Mzee Kikwete alionyesha mfano
Kitendo cha Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kujitokeza hadharani na kumsaidia msanii wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ ilikuwa ni mfano hai kuwa hata mzee wangu aligundua vijana wanapotea ndiyo maana akamsaidia Ray C ili wengine waige.

Taasisi magumashi
Inawezekana neno magumashi likakuchanganya mzee, lakini kwa sisi vijana ni neno la kawaida tunamaanisha ubabaishaji.
Kuna taasisi nyingi zimeanzishwa, nyingine zimeshapotea, nyingine zipo zinajiingizia fedha kwa gia ya kusaidia vijana waliothirika lakini wapo ambao hawana nia nzuri zaidi wanasaidia wachache na fedha nyingine wananenepesha matumbo yao.Juhudi za Kikwete zinapotea hewani, kwa kuwa kama ni ongezeko la watumiaji linazidi kukua kila siku.

Mitaani kumechafuka
Mzee wangu Magufuli ukipita mitaa fulani ya Dar es Salaam hapa Kinondoni kuna sehemu zinajulikana kabisa ni noma kwa unga, mbaya zaidi wengi wao hawana kazi za maana na kwa kuwa wanahitaji kutumia basi wanajikuta wakiingia kwenye makundi ya waporaji, majambazi na mengine mengi ambayo ni mabaya.

Tunakosa nguvu kazi michezoni, jeshini, kazini
Hakuna mchezaji ambaye anawekutumia unga na akacheza soka, lazima itafikia hatua ndani ya muda mfupi mwili wake hauwezi kuendana na kasi. Mbali na hapo huwezi kuwa mwanajeshi, mkulima, muimbaji mzuri kama unatumia unga, hapo namaanisha kuwa nguvu kazi ya taifa inapotea.

Waliojitokeza hadharani wasaidiwe
Kuna baadhi ya wasanii ambao wamejitokeza hadharani na kuomba wasaidiwe, mmoja wao ni Rashid Makwiro ‘Chid Benz’, kila nikikumbuka rapa huyu wa Hip Hop alivyokuwa bora, naumia kuona kipaji chake kimepotea kutokana na unga, yeye na wenzake ambao wanajitokeza kukiri kuathirika na madawa ni vema wakasaidiwa na liwe somo kwa wengine wajue kuwa poda ni adui wa binadamu.

Mtandao unajulikana
Kama tunao wanaotumia na wanajulikana, iweje wanaoingiza madawa hayo hawajulikani? Siamini katika hilo, najua inaweza kuwa ngumu kuumaliza mtandao wote lakini uongozi wako ukiwa mkali kama ilivyo ule wa Hong Kong, tutafanikiwa.

Najua wanaoingiza wana nguvu ya fedha na hata nguvu katika baadhi ya mamlaka lakini naamini kama umeweza kurejesha imani ya wanaoichukia siasa au wasiokichukia chama chako, amini hata katika hili unaliweza.

Magufuli: Nimekuelewa, nitayafanyia kazi maoni yako.
John: Asante sana mheshimiwa, nimalize kwa kusema tu kuwa nakutegemea ukoe kizazi hiki, ‘Mhola ya seba ibi nang’ho’.

Magufuli: (Anacheka) Kumbe na Kisukuma unakijua! Aya kazi njema.
John: Nakijua wapi mzee, nimeungaunga tu.

Leave A Reply