Afrika Kusini: Rais Ramaphosa Amfuta Waziri Kwa Uongo Bungeni

Johannesburg, Afrika Kusini —
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amemfuta kazi Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Nobuhle Nkabane, kufuatia tuhuma za kusema uongo bungeni kuhusu uteuzi tata wa wajumbe wa bodi katika taasisi za elimu ya juu.
Taarifa kutoka ofisi ya rais zinasema kuwa uamuzi huo umetokana na ripoti ya kamati ya maadili ya Bunge, iliyobaini kuwa Bi. Nkabane alitoa kauli za kupotosha kwa makusudi ili kulinda uteuzi wa baadhi ya watu walio na uhusiano wa karibu na chama tawala cha African National Congress (ANC).
Kwa wiki kadhaa sasa, chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kimekuwa kikitoa wito wa kuchunguzwa kwa Nkabane, kikidai kuwa alihusika moja kwa moja katika kufanikisha uteuzi wa wajumbe wa bodi kwa misingi ya kisiasa badala ya sifa na uadilifu. DA iliwasilisha malalamiko rasmi mapema mwezi huu, ikiambatanisha ushahidi wa barua pepe na mawasiliano ya ndani yaliyodaiwa kuonesha ushawishi wa kisiasa katika mchakato huo.
Kufukuzwa kwa Nkabane kumekuja katika wakati mgumu kwa ANC, ambapo baadhi ya mawaziri wake wamekuwa wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali za matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi. Mvutano ndani ya muungano wa vyama kumi vinavyounda serikali umekuwa ukiongezeka, huku mashinikizo yakiongezeka kwa Rais Ramaphosa kuchukua hatua kali za kurejesha imani ya umma.


Comments are closed.