AFYA za wafanyakazi katika sekta ya usafi hususani watoa huduma ya kutapisha vyoo katika mji wa Maswa na Bariadi mkoani Simiyu, ziko hatari kuambukizwa magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mlipuko kutokana na kufanya kazi bila ya vifaa kinga.
Wafanyakazi hao mara nyingi hukaribiana na uchafu wa kinyesi cha binadamu, na hufanya kazi bila ya vifaa au kinga kwa kutumia mikono yao suala ambalo huwaweka kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa mengi.
Wakizungumza kwa masikitiko na Mwandishi wetu walisema kuwa licha ya kutoa huduma hiyo muhimu katika jamii lakini viongozi wao waliowapa kazi hiyo hawajali afya zao licha ya kuwaingizia fedha.
Baadhi ya wafanyakazi hao waliokuwa wakitapisha choo katika mtaa wa Biafra bila ya kuwa na mipira ya kuvaa mikononi wala kifaa cha kufunika sehemu za pua na mdomo jambo ambalo ni hatari kwa afya zao walisema;
“Hii ndiyo hali yetu ya ufanyaji kazi siku zote sisi tumeajiriwa na kampuni ya usafi ya Mbiti ambayo ndiyo imeingia mkataba na halmashauri ya Maswa kufanya usafi katika mji huu ikiwa ni pamoja na kutapisha vyoo vilivyojaa lakini hatupewi vifaa vya kujikinga kama ubavyoona.
“Kazi hii ni ngumu kwani tunakumbana na kinyesi cha binadamu kwenye hivi vyoo bila tahadhari yoyote na afya zetu ziko rehani kupata magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mlipuko na hata kwenye jamii tunaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu na kuhara hasa kipindi hiki cha mvua za vuli,” alisema Jane John.
Walisema kuwa licha ya kuomba kupatwa vifaa kinga wanapokuwa kwenye kazi zao hizo lakini Msimamizi wao Mkuu, Masanja Mbiti amekuwa akiwapatia ahadi ambazo hazitekelezeki ndiyo maana wanaendelea kufanya kazi katika mazingira hao hatarishi.
Pia walitoa kilio chao kwa ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa kwa kutosikiliza kilio chao hicho licha ya kumjulisha kuwa wanahatarisha maisha yao kwa kufanya kazi bila vifaa kinga.
Akizungumzia malalamiko hayo, Msimamizi wa wafanyakazi hao Masanja Mbiti alisema kuwa siku za nyuma alikuwa akununua vifaa hivyo ambavyo ni mipira migumu ya kuvaa mikononi na barakoa kwa ajili ya wafanyakazi wake lakini sasa ni miezi sita hajalipwa fedha na halmashauri ya wilaya ya Maswa.
“Hata mimi sipendi hawa wafanyakazi kufanya kazi bila vifaa kinga lakini nashindwa nifanyaje maana tunadai fedha za miezi sita hatujalipwa na halmashauri maana ndiyo tulioingia nao ubia wa kazi hii nikipata fedha nitanunua kama ilivyo kawaida nami nathamini afya za hao wafanyakazi wangu,”alisema.
Aidha, alisema kuna wakati aliamua kutoendelea kufanya kazi hizo hadi hapo atakapolipwa fedha hizo lakini wafanyakazi hao waliamua kuendelea kazi bila vifaa kinga.
Afisa afya wa wilaya ya Maswa, Abel Machibya alisema usalama wa usafi lazima uambatane moja kwa moja na mazingira bora kwa wale wanaofanya kazi ya kutunza huduma za usafi na kulinda afya zao.
Alisema watu wote wanatoa huduma za usafi katika wilaya hiyo kabla ya kupatiwa kazi hizo hujaza mkataba na moja ya kipengere katika mkataba huo ni kulinda afya za wafanya usafi kabla ya kufanya usafi huo.
“Kila anayeomba kazi ya kufanya usafi katika wilaya yetu ni lazima kwanza hakikisheni usalama wa wafanyakazi wake kwa kuwa na vifaa kinga wakati wa kazi hatuwezi kukubali kuona wafanya usafi wakiwa hawana vifaa kinga hii ni hatari kwa afya zao na jamii kwa ujumla,”alisema.
Alisisisitiza iwapo wafanya usafi hawana vifaa kinga wakati wa kufanya kazi zao zikiwemo za kutapisha vyoo ni marufuku kufanya kazi hiyo na ikibainika wanafanya kazi katika mazingira hatarishi hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika wote kwani hali hii ikiachwa itaeneza magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya mlipuko.
Mwandishi Wetu



