Ajali ya Ndege Kenya Yauwa Watu 6, Wawili Wajeruhiwa

Watu sita wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa vibaya baada ya ndege ndogo ya shirika la misaada ya matibabu, Amref Flying Doctors, kuanguka katika eneo la makazi la Githurai, Kaunti ya Kiambu, karibu na Jiji la Nairobi, nchini Kenya.
Ajali hiyo imetokea Alhamisi alasiri, Agosti 7, 2025, dakika chache baada ya ndege hiyo kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Wilson ikielekea Hargeisa, nchini Somalia.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa Kamishna wa Kaunti ya Kiambu, Henry Wafula, watu wanne waliokuwa ndani ya ndege hiyo walifariki dunia papo hapo.
Miongoni mwao ni rubani, daktari, muuguzi na mfanyakazi mwingine wa shirika hilo la misaada ya matibabu.
Aidha, watu wawili waliokuwa ndani ya jengo la makazi ambalo ndege hiyo iliangukia pia walifariki dunia kutokana na athari za moto na mshtuko wa ajali hiyo.
“Ni tukio la kusikitisha sana. Ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Wilson. Ilianguka juu ya jengo la makazi na kusababisha moto mkubwa.
“Tunasikitika kuthibitisha vifo vya watu sita na majeruhi wawili ambao wamekimbizwa hospitalini kwa matibabu,” alisema Kamishna Wafula.
Ndege hiyo aina ya Cessna Caravan, mali ya Amref Flying Doctors, ilikuwa katika safari ya kutoa huduma za dharura za matibabu nchini Somalia.
Shirika hilo linajulikana kwa kutoa huduma za kuokoa maisha kwa watu wanaohitaji uhamisho wa haraka wa kiafya, hasa kutoka maeneo ya mbali yenye changamoto za miundombinu ya afya.


Comments are closed.