The House of Favourite Newspapers

AJIBU AONDOLEWA KIKOSINI YANGA

IBRAHIM Ajibu ambae amehusika kwenye mabao 11 ya Yanga msimu huu, hatokuwa sehemu ya mchezo wa leo usiku  wakati timu hiyo ikiiwavaa KMC kwenye Uwanja wa Taifa, hii ni baada ya kupata maumivu ya mgongo ambayo kwa sasa anaendelea na matibabu chini ya uangaliazi wa Daktari wa timu ili aweze kupona haraka na arejee kwenye majukumu yake kwa michezo inayofuata.

 

Hayo yamesemwa leo na uongozi wa Klabu hiyo ya Yanga yenye pointi 19 kwenye msimamo wa ligi huku KMC inayomtegemea kipa mwenye uanachama wa Simba, Juma Kaseja ikiwa na pointi 10.

Licha ya ubora wa Heritier Makambo ambaye ni Mkongomani, lakini Ajibu amekuwa kwenye fomu katika siku za karibuni na ndiye amekuwa akiibeba Yanga.

Mchezaji huyo anaongoza kwa asisti ndani ya Yanga na Kocha Mwinyi Zahera amekiri kwamba ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi kwa sasa ingawa bado amemtaka kujipanga zaidi.

“Wachezaji nimewaambia ndani ya dakika 10 nahitaji kupata matokeo mazuri ili kuweza kuleta ushindani, ligi sio nyepesi kwa kuwa kila timu imejipanga kushinda.

 

“Mchezaji ambaye atakuwa mvivu ndani ya uwanja sioni kazi kumtoa nje kwani nina wachezaji wengi ambao wana uwezo mkubwa hivyo hilo lipo wazi nimewaambia KMC sio timu ya kubeza ni timu ngumu,”alisema Zahera.

Zahera jana jioni alikaa hotelini na wachezaji wake wakaangalia video za mechi mbalimbali za KMC kwenye Ligi Kuu Bara kwa kile alichoeleza hakuwahi kuwaona uwanjani wakicheza.

 

Kocha Etiene Ndayiragije amekuwa akibadili staili yake ya uchezaji kila mara ingawa amekaririwa kwamba ni lazima afanye usajili mwingine wa maana kwenye dirisha dogo linaloanza Novemba 15 kwani hali ya kikosi chake siyo nzuri.

Eliud Ambokile wa Mbeya City ambaye ana mabao sita ndiye anayeongoza msimamo wa wafungaji akifuatiwa na Habib Kyombo wa Singida mwenye mabao matano.

LUNYAMADZO MLYUKA, DAR ES SALAAM

Comments are closed.