The House of Favourite Newspapers

AKATAA CHAKULA KIZURI KABLA YA KUNYONGWA!

Donnie Edward Johnson

DONNIE EDWARD JOHNSON aliyekuwa anasubiri kunyongwa huko Nashville, Tennessee, Marekani, alikikataa chakula chake maalum cha mwisho kabla ya kunyongwa wiki iliyopita Alhamisi, na badala yake aliwataka wanaomuunga mkono kuwapa chakula watu wasiokuwa na makazi.

 

Watu wanaohukumiwa kifo katika Jimbo la Tennessee, wanaweza kupewa chakula kinachofikia Dola 20 (Sh. 47,000) kabla ya kunyongwa lakini Johnson aliyenyongwa kwa kudungwa sindano ya sumu katika gereza  lijulikanalo kama Riverbend Maximum Security Institution huko Nashville, alikikataa chakula hicho.

Kelley Henry, mwanasheria wa Johnson, alisema uamuzi huo wa mteja wake ulitokana na mfungwa mwenzake,  Philip Workman, aliyetaka chakula chenye thamani kama hicho alichokuwa akile mara ya mwisho kabla ya kunyongwa mwaka 2007, kipelekwe kuliwa kwenye kituo cha watu wasiokuwa na makazi kwa kuwatengenezea ‘pizza’.

Maofisa wa gereza hawakupeleka chakula hicho kwenye kituo hicho, lakini watu waliokuwa wanamuunga mkono Workman, walipeleka.  Johnson alitaka watu wanaomuunga mkono wafanye hivyo pia.

“Bw. Johnson alitambua kwamba Dola 20 hazingetoa chakula kwa watu wengi wasio na makazi,” alisema Henry mwanzoni mwa wiki hii akiongeza: “Ombi lake ni kwamba watu wanaomuunga mkono wawe na tabia ya kutoa chakula kwa watu wasiokuwa na makazi.”

Johnson alikuwa ni mtu wa 136 kunyongwa jimboni humo tangu mwaka 1916 na mtu wa nne tangu jimbo hilo lifufue adhabu za kifo mwaka jana.

 

Mtu huyo aliyekuwa na umri wa miaka 38 alihukumiwa kifo kwa mauaji ya mkewe, Connie Johnson huko Memphis,  mwaka 1984, kwa kumsukumizia kooni mfuko wa takataka.

Johnson na wanasheria wake hawakuzungumzia mauaji ya kikatili aliyoyafanya, bali waliomba msamaha kwa Gavana wa jimbo hilo, Bill Lee, kutokana na mfungwa huyo kubadilika vizuri kutokana na mafundisho ya dini akiwa gerezani.  Hata hivyo, gavana huyo alikataa kutoa msamaha.

Pamoja na hayo, baada ya kunyongwa, familia yake imekubali yaishe ikisema atakumbukwa na wengi waliofuatilia mlolongo wa kesi yake hadi mwisho!

Comments are closed.