The House of Favourite Newspapers

Al-Shabaab waua 400 kwa miaka 2

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Mpenzi msomaji bado ugaidi ni tatizo kubwa duniani. Hivi karibuni Kundi la Kigaidi la ISIS liliua watu 130 huku 350 wakijeruhiwa vibaya katika Jiji la Paris nchini Ufaransa. Wiki iliyopita tuliona jinsi ambavyo kundi korofi la kigaidi la Al-Shabaab la nchini Somalia lilivyosambaratishwa na Marekani kwa kushirikiana na majeshi ya Umoja wa Afrika (AU). SASA ENDELEA…

Baada ya mashambulizi ya wanamgambo hao katika Eneo la Mpeketoni, kikosi cha anga cha Kenya kiliingia kazini na kusambaratisha kambi mbili za Al-Shabaab nchini Somalia.
Hata hivyo, wakati mashambulizi hayo yakiendelea, Kundi la Al-Shabaab lilikuwa likitumia nguvu kubwa kukanusha habari kuwa kambi zake zilishambuliwa na kwamba milipuko ya mabomu iliangukia shambani.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya, David Obonyo alikaririwa akisema kuwa ndege za kivita za Kenya zilikuwa zimeshambulia kambi hizo zilizokuwa Mkoa wa Gedo unaopakana na Kenya.
Msemaji huyo alieleza kwamba picha walizopiga kutoka angani zilionesha kwamba kambi hizo ziliangamizwa kabisa na kwamba iliwawia vigumu kukadiria kiwango cha maafa kutokana na mawingu yaliyotanda angani.
Obonyo alitamba kwamba, mashambulizi hayo yalikuwa ni sehemu ya mchakato wa kuzuia Wanamgambo wa Al-Shabaab kuvuka mpaka na kufanya mashambulizi nchini Kenya.
Mashambulizi hayo yalikuja kufuatia onyo la Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwamba atalipiza kisasi kwa hatua kali kadiri inavyowezekana dhidi ya shambulizi lingine la Wanamgambo wa Al-Shabaab katika Chuo Kikuu cha Garissa kilichopo takribani kilomita 200 kutoka mpaka wa Somalia na Kenya.
Kundi hilo la wanamgambo lenye mafungamano la Al-Qaeda lilikuwa limeua zaidi ya watu 400 katika ardhi ya Kenya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Kenya imekuwa ikihangaika kuzuia kuingia kwa wanamgambo hao na silaha kwa kupitia mpaka wake na Somalia wenye urefu wa kilomita 700 na ghasia hizo zimekuwa zikiharibu uchumi wa nchi hiyo kwa kuwatia hofu watalii na wawekezaji.
Msemaji wa operesheni za kijeshi wa Al-Shabaab, Abdasis Abu Musab alikaririwa akisema kuwa moja ya kambi zake iliharibiwa katika mashambulizi hayo lakini mashambulizi mengi badala ya kushambulia kambi yalishambulia mashamba.
Hata hivyo, katika mashambulizi hayo, kuliibuka shutuma katika vyombo vya habari nchini Kenya kuwa taarifa muhimu za ujasusi zilikuwa zikipuuzwa na kwamba ilichukua saa saba kwa vikosi maalum vya usalama vya Kenya kufika katika chuo kikuu hicho kilichoko kilomita 365 kutoka Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi.
Katika shutuma hizo, vikosi vya usalama vilijitetea kwa namna ilivyokabiliana na shambulio hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba kupambana na ugaidi ni kama vile kuwa mlinda mlango wa timu. Unachokifanya ni kuokoa mabao 100 na hakuna mtu anayekumbuka. Kitakachotokea ni kwamba ukifungwa bao moja litakumbukwa zaidi kuliko yale 100 uliyookoa.
Kwa upande wake kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga ambaye alikuwa Waziri Mkuu wakati Kenya ilipotuma wanajeshi wake nchini Somalia mwaka 2013 kupambana na Al-Shabaab alisema kuwa Serikali ya Kenya ilipaswa kuanza kufikiria namna ya kujitoa nchini Somalia kwa kuviondoa vikosi vyake.
Odinga alikaririwa na Gazeti la Kenya la Standard akisema: “Marekani ilikuwa na wanajeshi wengi nchini Somalia lakini iliwaondoa. Kenya pia inapaswa kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Somalia.”
Hata hivyo, kauli hiyo haikusaidia kwani Kenya haikuonesha dalili yoyote ile ya kujitoa Somalia ambapo wanajeshi wake wakiwa sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika (UN) waliyakomboa maeneo mengi yaliyokuwa chini ya mikono ya Wanamgambo wa Al-Shabaab.
Wanadiplomasia wa nchi za Magharibi walidai kwamba kupoteza maeneo hayo hakukudhoofisha uwezo wa Al-Shabaab kufanya mashambulizi ya kushtukiza nchini Somalia au nje ya nchi hiyo.
Mashambulizi ya Garissa ni mashambulizi mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika ardhi ya Kenya tangu Al-Qaeda waliposhambulia Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi mwaka 1998 na kuua zaidi ya watu 200 na kujeruhi wengine maelfu.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.