The House of Favourite Newspapers

ALIYECHINJA WANAE, MKEWE KISHA KUJINYONGA

DAR: Walipozaliwa watoto Clara Dotusi (5), Herieth Dotusi (3), hawakujua kama baba yao Dotusi Isaya angekuja kuwaua kwa kuwacharanga mapanga; lakini usiku wa Septemba 14, mwaka huu wasichokitarajia kilitokea; Uwazi limeibua Ripoti ya Kutisha katika tukio hilo la kusikitisha.  

 

Baba mzazi wa Clara na Herieth, mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam, aliwaua watoto wake wote wawili na kisha kuwajeruhi mkewe aitwaye Mariam Lucas na mama yake mzazi Amanda Joseph ambaye ni mkwewe; kisha naye akaenda kujinyonga.

Tafakuri ya tukio inasisimua ndiyo maana Uwazi liliamua kusogea hadi Nachingwe mkoani Lindi nyumbani kwao Mariam lilikofanyika tukio ili kuchimba undani zaidi.

 

CHANZO CHA TATIZO

Chanzo cha kuaminika kililiambia Uwazi kuwa Dotusi na Mariam walikuwa wakiishi Chanika jijini Dar es Salaam kama mume na mke ambapo walifanikiwa kuzaa watoto hao wawili. “Walikuwa wanaishi hapa (Chanika) maisha yao yalikuwa mazuri tu, lakini baadaye zilianza chokochoko wakawa wanagombana.

 

“Marehemu (Dotusi) aliwahi kuniambia kuwa mke wake ameanza kumdharau, nikawa na mshauri amuulize sababu na ikiwezekana watafute ufumbuzi wa tatizo. “Hilo halikusaidia, ugomvi ulipozidi mke akaamua kuondoka kurudi kwao,” chanzo cha karibu na marehemu Dotusi kililiambia Uwazi kwa sharti la kutotajwa jina.

 

UGOMVI WASHIKA KASI

Inaelezwa na vyanzo vingine vya habari kwamba mara baada ya mke huyo kurudi kwao aliondoka na watoto wake jambo ambalo mume hakuliafiki kwa madai kwamba alitaka aishi nao.. “Mke alimkatalia, akamwambia watoto wakikua atawachukua lakini kwa sasa bado wadogo na kwamba wanahitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa mama,” chanzo chetu kilisema.

 

Aidha, inasimuliwa kuwa awali Dotusi alipoona hawezi kuishi peke yake alimfuata mke wake na kurudi naye Dar, hata hivyo, hawakudumu sana kwani mke alikuwa akimtuhumu mume kuwa ni mbabe na kwamba mara kwa mara alikuwa akimshushia kipigo huku akitishia kumuua na hivyo kuamua kurejea tena nyumbani kwao na kuendelea na maisha yake.

 

VITISHO VYA KUUA VYAZIDI

Mama mzazi wa Mariam; Amanda ambaye naye alijeruhiwa katika tukio hilo alisema kuwa alichokifanya Dotusi alikuwa amekipanga kwa muda mrefu.

“Mara nyingi alikuwa akimtishia mwanangu kumuua, hata aliporudi nyumbani ‘wimbo’ wa kuua ulikuwa mdomoni mwake,” Amanda alisema alipozungumza na Uwazi. Inaelezwa kwamba, vitisho hivyo vya kuuawa alivyotolewa mara kadha na Dotusi; Mariam anatajwa kuviripoti polisi ambako aliambiwa atulie.

 

DOTUSI ATOKA DAR -LINDI

Habari kutoka Chanika zinaeleza kwamba hivi karibuni Dotusi alipanga safari ya kumfuata mkewe huko Lindi kwa kile alichodai ni kwenda kuwachukua watoto wake ili aondoke nao kwenda Bukoba ambako ni nyumbani kwa wazazi wake. “Lakini cha kushangaza siku anaondoka kwenda Lindi alikusanya vitu vyake zikiwemo nguo na kuvichoma moto.

 

“Tukaona hilo si tukio la kawaida, kuna rafiki yangu ikabidi ampigie simu Mariam kumtahadharisha kwamba awe macho kwa sababu mumewe kachoma vitu na amepanga kumfuata huko, wamwangalie asije kufanya tukio baya maana anaonekana hayuko sawa,” chanzo kutoka Chanika kilisema. Hata hivyo, tahadhali hiyo haikusaidia kwani Dotusi aliondoka Dar na kuelekea Lindi huku akiwa na siri ya mauaji moyoni mwake na kwamba alichokuwa akisubiri ni muda wa kufanya tukio ufike.

 

USIKU WA TUKIO

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nambambo Mazoezi, Aron Banda, anaeleza kwamba siku ya tukio Mariam ambaye kwa sasa ni mahututi anadaiwa kwenda kutWoa taarifa polisi ya kutishiwa maisha na mumewe na kwamba kulikuwa na kitisho cha mtuhumiwa kufika Lindi kumtafuta. Inaelezwa kuwa Dotusi alipowasili Lindi huku akiwa amejaa roho ya kishetani aliandaa panga na kukaa mafichoni hadi giza lilipoingia, ambapo alijisogeza nyumbani anapoishi mkewe na watoto na kuanza kuwavizia.

 

Wakati mkewe akikosa taarifa ya mumewe kuwepo eneo analoishi, Mariam aliendelea kufanya shughuli zake; lakini ilipofika saa 5 usiku, Dotusi aliyekuwa amejihifadhi kwenye pagala aliingia ndani kwa kuruka ukuta kupitia sehemu ambayo haijamalizika kujengwa.

 

Taarifa zinaeleza kwamba Dotusi alipoingia ndani mtu wa kwanza kukutana naye ambaye kwa wakati huo alikuwa hajalala alikuwa ni mkewe ambapo alianza kumshambuliwa kwa kumkata mapanda kisogoni na mabegani. Baada ya kujeruhiwa Mariam alipiga kelele kidogo kisha akandondoka chini, jambo ambalo Dotusi alijua kuwa amekwisha muua na kwamba zamu ya wengine kufa ilikuwa imewadia.

 

Wakati Dotusi akigeuka na kumuacha Mariam akiwa anavuja damu, alikutana na mkwewe ambaye hakumkawiza alimjeruhi kwa panga jambo lililomfanya mkwe huyo akimbilie nje kuomba msaada kwa majirani. Hata hivyo, kinachoonekana kwa mujibu wa silimulizi kutoka eneo la tukio msaada wa majirani ulichelewa kutolewa, jambo lililompa nafasi muuaji kuendelea kufanya unyama wake.

 

DOTUSI AWAFUATA WANAYE CHUMBANI

Wakiwa hawajui kuwa dakika za kuwepo kwao dunia zimebaki chake na wao kundelea kulala wakiamini ni amani, Clara na Herieth waliposhtuka walijikuta wamevamiwa na baba yao aliyefika kuwatoa uhai.

 

Inaelezwa kuwa kwenye chumba hicho walikuwa wamelala watoto wanne, wawili wa ndugu wa Mariam na wengine ni wa Dotusi. Inaelezwa Dotusi alipomwinua mtoto wa kwanza alitambua kuwa hakuwa wa kwake, akamsukumiza chini na kumwacha akilia asijue kinachoendelea.

 

Alipomwinua mwingine alimwita kwa jina; “Clara,” mtoto alipoitika ikawa ndiyo kauli yake ya mwisho kwani baba yake alimcharanga kwa mapanga mwilini kisha kumkata kichwa na kumwacha kama mnyama akivuja damu huku akikata roho. Kama hilo halitoshi, alimfuta Herieth alikokuwa amejilaza naye bila huruma alimmaliza kinyama kisha kumkata kichwa kisha kutoka chumbani akiwa amelowa damu kama kachinja ng’ombe.

 

MARIAM APATA FAHAMU

Huku akiwa ametapakaa damu ile hali ya kupoteza fahamu aliyopata baada ya kushambuliwa na mumewe ilimtoka Mariam na kujikuta akisikia purukushani chumbani kwa wanaye zikiendelea ambapo aliamua kukimbilia polisi kuomba msaada.

Inaelezwa kuwa, alipofika polisi huku akiwa hajui kilichotokea nyuma yake aliripoti tukio la kushambuliwa kwake asijue kuwa wanaye walikuwa wameuawa kinyama. Inaelezwa kwamba, hatua ya kwanza waliyochukua polisi ni kumsaidia Mariam kumpeleka hospitalini kwa ajili ya taratibu za matibabu lakini wakati wanaendelea na zoezi hizo mwewenyekiti wa mtaa alifika kituoni hapo huku akitweta.

MWENYEKITI ASIMULIZA MAUJI.

“Mimi nimekuja kuamshwa kuwa Mariam anashambuliwa na mumewe, nilipokusanya wenzangu tumefika nyumbani kwake tumekuta mauaji ya kutisha,” mwenyekiti aliwasimulia polisi alichokiona. Mara baada ya kusimulia hayo polisi waliondoka kwenda eneo la tukio ambako walikuta majirani wamekusanyika huku kila mtu akihuzunika kivyake na baadhi ya wanawake wakilia.

MTUHUMIWA KUJINYONGA

Polisi walipomaliza kujionea unyama waliofanywa na Dotusi, kazi yao ilikuwa ni kuanza kumtafuta ambapo wengi waliamini kwamba ametokomea kusikojulikana na ilikuwa lazima atiwe mbaroni. Katika hali ya kushangaza polisi walipofungua chumba anacholala Mariam, walimkuta Dotusi akiwa amejinyona kwa kutumia kanga ya mkewe huku ikielezwa kwamba kabla ya kujinyonga pia alikunywa maji makali ya betri.

KISA CHA DOTUSI KUUA NI NINI?

Chanzo cha kuaminika kinasema kwamba msongo wa mawazo ulikuwa unamsumbua Dotusi kwa muda mrefu, kwa kile kinachotajwa kuwa hali yake ya maisha kuyumba. “Mwanzo alikuwa na maisha mazuri lakini yakayumba, akawa mtu wa mawazo, hata tabia zilibadilika, akawa mkorofi nafikiri ndiyo kisa cha mke kumkimbia.

“Baada ya hapo akaanza kumtuhumu mkewe kwamba amemkimbia kwa sababu ameona maisha yameyumba na kwamba huko Lindi ana mwanaume mwingine,” chanzo kilidai kuwa huwenda ndiyo chanzo cha Dotusi kufikia hatua za kufanya unyama huo.

Aidha, kuhusu kuwaua watoto wake inaelezwa kwamba alifikia hatua hiyo kwa imani ya ovyo kwamba hakupenda kuwaacha watoto wake duniani eti wangeteseka na kwamba heri awaue wasipate tabu ya maisha, jambo ambalo halitakiwi kuaminiwa kwa sababu duniani kuna yatima wengi wanaishi kwa mafanikio bila kusaidiwa na wazazi wao.

DADA WA MARIAM ASIMULIA

Alipotafutwa dada wa Mariam, aitwaye Ashura Abdallah, ambaye yuko hospitali akimuuguza mgonjwa alisema: “Kwanza hili tukio la kinyama sana, linaumiza na kusikitisha mno, lakini ndiyo kama mlivyosikia, kwa sasa sipo hospitalini nimetoka kidogo. “Mdogo wangu hali yake bado ni mbaya, tunahangaika kuokoa maisha yake, kama unavyojua matibabu ni gharama. “Tunashukuru kwa ushirikiano tunaopata kutoka kwa ndugu na marafiki, lakini tunaomba kwa mtu yeyote ambaye anaweza kutusaidia chochote asisite, tutamshukuru sana,” alisema dada huyo wa Mariam.

CLARA, HERIETH WAZIKWA

Katika masikitiko makubwa Jumamosi wiki iliyopita watoto Clara na Herieth walizikwa bila wazazi wao kutupa udongo kwenye makaburi yao kutokana na mama yao kuwa mahututi hospitali.

“Masikini watoto hawa, wamekosa nini kwa Mungu jamaniii, kwa nini hakuwaacha waishi kama ni matatizo yalikuwa yake, ooooh…” alisikia mama mmoja akilia wakati miili ya watoto hao ikipelekwa makaburini. MUNGU AZILAZE ROHO ZAO MAHALI PEMA PEPONI.

NDUGU WA DOTUSI WASIKITIKA

Katika hatua nyingine ndugu wengi wa marehemu Dotusi wamekuwa katika huzuni kubwa kufuatia tukio hilo la kusikitisha ambalo wanaamini nyuma yake ipo nguvu kubwa ya ibilisi.

Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa tangu siku ya tukio ndugu hao wamekuwa wakikutana kujadili namna ya kushughulikia msiba huo mzito unaohusisha ndugu yao, watoto wake na kuwepo kwa majeruhi wawili walioshambuliwa kwa mapanga na Dotusi kabla hajajiua. Kamanda wa polisi Mkoa wa Lindi Pudensiana Protus amethibitisha kutokea kwa tukio hili.

MCHANGO WAHITAJIKA

Kufuatia gharama za matibabu ya Mariam wewe msomaji kama umeguswa na habari hii unaweza kuchangia chochote kupitia namba ya dada wa mama wa watoto aitwaye Ashura Abdallah kupitia namba za simu 0652 780 320.

Comments are closed.