The House of Favourite Newspapers

AMA KWELI HUJAFA HUJAUMBIKA…MAMA AOZA HUKU AKITEMBEA

HICHO ndicho anachokutana nacho mwanamama Rhobi Mwita Chacha, mkazi wa Sirari-Tarime mkoani Mara ambaye amejikuta akioza huku akitembea.  Rhobi hana mume, alijikuta akitolewa jicho moja baada ya kutokea kipele kwenye jicho lake la kulia, lakini baadaye uvimbe mdogo ulianza kidogokidogo pembeni mwa jicho na kufunika hadi eneo la sikio.

HARUFU KALI

Mwanamama Rhobi anatoa harufu mbaya na kali kiasi kwamba akiwa umbali wa mita 200 harufu inasikika hivyo watu kumkimbia na maisha yake sasa yamekuwa magumu mno. Rhobi amekuwa akiomba msaada sehemu mbalimbali bila mafanikio.

MSIKIE RHOBI

Akisimulia kisa na mkasa na kujikuta kwenye hali hiyo, Rhobi, katika mazungumzo na mtangazaji Flora Lauwo wa Nitetee TV, alisema; “Nimefikia hatua ya kuja huku Igoma- Mwanza kwa ajili ya kuomba msaada.

MUME AFARIKI DUNIA

“Kabla ya yote, mwanzoni nilikuwa ninaishi vizuri na mume wangu kule Mugumu (Mara), lakini mume wangu alifariki dunia. “Baada ya mume wangu kufa niliamua kuondoka Mugumu na kwenda kutafuta maisha kule Sirari-Tarime.

KITU KAMA UPELE

“Nakumbuka nilianza kuumwa jicho baada ya kutokewa na kitu kama upele, niliumwa sana na jicho

ATOLEWA JICHO

“Baadaye upele ulikuwa mkubwa kiasi cha jicho kuning’inia. Ndipo nikaenda Bugando (hospitalini Mwanza) ambapo jicho langu la kulia lilitolewa, nikabaki na jicho moja. “Baada ya kutolewa jicho nilikaa kama miezi sita ndipo uvimbe kama uleule wa jichoni ukaanza tena kwenye sikio. Huo uvimbe ulianza kama ule wa jicho kwani kilijitokeza tu kinyama kidogo kikiwa na muwasho. Nilianza kujikuna sana kabla ya kuamua kwenda kliniki.

“Nilipokwenda kliniki waliniambia nikapime mionzi ili kujua kama itakuwa ni kansa ijulikane ili ikatolewe kabla ule uvimbe haujawa mkubwa. Tatizo lililojitokeza hapo sikuwa na hiyo hela.  “Nilipokwenda kwenye kipimo cha mionzi nilishindwa kupima kwa kuwa sikuwa na hela hivyo ilinilazimu kurudi nyumbani.

TATIZO LAZIDI

“Hapo sasa ndipo tatizo langu lilipozidi kwani ule uvimbe ulizidi kuongezeka kabla ya kupasuka na damu zikaruka. “Baada ya hapo nilikimbizwa hospitalini, ikabidi kwanza niongezewe maji dripu tano. Baada ya hapo nilipelekwa Tarime (hospitalini), huko nililazwa na baadaye niliambiwa nirudi Bugando.

LAKI SABA YAHITAJIKA

“Niliporudi Bugando sikuwa na hela hivyo waliniambia nitoe shilingi laki saba ili wanipime na kufanyiwa operesheni, lakini tatizo likawa ni lilelile la kutokuwa na hela. “Baadaye walitangaza kuwa kuna wataalam wanakuja kupima watu macho na uvimbe bure hivyo na mimi nikaenda, lakini waliponiangalia waliniambia niende Moshi (Kilimanjaro) nikatibiwe huko, lakini kiukweli sikuweza kwani sina uwezo na nina maisha magumu sana. “Nina watoto wananitegemea, wakati mwingine nalala hivyohivyo tu.

MAJIRANI WAMKIMBIA

“Majirani wananikimbia ninanuka, hata nikienda kupanga majirani wanahama, wananitukana kutokana na kidonda changu kinavuja damu, kinavuja usaha, kinatoa maji usiku kucha nalala kama nimemwagiwa maji. “Kiukweli nimechanganyikiwa, sina hela, sina jinsi naomba Watanzania mnisaidie kwa sababu hapa nilipo nimeoza, ninanuka. Hata nikipanda kwenye daladala, watu wanashuka, wananikimbia kutokana na harufu.

ASHINDWA KULA

“Ukweli ninanuka maana hata nikikaa mwenyewe nashindwa kula kutokana na harufu kunijia, usiku sijifuniki, nafunga tu kitambaa na muda siyo muda kile kitambaa kinakuwa kinanuka. “Nalala kwa shida sana na nimeambia kutibiwa ni shilingi laki saba, lakini sina uwezo ndiyo maana ninateseka kiasi hiki. “Kwa sasa ninaishi kwa kuzunguka kuombaomba kwa kutumia karatasi ambayo inaonesha ninahitaji msaada ndiyo inayoniwezesha kuishi mimi na wanangu.

UGONJWA GANI?

“Mpaka sasa hivi hawajaniambia ni ugonjwa gani na sina hela hata ya kwenda hospitalini kuosha kidonda hiki,” anasema Robby na kuongeza: “Ndugu zangu wengi ambao wangeweza kunisaidia walishafariki dunia. Alibayebaki ni mama ambaye naye anaumwa mguu na mama mdogo alishakuwa kipofu hivyo sina pa kukimbilia kwani hata ndugu wa mume wangu walishanitenga.

“Ninawaomba chondechonde Watanzania wenzangu wanisaidie kwani sina pa kukimbilia. Usiku silali, ninakaa tu kitandani na mawazo tele, nikitoka kukaa nje majirani wananikimbia na wengine kuhama nyumba, wanasema ninanuka na nimeoza hivyo hata kujisaidia ni humohumo ndani ya chumba na watoto wangu maana nikionekana msalani au bafuni watu wananitukana. “Watoto wangu tu ndiyo wananiambia hata kama ninanuka watabaki na mimi hivyohivyo hadi mwisho.

YEYOTE ANAYEGUSWA

Sote tunatamani huyu mama aanze matibabu na tunaanini kabisa akipata matibabu atapona hivyo kwa yeyote anayeguswa na tatizo lake awasiliane naye kwa namba 0759 665 555 au 06775 55 550.

Comments are closed.