The House of Favourite Newspapers

ARDHI KUSAJILIWA KIELEKTRONIKI KWA SHILINGI 5,000

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.

 

WIZARA ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua rasmi mpango wa kutambua na kusajili kila kipande cha ardhi kwa Mkoa wa Dar es Salaam kama sehemu ya kuongeza usalama wa milki ya ardhi.

 

Kupitia mpango huo wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wote watatambuliwa na kisha kupewa leseni ya makazi au hati ya makazi ambayo itakuwa katika mfumo wa kieletroniki.

 

Akizungumza  Machi 16,2019 wakati wa uzinduzi wa mpango huo ambao utaanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam na kisha kuendelea mikoa yote nchini, Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema leseni hiyo baada ya kutolewa itadumu kwa miaka mitano.

 

“Ndani ya hii leseni ya kieletroniki ambayo itadumu kwa miaka mitano kutakuwa na taarifa zote muhimu.Kutakuwa na jina la mmiliki wa ardhi, ukubwa wa kiwanja, majirani zake, namba za kitambulisho cha Taifa na taarifa nyingine muhimu.

 

“Kwa hiyo leseni hiyo ya makazi itawezesha kila kipande cha ardhi kutambuliwa kikamilifu, hata ukiwa nje ya Tanzania kiwanja kitaonekana maana kipo kieletroniki.

 

“Tutaondoa changamoto za ujambazi wa viwanja lakini pia wakati huo huo leseni ya makazi itasaidia katika kupata mkopo benki na leseni hii itarahisisha masuala ya ulinzi na usalama,”amesema Lukuvi.

 

Amesema kila mwananchi atatakiwa kuchangia Sh.5000 ambapo Sh.4000 zitakwenda katika manispaa na Sh.700 itakwenda kwa kijana ambaye ni mtaalama anayetembea na simu kwa ajili ya kufanya usajili huo na Sh.300 zitakwenda kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ambaye atakuwa na mtaalam husika.

 

Amefafanua kuwa jambo hilo litakwenda nchi nzima na haamini kama kuna Mtanzania atashindwa kupata Sh.5000 kwa ajili ya kupata leseni ya makazi ambayo haina tofauti na hati zaidi ya kwamba yenyewe itakuwa ya miaka mitano.

Amesema leseni hiyo ya makazi itakuwa na taarifa zote kama zile ambazo ziko kwenye hati ya makazi na kubwa zaidi thamani ya mwenye hati na leseni ya makazi wote wako sawa.

 

Lukuvi ametoa ombi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Seleman Jafo akatoa mkazo wa kuhakikisha kote nchini wanashiriki kikamilifu mchakato huo ambao pia utasaidia kuongeza makusanyo ya kodi ya Serikali.

 

Amesema leseni hizo mpya ni muhimu na kutoa ufafanuzi kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni muhimu kuwa nazo kwani leseni za makazi zilizokuwepo zimekwisha muda wake maana ni za mwaka mmoja mmoja tu.

 

“Sheria ya makazi inaeleza wazi walioko kwenye maeneo ambayo hayajapimwa na yapo kiholela badala ya kubomoa makazi yao yanatakiwa kuboreshwa.Nia ya Serikali ni kuhakikisha watu wanaishi kwa usalama katika makazi yao, kikubwa tunaomba ushirikiano kufanikisha mchakato huu.Hatutatoka Dar es Salaam hadi pale ambapo tutaona tumemaliza kazi,”amesema Lukuvi.

 

Kabla ya mpango huo, amesema kulikuwa na mchakato wa kurasimisha makazi lakini ukweli mchakato huo unachangamoto zake kwani wapo wenye leseni za makazi lakini wahusika wameshindwa kuzichukua kutokana na gharama yake kuwa kubwa lakini kupitia mpango huo mpya gharama iko chini.

 

Akifafanua zaidi kuhusu mpango huo amesema hatua ya kwanza itakuwa ni kupita maeneo yote na kisha kuchukua taarifa za kila mhusika na baada ya hapo wataalam wataziweka katika daftari na kisha kurudisha tena kwa wananchi kulipitia na baada ya hapo sasa ndio zitaandaliwa taarifa rasmi ambazo zitakuwa mtandaoni na zipatikana hata kwenye simu ya mkononi.

“Kwa mara ya kwanza kila Mwenyekiti wa mtaa na Serikali ya mtaa watakuwa na daftari ambalo litaonesha taarifa zote,”amesema Lukuvi na kufafanua.

Comments are closed.