The House of Favourite Newspapers

Asali Yenye Miaka 2000 Yakutwa Kwenye Mapiramidi

0

MAPIRAMIDI ya Misri ni miongoni mwa maajabu saba ya dunia lakini ndani yake, kumegunduliwa maajabu mengine yaliyowashangaza wengi.

Mwaka 2006, wataalamu wa mambo ya kale waliokuwa wakifanya utafiti kwenye mapiramidi hayo, waligundua kitu kilichowashangaza sana. Ndani ya moja ya mapiramidi hayo, walikuta chungu kikubwa, kikiwa na asali.

 

Uchunguzi wao ulionesha kwamba asali na chungu hicho, vimekaa eneo vilipokutwa kwa zaidi ya miaka 2000 lakini cha ajabu, asali bado ilikuwa nzima na waliopata fursa ya kuionja, walikiri kwamba ilikuwa na ladha halisi ya asali na usingeweza kuitofautisha na asali iliyotoka kurinwa muda huo.

 

Jambo hilo liliwashangaza sana wote waliokuwa kwenye utafiti huo ambapo ili kujiridhisha, ilibidi chungu hicho kitolewe na kupelekwa maabara ambapo uchunguzi wa kina ulianza kufanyika.

 

Kilichobainika, ni kwamba licha ya asali hiyo kukaa miaka yote hiyo, bado haikupoteza sifa yake hata moja, ilikuwa katika ubora wake na ingeweza kutumika kwa shughuli yoyote kama yalivyo matumizi ya kawaida ya asali.

 

Hata hivyo, uchunguzi zaidi kwenye chungu hicho, ulibaini mabaki ya mifupa ya mtoto mdogo, yaliyokuwa chini kabisa ya chungu, ambayo hayakuwa yamecha-nganyikana na asali hiyo.

 

Baadaye, ikaja kubainika kwamba watu walioishi kwa kipindi hicho, walikuwa na utamaduni wa kuwatoa kafara watoto wachanga, hasa wa kiume kwa kuwaua kisha kuiweka miili yao kwenye vyungu vikubwa vilivyojaa asali, kama sadaka kwa miungu yao ili kuwakinga na mabalaa mbalimbali.

 

Ili kujiridhisha zaidi, watafiti hao walirudi tena kwenye mapiramidi ambapo walifanikiwa kupata vyungu vingine kadhaa, vikiwa na asali ambayo chini ilikuwa na mabaki ya mifupa ya watoto, lakini yenyewe ikiwa kwenye ubora wake uleule.

 

Kitaalamu, inaelezwa kwamba asali ndiyo chakula pekee kisichoweza kuharibika. Hii ni kwa sababu, asali ina mchanganyiko wa kipekee wa maji na virutubisho vingine, ambavyo kwa pamoja hufanya kiwango cha asidi (pH) kuwa kati ya 3.2 hadi 4.5.

 

Kiwango hiki cha asidi, hakiwezi kuruhusu kuzaliana au kuishi kwa kiumbe chochote, si bakteria, vimelea vya magonjwa wala virusi ndiyo maana huwa haiharibiki hata ikae maelfu ya miaka.

Leave A Reply