The House of Favourite Newspapers

Azam kuja na vifungashio vipya vya unga wa ngano

Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni ya Said Bakhresa Group, Hussein Sufian (kushoto) na Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni hiyo, Ahmed Jaruan, wakiwaonyesha waandishi wa habari mwonekano mpya wa vifungashio vya unga wa ngano wa Azam ujulikanao kama Ngano Bora, ikiwa ni mkakati wa kulinda ubora na kutambulisha bidhaa zake kwa wateja.

 

UONGOZI wa kampuni ya kutengeneza vyakula inayomikiliwa na makampuni ya Said Salim Bakhresa &Ltd,  na inayozalisha unga bora wa ngano wenye jina la kibiashara la Azam, imetangaza kubadilisha mwonekano wa bidhaa yake maarufu ya unga wa ngano unaojulikana kwa chapa ya Ngano Bora.

Mwonekano mpya wa kifungashio (mfuko) wa bidhaa hii umeboreshwa ili kuwapatia wateja wake kuitambua kwa urahisi na kuweza kuitofautisha na bidhaa zenye vifungashio vinavyofanana nayo.

Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni hiyo, Hussein Sufian , amesema kumekuwepo na wazalishaji ambao wanaiga na kubadilisha rangi za muonekano wa bidhaa zao zifanane na bidhaa za AZAM, hali ambayo imekuwa ikiwachanganya wateja kwenye masoko kutambua bidhaa za kampuni hiyo.

Alisema kutokana na kubadilisha vifungashio, wateja wa Ngano Bora, unaotengenezwa na AZAM kwa sasa wataweza kutambua bidhaa hizo kwa urahisi pia ametoa tahadhari kwa wazalishaji wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiiga muonekano wa bidhaa za kampuni hiyo  kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wanavunja sheria na tayari wameishatoa taarifa kwa mamlaka mbalimbali, watakaokamatwa kwa kufanya udanganyifu huu watachukuliwa  hatua za kisheria.

Aidha kampuni imetoa tahadhari kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitumia vifungashio vya bidhaa za kampuni hiyo zilizotumika na kujaza bidhaa nyingine na kuziuza kwa wateja kama bidhaa za kampuni ya AZAM. Sufian alisema kampuni inapenda kuwahakikishia wateja wake kuwa itaendelea na ubunifu na uzalishaji wa bidhaa zenye kiwango cha juu cha ubora ili kukidhi matakwa ya wateja wote ndani na nje ya nchi.

Comments are closed.