Baada ya Harmonize Kusepa… Mbosso, Rayvanny Vita Nzito !

DAR ES SALAAM: Bado upepo haujatulia ndani ya lebo kubwa ya muziki barani Afrika ya Wasafi Classic Baby (WCB), chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ baada ya mmoja wa memba wake, Rajab Abdul ‘Harmonize’ kusepa zake.

VITA NZITO

Habari mpya inawagusa memba wake wengine wawili, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ na Mbwana Kilungi ‘Mbosso’ ambao wanadaiwa kuwa kwenye vita nzito ya kuziba pengo la Harmonize ndani ya Wasafi.

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba, baada ya Harmonize kujitoa Wasafi, Rayvanny na Mbosso wamekuwa wakisababisha tafrani vijiweni, magrupu ya WhatsApp, Facebook na Instagram kutokana na ubishani mkubwa.

NDANI YA WASAFI

Chanzo cha ndani kilifunua kuwa, baada ya Harmonize, Diamond anahitaji mtu wa kumuonesha njia mbalimbali alizopita yeye hasa kutoboa kimataifa kama alivyofanya kwa Harmonize. “Ni ukweli usiofichika kwamba, Diamond ndiye alimuonesha njia Harmonize hadi akatoboa kimataifa kiasi cha kujiona sasa anaweza kusimama mwenyewe.

“Kuna kitu watu hawakijui. Diamond siyo mchoyo kabisa linapokuja suala zima la kusaidia mtu ili atoboe. Ndicho alichokifanya kwa Harmonize na sasa anafanya kwa memba wake mwingine na hapo ndipo vita ya Rayvanny na Mbosso ilipoibukia. “Habari za ndani ni kwamba baada ya Harmonize kusepa, Diamond anataka kumpandisha mmoja kati ya Rayvanny na Mbosso ambaye ataziba pengo la Harmonize.

“Hapo ndiyo kuna kimbembe kwani jambo hilo limesababisha mpasuko ndani ya Wasafi wenyewe kisha kwa mashabiki wao mitaani ambao kwa sasa ni mamilioni; wa ndani na nje ya Bongo.

NI RAYVANNY?

“Wapo wanaomuona Rayvanny ndiye atachukua nafasi ya Harmonize kutokana na vigezo anavyovitaka Diamond. “Baadhi ya vigezo hivyo ni pamoja na uwezo binafsi. Rayvanny ana uwezo mkubwa wa kutunga mashairi kwa kucheza na maneno hata yasiyokuwa na maana ilimradi tu yanaimbika na kuendana na mdungo wa biti kama anavyofanya Diamond mwenyewe kwenye baadhi ya nyimbo zake.

“Kigezo kingine kinachombeba Rayvanny ni uwezo wa kuimba na kufanya shoo kubwakubwa ndani na nje ya nchi.

“Tayari Rayvanny amefanya vizuri kwenye shoo za nchi mbalimbali Afrika, Ulaya kama Uingereza, Marekani na mabara mengine. “Lakini kubwa zaidi kwa Rayvanny ni kwamba tayari ametoboa kimataifa maana ana kolabo nyingi za wasanii wa nje baada ya Diamond mwenyewe na Harmonize.

“Rayvanny ana kolabo na wasanii kama Rowlene na DJ Mapholisa wa Afrika Kusini, Bahati na Willy Paul wa Kenya, Pitbull wa Marekani na wengine kibao. “Kingine ni tuzo. Rayvanny ana tuzo kubwa ya BET na nyingine kama Afrimma na nominations (kuchaguliwa kushiriki) kwenye tuzo kama ya MTV.

MBOSSO NI ‘HARMONIZE MPYA’?

“Lakini wapo wanaoamini Mbosso ndiye ‘Harmonize mpya’ pale Wasafi kutokana na namna anavyokuja juu kwa kasi kulinganisha na Rayvanny.

“Mbosso ni mtunzi mzuri sana wa mashairi yanayoimbika na yenye ujumbe mzito hasa wa kimahaba, ni mwimbaji na anajua kufanya shoo kubwa na zenye kuamshaamsha. “Tayari amefanya shoo nyingi kubwa sehemu mbalimbali duniani tangu akiwa na Yamoto Band kama barani Afrika, Ulaya, Marekani na kwingineko hivyo na yeye siyo mdogo kiivyo.

“Kuhusu kolabo za kimataifa na yeye yumo maana amefanya na wasanii kutoka nchi mbalimbali kama Chikune wa Namibia, Reekado Banks, Tekno wa Nigeria, Gabu, Will Paul, Bahati na Otile Brown wa Kenya na wengine kibao,” kilimaliza kufunguka chanzo hicho cha ndani ya Wasafi.

NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII

Hata hivyo, katika upekuzi wa gazeti hili uligundua kuwa, Rayvanny anabebwa na kigezo kingine cha kuwa na idadi kubwa ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram na YouTube.

Kwa upande wa Instagram, Rayvanny ana wafuasi milioni 3.7 wakati Mbosso ana milioni 2.3. Kwingineko kwenye YouTube, Rayvanny ana wafuatiliaji waliojiunga kwake wapatao milioni moja wakati Mbosso ana laki sita.

DIAMOND AMSIFIA RAYVANNY

Hata hivyo, wakati ubishani huo ukiendelea, mara kadhaa Diamond amekuwa akimsifia na kumkubali Rayvanny kama alivyofanya hivi karibuni kwenye Tamasha la Wasafi mjini Moshi ambapo katika moja ya nyimbo zao alimtaka Rayvanny kuimba kipande cha wimbo ambacho alipaswa kukiimba Harmonize ambaye hakuwepo baada ya tetesi za kujitoa Wasafi kushika kasi.

HUYU NDIYE RAYVANNY

Rayvanny, kabla ya hapo alijulikana kwa jina la Raymond akiwa kwenye Kundi la TipTop Connection ambako huko hakuwika sana. Rayvanny alianza kupata umaarufu mkubwa baada ya kusainiwa Wasafi ambapo aliachia wimbo wake wa Kwetu, siku chache baada ya Harmonize kuachia wa kwake wa Bado.

Baadaye aliachia ngoma nyingine kali kama Natafuta Kiki, Sugu ambayo imetolewa kama wimbo wa ziada tu hasa ukizingatia umechukua biti ya Bow Wow (What’s My Name). Kisha aliachia Mbeleko, Shikwambi, Zezeta na Kijuso aliyoimba na Queen Darleen, Pochi Nene aliyoimba na s2kizzy na baadaye Mwanza wimbo ambao aliimba na bosi wake, Diamond Platnumz. Wimbo huo ulifungiwa na Baraza la Sanaa nchini Tanzania (Basata) kutokana na kutokuwa na maadili hivyo kufanya wimbo huo kutopigwa kwenye vyombo vya habari nchini Tanzania.

Baada ya wimbo huo kufungiwa yeye na Diamond waliachia wimbo uitwao Tetema, wimbo ambao ulipendwa na watu wengi na kuufanya kuwa na watazamaji wengi kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mfupi sana.

HUYU NDIYE MBOSSO

Katika safari yake ya kimuziki, umaarufu wa Mbosso ulianza akiwa na kundi zima la Yamoto Band ambalo ndani yake kulikuwa na Aslay, Beka Flavour, Enock Bella na yeye Mbosso.

Kwa pamoja walikuwa wanaunda Yamoto Band chini ya Mkubwa Fella na Wanawe. Baada ya Yamoto Band kufa, Mbosso aliamua kurudi nyumbani kwao kijijini huko Kibiti mkoani Pwani. Akiwa kijijini alijihusisha na vitendo mbalimbali vya kihalifu kufuatia kukata tamaa na kuona wenzake wakiwa wanapata mafanikio yeye akiwa amebaki tu nyumbani.

Jambo hili, lilikuwa tofauti kidogo na kina Aslay na Beka Flavour. Hawa waliendelea kutamba katika muziki hadi hapo Diamond alipoona muda unafaa sasa kumrudisha Mbosso katika tasnia ya muziki kama alivyomuahidi mwaka 2014 kwamba atamsaidia na kumuweka kwenye ramani ya muziki wa Bongo Flava.

Wimbo wa kwanza wa Mbosso ulitoka mnamo Januari 28, 2018 na ulikwenda kwa jina la Watakubali. Januari 29, 2018, Mbosso alitambulishwa mbele ya hadhira ya kwamba yeye ni msanii kamili aliyesaini mkataba na Wasafi.

Hadi sasa Mbosso ametoa nyimbo kibao kama Watakubali, Nimekuzoea, Alele, Shida, Picha Yake, Hodari, Nipepee, Hodari, Tamu na nyinginezo. Wimbo mwingine aliotoa na Wasafi ni Zilipendwa na mwingine aliutoa na Diamond na Lava Lava unaoitwa Jibebe.


Loading...

Toa comment