The House of Favourite Newspapers

BALAA LA MVUA Maiti 3 Zaopolewa, Bado 9

MARA: Balaa la mvua! Baada ya watu 12 kusomwa na maji wakiwa kwenye mtumbwi katika Mto Mara uliopo mpakani wa Serengeti na Tarime mkoani Mara wiki iliyopita, miili ya watu watatu imepatikana.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alithibitisha kupatikana kwa miili hiyo alipokuwa akitoa taarifa ya tukio hilo kwenye Baraza la Madiwani wiki iliyopita.

Aliwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo huku tisa wakiwa wamenusurika kuwa ni Chacha Wambura (24), Mwikwabe Mahende (23) wakazi wa Kijiji cha Buchanchari na John Waibe (35) mkazi wa Kijiji cha Marasomoche.

“Mtumbiwi huo ulikuwa umebeba watu 12 kutoka Buchanchari wakiwa na maziwa na bidhaa nyingine kama mkaa na ukazama na watu hao watatu wakafariki dunia, juhudi za kutafuta miili ya wengine tisa inaendelea hadi ipatikane,” alisema mkuu huyo wa wilaya. Watu hao walikuwa wanavuka kutoka Serengeti kwenda Nyamongo kwa ajili ya kuleta bidhaa zao sokoni.

Ajali hiyo ilitokea saa saba mchana na gazeti hili la UWAZI lilizungumza na manusura wa ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Matiko Ikenge, mkazi wa Serengeti aliyedai kuwa wingi wa maji ndiyo ulisababisha mtumbwi kupinduka.

“Hapa hatuna kivuko kingine salama kwani mitumbwi ni mibovo pia wanapakia watu wengi pamoja na mizingo.“Tunaomba serikali itusaidie kuondoa kero hii kwani inatugharimu maisha, kwa mfano leo, tunawasaka watu hao tisa waliosombwa na maji,” alisema Ikenge.

Naye mwanamke mmoja ambaye pia alinusurika, mkazi wa Buchanchari, aliyejitambulisha kwa jina la Gati Chawana alisema kuwa maji yalikuja wa kasi na kumshinda mpiga kasia hivyo kusababisha mtumbwi kupinduka na kuzama. “Kilichoniokoa mimi ni kule kung’ang’ania gunia la mkaa hadi kuokolewa na watu waliokuwa karibu kwani maji yalikuwa mengi.

“Ajabu ni kwamba watu wanaendelea kutumia vivuko hivyo vya mtumbwi na Serikali haioneshi kuleta kivuko mbadala,” alisema Gati. Naye diwani wa kata iliyotokea ajali, Furomena Marwa alipohojiwa alisema: “Natoa rai kwa wananchi wa pande zote za Serengeti na Tarime kusitisha uvushaji wa watu wa eneo hili.

“Nawaomba wananchi wazunguke darajani kwa usalama zaidi kwani mvua bado ni nyingi na hufanya mto kufurika na kuhatarisha usalama kwa watu wa eneo hili,” alisema kiongozi huyo.

Polisi wa Kituo cha Nyangoto wakishirikiana na wananchi wanaendelea kuwatafuta watu tisa waliosombwa na maji katika mto huo ambao hawajapatikana. Naye Diwani wa Kata ya Kisaka, Samwel Mwita alisema mbali na watu kuzama, wananchi wamepata madhara makubwa ya mvua hasa waliolima kandokando ya mto huo.

“Hatujafanya tathimini lakini wananchi wamepata hasara kubwa na naomba Serikali ifuatilie athari za Mto Mara ili kupunguza vifo kwa kuwa mitumbwi inayotumika kuvusha watu haina ubora,” alisema Diwani Mwita.

STORI: NELSON BONZO, UWAZI

Comments are closed.