The House of Favourite Newspapers

Banana Zoro Atoboa Siri ‘Dred Rock’ za Wanaye

UKIPE-NDA unaweza kumuita ‘the lejend’, ‘best vocalist of all time’, baba Randy, baba Jermaine au baba Risherde, Ton Pow kama anavyopenda kujiita au jina lolote ambalo ungependa kumbatiza kutokana na uwezo wake mzuri wa kuimba na kucheza na gitaa.

 

Lakini pamoja na majina hayo yote, jina lake la kwenye paspoti ni Banana Ally Zahir Zorro na wengi mnamfahamu kama Banana Zorro.

Huyu ni mwanamuziki mkongwe aliyefanikiwa kujitengenezea heshima kupitia gemu la Muziki wa Bongo Fleva na Zokou kutokana na kazi nyingi alizofanya ambazo ni pamoja na Niko Radhi, Mapenzi Gani, Wasiwasi, Mama, Bado Kidogo, Nzela na hit nyingine nyingi zikiwemo kolabo mbalimbali.

 

Huyo ndiye Banana Zorro ambaye anatoka kwenye familia ya muziki, kwani baba yake, mzee Zahir Zorro ni mwanamuziki mwenye heshima kubwa kwenye Muziki wa Dansi na dada yake Maunda Zorro amewahi kutamba pia kwenye Muziki wa Bongo Fleva.

 

Hata hivyo, pamoja na kuwa kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 20, Banana ni miongoni mwa wanamuziki wachache ambao wamejitenga na skendo.

Wengi mngependa kufahamu juu ya maisha yake binafsi ikiwemo familia, kwa nini hasikiki kwenye kolabo kama zamani, mipango yake ya muziki na mengine mengi. Ijumaa linakusogezea, huyu hapa, telemka naye;

 

Showbiz: Hebu tueleze mwenendo wako wa kazi kwa sasa, kama mwanamuziki solo na bendi pia.

Banana: Kazi zipo nyingi na ninaendelea kurekodi, muda si mrefu nitaanza kuziachia.

Showbiz: Kwa sasa husikiki kwenye kolabo nyingi kama ilivyokuwa awali, kuna sababu katika hili?

Banana: Kiukweli nimeamua kupunguza kutoshirikishwa ingawa maombi ni mengi. Lakini pia kushirikiana lazima kuwe na sababu la sivyo unaweza kujimaliza kimuziki.

Showbiz: Unalizungumziaje gemu la Bongo Fleva?

 

Banana: Biashara ya muziki inakuwa na inatoa ajira kwa watu wengi. Mbali na wanamuziki tu, kuna wanasheria, wapiga picha, wataalamu wa mtandao na wasomi wa biashara. Kiukweli tumefika mbali!

Showbiz: Ni mwanamuziki gani ndani ya Bongo au nje ambaye umewahi kutamani kufanya naye kazi na hajafanikiwa?

Banana: Mipango ipo mingi sana bado. Endeleeni kusubiri.

 

Showbiz: Unamkubali mwanamuziki gani kwenye gemu la Bongo Fleva kwa sasa?

Banana: Wengi sana ila Nandy anatisha.

Showbiz: Kwa upande wa bendi, unadhani nani ni mshindani wa bendi yako ya The B-Band?

Banana: Hakuna bendi ya kushindana na B-Band. Ni bendi kubwa kuliko hata mimi mwenyewe. B-Band ni miziki ya miziki aisee!

 

Showbiz: Kwa upande wa maisha yako binafsi, umefanikiwa kukwepa sana skendo, hili umewezaje?

Banana: Kikubwa huwa ninamuomba Mungu na ninajitahidi kuepuka hizo skendo au kashfa.

Unajua wakati ni ukuta, mazuri ya mtu watu huyasahau haraka sana, lakini mabaya ndiyo baadaye husimama kama mnara wa kumbukumbu za zama zako. Mungu ibariki na kuilinda sanaa na Tanzania.

Showbiz: Tungependa kufahamu namna unavyowalea watoto wako, Randy, Jermaine na Risherde, wana dred, nini hasa kimekuvutia kuwalea katika muonekano huo wa kistaa?

Banana: Hahaa (Anacheka), Kifupi ninawalea wakue kwa heshima, wapate elimu na wawe watu wa kujituma. Kwa upande wa dred rock, siyo hata muonekano wa kistaa, kwani asili yake ni Afrika, kwa hiyo ninatunza utamaduni.

 

Showbiz: Vipi shuleni, hawasu-mbuliwi kutokana na muonekano wao?

Ban-ana: Shule wanayo soma ya Fountain Gate Academy haina tatizo kabisa na muonekano wao, hata hivyo watoto wa mastaa mbalimbali wanasoma katika shule hiyo. Show-biz: Vipi kuhusu mama yao, naye anadred rock kama wewe na watoto?

Banana: Hahaa! (anacheka tena), hapana, hana dred rock.

 

Showbiz: Kwa kumalizia unaweza kuzungumza lolote lile unalopenda kuhusu muziki, lakini pia nikushukuru kwa ushirikiano.

Banana: Asante pia. Kikubwa muziki ni kazi tuheshimu kazi yetu, tuipe heshima inayos-tahili kama sisi tulivyo-ipokea kwa kizazi kilichotangulia.

BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.