The House of Favourite Newspapers

Banda Kutoka Kuonekana Hafai Bongo Hadi Tegemeo Sauz

Mtanzania pekee mwenye uhakika wa namba katika Ligi Kuu Afrika Kusini Afrika Kusini, Abdi Banda.

 

GAZETI la Championi ndilo linaloongoza kwa kusafiri sehemu mbalimbali duniani kuhakikisha wasomaji wake wanapata kile ambacho kitakuwa huenda kilionekana hakiwezi kupatikana au kina ugumu.

Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally Jembe (kulia) akiwa na beki wa Baroka FC, Abdi Banda, Mtanzania pekee mwenye uhakika wa namba katika Ligi Kuu Afrika Kusini Afrika Kusini.

Kama unakumbuka, tulikuletea mahojiano ya ana kwa ana na Neymar wakati huo akiwa FC Barcelona na sasa ndiye mchezaji ghali zaidi duniani.

 

Baadaye ikawa mahojiano ya ana kwa ana na Gerard Pique na Luis Suarez kutoka Barcelona pia tukakuletea mubashara kuhusiana na viwanja vya Santiago Bernabeu unaomilikiwa na Real Madrid na Camp Nou mali ya FC Barcelona tukikueleza mengi sana.

 

Tunakukumbusha tena kwamba Gazeti la Championi ndiyo pekee kwa Tanzania na Afrika Mashariki kupata nafasi ya kuingia kwenye viwanja vya mazoezi vya klabu kubwa duniani vya Real Madrid.

Wakiwa kwenye pozi.

Yaani liliingia ndani ya Uwanja wa Ciudad Madrid ambako lilifanya mahojiano na Kocha wa Vijana wa Madrid, Guti na pia La Masia ambako ndani lilizungumza na Pique.

Kama hiyo haitoshi, tuliendelea kufunga safari na kukuletea sifa na haiba ya viwanja vya Old Trafford wa Manchester United, Stamford Bridge mali ya Chelsea na ule wa Emirates unaomilikiwa na Arsenal.

 

Championi lilikueleza kuhusiana na viwanja hivi likiwa ndani kabisa ya dimba la viwanja hivyo na mengi ulijifunza likiwa huko Manchester na baadaye London likikushushia nondo za kutosha.

 

Usisahau, kwa ajili ya kuhakikisha unapata unachotaka, ana kwa ana tuliwahoji magwiji wa soka duniani kama Edgar Davids, Dwight Yorke, Andy Cole, Gaizka Mendieta, Park Ji Sung na wengine kibao.

 

Tunasafiri kila sehemu kwa ajili yako msomaji wetu, tunajua unachotaka ambacho hauwezi kukipata kwingine na sasa, tunaonyesha uzalendo, timu yetu ikiongozwa na mwanao Saleh Ally JEMBE iko Afrika Kusini kwa mahojiano maalum na beki wa Baroka FC, Abdi Banda, Mtanzania pekee mwenye uhakika wa namba katika Ligi Kuu Afrika Kusini.

Banda ni mchezaji aliyechipukia kisoka katika Klabu ya Coastal Union ya mkoani Tanga.

Aliaminika kama namba tatu, lakini baadaye akapata nafasi ya kucheza kama beki wa pembeni upande wa kushoto. Alipojiunga Simba, baadaye taratibu alianza kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kama beki wa kati.

Hata hivyo, Banda hakudumu sana Simba baada ya kuingia katika migogoro kadhaa ikiwemo ile na viongozi.

 

Wako walioeleza kwamba hakuwa mwenye nidhamu sahihi na baadaye alishutumiwa kwa suala la uvivu na kutofanya mazoezi ya kutosha na hali ilivyokwenda kulikuwa na kila dalili kwamba anarejea tena Coastal Union au timu nyingine za chini.

 

Banda sasa, anakipiga katika timu ya Baroka FC ambayo ni kati timu zisizo na hofu ya kuteremka daraja kutokana na kubaki katika nafasi za kati.

 

Banda alijiamini na anajiamini hapa Afrika Kusini kwamba ana uwezo wa kusonga mbele zaidi ya ilivyokuwa inatarajiwa. Sasa utajiuliza kwa nini alishindwa Tanzania aweze Afrika Kusini? Kipi alikosa Simba anakipata Baroka?

 

Banda ana majibu ya mengi katika mahojiano yake aliyofanya na gazeti hili hapa Johannesburg na anaamini aliyopitia yatamsaidia kujifunza Mtanzania yeyote anayependa mpira na ikiwezekana kufika mbali zaidi.

Anaamini pia alichojifunza yeye na kupita mitihani yote kufikia hapa, itamsaidia yeye na Mtanzania yeyote kutokubali kukatishwa tamaa au kukubali kurudishwa nyuma.

 

Je, yeye alirudishwa nyuma kama ni ndiyo na nani? Kama alikatishwa tamaa nani alifanya hivyo, ni kiongozi au mashabiki au yeye mwenyewe alijiangusha?

Keshokutwa Jumatatu, Banda ataanza kuelezea maisha yake hadi anaondoka Simba, alivyofanikiwa kuondoka Simba na machungu yake. Lakini alichopanga kukifanya na matarajio yake lakini usisahau, anavyoishi hapa Afrika Kusini.

USIKOSE, NDIYO TUMEANZA HIVYO.

PICHA NA HILALY DAUD

Comments are closed.