The House of Favourite Newspapers

Barua Nzito: Aslay Sikio Lisizidi Kichwa!

0

NIWASHUKURU wasomaji wa Barua Nzito kwa maoni na ushauri wenu mbalimbali. Kama ambavyo niliwahi kueleza awali kuwa lengo la safu hii ni kukumbushana, kuelimishana, kuonyana na kusawazishana. Moja kwa moja ujumbe wangu umfikie mdogo wangu Aslay Isihaka ambaye ni mmoja wa wasanii mahiri wa Bendi ya Yamoto ambayo kwa sasa ni kama imesambaratika. Baada ya wasanii hao kutawanyika kila mmoja anaonekana kushika hamsini zake, huku Aslay na Becka Flavour wakionekana kufanya vizuri kwenye gemu.

 

Lakini Aslay akibamba zaidi na mtindo wake wa kuachia nyimbo kali kila mara. Kwa kumbukumbu zangu, Becka ameachia nyimbo kama Sikinai, Libebe na nyingine ambazo ameshirikishwa lakini Aslay ameachia nyimbo zaidi
ya tano, ikiwemo Tete, Mhudumu, Pusha, Koko Tu, Angekuona, Kidawa, Rudi, Natamba na nyinginezo.

Aslay amekuwa akiachia wimbo mpya kila baada ya wiki au wiki mbili, hali ambayo imemfanya awe anasemwa sana midomoni mwa watu, kwani ukipita kwenye vibanda umiza, vibanda vya kuuzia filamu, bodaboda, saluni na kwingineko, nyimbo zake ndizo hasa zinazosikika.

 

Lakini sasa nilichokibaini kwa mdogo wangu Aslay, ni kama sikio lake limeshaanza kuzidi kichwa, hii ni kutokana na kutokuwa na ushirikiano na vyombo vya habari. Malalamiko yamekuwa mengi ya waandishi kumpigia simu na kutopokea au kujibu chochote aidha kwa dharau au kwa sababu nyinginezo.

 

Binafsi sijawahi kuwa na ugomvi naye wala sijawahi kuchukia nyimbo zake, lakini kwenye ukweli nasimama kama mwandishi, shabiki na mdau wa burudani ili kumrekebisha. Mimi mwenyewe nilishamtafuta mara kadhaa lakini hakupokea simu wala kujibu ujumbe wangu, nikachukulia pengine ni majukumu. Nilipoanza kusikia malalamiko kwa wengine tena wa vyombo vingine, nikaanza kuhisi kuna tatizo kwa huyu msanii.

Aslay, wanahabari ndiyo hasa wanaokufanya ufikie hapo ulipofika kwa habari na kazi zako kuzitangaza kwenye vyombo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Inapofika sehemu unaanza kuhisi wewe ni mkubwa zaidi ya wao unakuwa unakosea.

 

Kama unaringia You Tube, ni mtandao ambao wewe umeanza kuufanyia kazi hivi karibuni, kwa maana nyingine, wanahabari walikuwepo kabla ya huo mtandao. Nitashangaa sana kama unahisi kuwa mashabiki uliyonayo kwenye chaneli ya You Tube wanakutosha kuliko wengine wanaohitaji kukusoma na kukusikiliza zaidi.

 

Hivi ni kweli mdogo wangu nyimbo ulizotoa zimekuvimbisha kichwa? Umewahi kujiuliza nyimbo ambazo unazitoa zinaishi au zitaishi kwa muda gani wakati kila moja inaufunika wimbo mwingine? Nikiwa katika michakato yangu ya kila siku, nilijaribu kuwasiliana na wadau wangu wa nje ya Bara la Afrika na Afrika Mashariki.

 

“Wakati nachati na mwanahabari mmojawapo kutoka Afrika Mashariki, nilimuuliza kuhusu wewe Aslay. Cha ajabu jibu alilonipa yule mwandishi ndiyo hasa lililonifanya nikuandikie barua hii. Nanukuu sehemu ya maelezo ya ujumbe wa mwanahabari huyo: ” Aslay sijui mambo yake, sitaki hata kuyajua aise!. Aliniletea madharau nishafuta hata nyimbo zake. Achana naye usiniulize habari zake. Na simu napiga ananijibu kwa madharau duuu! “Wapo wasanii wengi nitawapromoti na watafanya vizuri.

 

Sasa huyo wa nini? Simuhitaji muache aendelee kuwa Nation badala ya International.” Nilijiuliza sana moyoni mwangu kwa nini hataki kukusikia wewe Aslay? Nini hasa kikubwa ulichokifanya kwake? Au mimi nilikosea kitu gani, kwani alivyonitumia ujumbe wake ni dhahiri ulionekana ni wa kughadhabika. Mwanahabari huyo wa nje alinitumia hata baadhi ya chatingi zenu ambazo alikutaka mkutane kwa ajili ya kufanya mahojiano. Aslay, hiyo kwako ilikuwa ni fursa nzuri ya kujitangaza kimataifa, huo ulikuwa ni muda muafaka wa wewe kuanza kufanya shoo nje ya Tanzania bila kujali kama uliwahi kufanya huko nyuma.

 

Aslay kaka, hata kama hutaki kufanyiwa mahojiano basi angalia namna ya kumjibu au kumweleza mtu akakuelewa kuliko kumuonesha dharau ambazo mtu anaendelea kukufikiria vibaya. Kama ulikuwa hujui mwanahabari huyo hapigi nyimbo zako na anafanya kampeni ya kuzungumza na wanahabari wenzake ili ikiwezekana nchi nzima isipige nyimbo zako. Nimekuandikia barua hii kwa sababu nakupenda, napenda ufike mbali zaidi kwa sababu uwezo unao lakini sikio lako la mitandao ya kijamii lisizidi kichwa (wanahabari).

Na Gabriel Ng’osha, Barua Nzito, Maoni&Ushauri: 0620 744 592 

Leave A Reply