The House of Favourite Newspapers

BI KIDUDE ASHANGAA MZEE YUSUF KUACHA TAARAB!

Bi Kidude, enzi za uhai wake.

MILIO ya ndege inasumbua masikio yangu, kijua cha jioni ndicho kinaonekana kuishiaishia, kwa mbali naona milima mingi.

Nimetembea umbali mrefu kidogo na sijui nimetokea wapi, naelekea wapi. Najaribu kuvuta picha ya eneo nililopo, nashindwa kupatambua.

Zaidi nasikia milio ya wanyama ambao hata sijui ni wanyama gani. Wakati nikiendelea kutafakari, kwa mbali namuona bibi ameshika mkongojo.

Anakuja eneo nililopo kwa mwendo wa taratibu huku akivuta sigara na moshi wake wenye harufu kali ukianza kunipata kabla hata hajafika.

 

Anaponisogelea zaidi nagundua bibi huyo ni mkongwe wa muziki wa Taarab nchini, Fatuma Binti Baraka. Yes ni yeye, anaanza kunisemesha!

Bi Kidude: Wewe kijana ni nani na hapa unafanya nini?

Mimi: Kwa kweli mimi ni mwahabari, lakini hapa hata sijui nimekuja vipi na kufanya nini.

Bi Kidude: Mwanahabari unanijua mimi? Maana wanahabari wa siku hizi wengi wao hawajui historia za wakongwe kama sisi.

 

Mimi: (Nikamkazia macho) Mimi nisikujue wewe? Bi Kidude mimi nakutambua vizuri kupitia muziki wako. Ulikuwa unaimba bwana…nani asiyekujua wewe?

Bi Kidude: (akaweka sura ya ukali kidogo) Acha kuongea sana wewe hebu niambie kwanza nani amekiweza kukivaa kiatu changu huko ulimwenguni kama kweli wewe ni mwandishi wa habari.

Mimi: Kiatu chako wewe?

 

Bi Kidude: Ndiyo kwani hapa nazungumza na nani?

Mimi: Oooh! Kwa kweli hakuna, wengi wameendelea kujaribujaribu, lakini hakuna aliyeweza kufika levo zako zile za kupandaa na kushuka.

Bi Kidude: Hahaha! Kwani nani sasa hivi anakimbiza kwenye ulimwengu wa Taarab?

Mimi: Wapo Jahazi wanaendelea kufanya vyema, lakini si kwa kasi ile. Yupo Isha Mashauzi, Khadija Kopa na wengine ambao kimsingi kidogo hawavumi sana kama ilivyokuwa zamani.

 

Bi Kidude: Mbona hujamtaja Mzee Yusuf, yule nilikuwa namfuatilia sana, alikuwa anakwenda kuuvaa umaarufu kama wangu.

Mimi: Huyo ameshaachana na mambo ya muziki. Amemrudia Mungu wake na kusema hataki tena kujishughulisha na muziki ambao unamweka dhambini.

Bi Kidude: Heeh! Kaacha muziki? Nini kimemkuta jamani?

Mimi: Ni mambo tu ya kuguswa na imani, akaona Taarab inamweka kwenye dhambi hivyo hana budi kuachana nayo.

 

Mzee Yusuf.

 

Bi Kidude: Jamani…ni jambo jema kuishi katika misingi ya kumjua Mungu, lakini mashabiki wake atakuwa amewaweka njiapanda. Unajua muziki una ‘uchizi’ wake. Unamshika mtu kama dini vile.

Ndiyo maana mimi enzi zangu ilikuwa hata waje wanamuziki gani, lakini mimi nilikuwa nikipanda tu, sauti yangu wakaisikia, basi kila mtu atashangilia.

Mimi: Hilo ni kweli, siwezi kukubishia…

Bi Kidude: Nini sasa lakini kinaufanya muziki wa Taarab ushuke kiwango kwa sasa?

 

Mimi: Mi’ nandhani ni upepo tu wa mihula ya kiburudani. Sasa hivi Bongo Fleva angalau imekamata, wasanii wake wanapata shoo nje na ndani ya nchi.

Bi Kidude: Nawajua baadhi ya hao wasanii wa Bongo Fleva…hivi Lady Jaydee yupo? Wale wajukuu zangu akina Linah je?

Mimi: Lady Jaydee yupo, anafanya vizuri bado. Linah sasa hivi ni mama wa mtoto mmoja. Anafanya bado muziki japo si kwa kiwango kile cha awali, nadhani masuala ya familia nayo yamechangia.

 

Bi Kidude: Nimemkubuka Diamond naye yupo? Kamuoa Wema au bado wanaishi kama wachumba?

Mimi: Daaah! Wale wana historia ndefu, lakini kimsingi tu ni kwamba wamekuwa na rekodi ya kuachana na kurudiana. Mara ya mwisho alipomuacha, Diamond alikutana na Mganda aitwaye Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ akazaa naye watoto wawili naye juzijuzi tu hapa wameachana.

Bi Kidude: Sasa tatizo ni nini? Diamond mkorofi au hao wanawake ndiyo wakorofi?

Wakati nataka kumjibu, ghafla nikashtuka na kuangalia pembeni, naona mazingira ya kitandani kwangu. Daah! Kumbe mazungumzo yangu na Bi Kidude yalikuwa ni ndoto na si halisi!

 

SAA TISA USIKU KITANDANI KWANGU

Comments are closed.