The House of Favourite Newspapers

Black Rhyno Afunguka Kilichompoteza

 

MWAKA 2009, Wimbo wa Black Chata ulifanya poa sana ndani na nje ya Bongo kiasi cha kumtambulisha vyema kwenye anga za kimataifa mwanamuziki Nicholaus HauleBlack Rhyno’, baada ya kushindanishwa kwenye vipengele viwili vya Tuzo za Channel 0 katika vipengele vya Video Bora ya Mwaka ya Hip Hop Afrika na Video Bora ya Mwaka ya HipHop Afrika Mashariki.

 

Mbali na kumtambulisha Rhyno, lakini video hiyo pia iliupeleka muziki wa Bongo Fleva mbali na mashabiki wengi duniani wakaufahamu. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba Rhyno, C-Pwaa na A.Y ni miongoni mwa wanamuziki wa mwanzo kabisa kulitambulisha gemu la Bongo Fleva kimataifa.

 

Nyimbo nyingine zilizomtambulisha kwenye gemu ni Mistari na I am So Happy aliyoshirikiana na Noorah.

Hata hivyo, kama walivyo wakongwe wengi, baada ya kukimbiza kwa muda, Rhyno alipotea kwenye gemu na akawa hasikiki kabisa. Hivi karibuni amerudi na ujio unaoitwa Panda Mnazi ambao video yake amefanya na Director Msafiri wa Kwetu Studio. Kwa nini alipotea pamoja na mengine mengi kuhusu muziki wake, anajibu kwenye makala hii;

 

Risasi: Kimya sana kaka!

Rhyno: Nipo, lakini kwenye muziki siyo kimya kiivyo maana mara kwa mara nimekuwa nikitoa ngoma sema ndo’ vile hazifiki mbali.

Risasi: Tofauti na huu ujio mpya mara ya mwisho umetoa ngoma lini?

Rhyno: Mwaka uliyopita na Jux.

Risasi: Ni kweli nakumbuka na umewahi kutoa pia kipindi cha nyuma, lakini kwa nini nyimbo hazifiki mbali na mashabiki wako hawakusikii kama ilivyokuwa zamani?

 

Ryno: Ninafikiri ni kwa sababu nilikuwa sitoi nyimbo pamoja na video. Ukitazama nyimbo zote nilizotoa miaka ya hivi karibuni nilikuwa sitoi video, ninahisi ndiyo maana sijapata nafasi kiivyo kwenye media.

Risasi: Kwa nini hutoi nyimbo pamoja na video wakati muziki ndiyo upo huko kwa sasa, tatizo mkwanja?

Rhyno: Tatizo siyo mkwanja. Kwa mfano huo wimbo nilioufanya na Jux nilishindwa kutoa pamoja na video kwa sababu Jux alikuwa bize na safari zake za nje. Hakuwa akipatikana kabisa.

 

Risasi: Mara ya mwisho kutoa wimbo pamoja na video ilikuwa mwaka gani?

Rhyno: 2015, wimbo unaitwa Taking Over na nilifanya video na Adam Juma (director). Miaka mitatu hivi imepita.

Risasi: Kwa sasa muziki wa HipHop unauzungumziaje kwenye suala la ushindani?

Rhyno: Ushindani umeongezeka siyo kama zamani. Kwa sasa kila nyumba Dar, kuna msanii. Na wasanii wenyewe kila mmoja anakomaa kuhakikisha anafanya poa, kwa hiyo ushindani ni mkali.

 

Risasi: Wanamuziki wakongwe kama wewe siku za hivi karibuni wamekuwa wakilalamika kwamba hawapewi nafasi kwenye vyombo vya habari, hili unalizungumziaje?

Rhyno: Ni kweli kinachosemwa. Hii inatokana na kwamba muziki umebadilika, unaangalia ladha na maneno ambayo yatakubalika mara moja hata kama ni kwa muda mfupi na si kama wanamuziki wengi walivyokuwa wanafanya zamani, kuimba nyimbo za meseji, jambo ambalo mpaka sasa wanataka kuendelea kulifanya.

 

Lakini ni vyema muziki wote ukapewa nafasi kwa sababu muziki wa aina zote una mashabiki.

Risasi: Jambo lingine lolote kwa mashabiki wako?

Rhyno: Waendelee kunipa sapoti hasa kwenye ujio wangu mpya wa Panda Mnazi, wafahamu kwamba nipo na nitazidi kuwepo.

Makala: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.