The House of Favourite Newspapers

Bobi Wine; Saa 240 za Machozi, Jasho na Damu

KWENYE Tasnia ya Muziki Uganda, majonzi yametawala kutokana na wakati mgumu aliopitia mwanamuziki Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’ kwa takriban siku 10 (saa 240) tangu akamatwe na kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi.

 

Ukitazama kwenye mitandao ya kijamii ya wanamuziki wengi nchini humo na mashabiki wa muziki utaona wameposti picha ya mwanamuziki huyo na kuandika ujumbe wenye ‘hashi tagi’ inayosomeka ‘Free Bobi Wine au ‘Release Bobi Wine’.

 

Wasomaji wengi wanaweza kuwa wanafahamu kilichompata mwanamuziki huyo mpaka kupitia wakati mgumu kiasi cha wanamuziki na mashabiki kuinuka sehemu tofautitofauti Afrika Mashariki kupaza sauti kwa ajili yake, kama hufahamu ungana nami hapa nitakueleza kwa kina!

 

ANUSURIKA KIFO

Bobi Wine alitiwa mbaroni Agosti 14, mwaka huu huko Kaskazini- Magharibi mwa Mji wa Arua, akihusishwa na shambulio la Rais Yoweri Museveni pamoja na kudaiwa kumiliki silaha za moto.

Bobi Wine alikamatwa pamoja na wanasiasa kadhaa wa upinzani na ndani ya siku mbili toka akamatwe watu takariban 68 walikuwa wamekamatwa pia.

Hata hivyo, kabla ya kukamatwa kwake, kupitia Mtandao wa Twitter muda mchache baada ya gari lake kushambuliwa na askari wa ulinzi aliandika kwenye Mtandao wa Twitter kwamba; “Dereva wangu ameuawa, walifikiri wamenipiga mimi lakini nipo hai!”

 

AWASIKITISHA WENGI

Baada ya kukamatwa Bobi Wine alipelekwa kuhifadhiwa kwenye selo ya kijeshi. Siku chache toka ahifadhiwe kwenye selo hiyo picha za kusikitisha zilianza kusambaa zikimuonyesha mwanamuziki huyo akiwa hatamaniki.

 

Uso umejaa manundu, mdomo umevimba na kiukweli alikuwa anasikitisha na mtu anayemfahamu akitazama picha hiyo inayosambaa kwa sasa anaweza kufikiri ni watu wawili tofauti.

 

MASTAA WAUNGANA KUMPIGANIA

Mastaa mbalimbali Afrika Mashariki wameungana kumpigania Bobi Wine ili aweze kauchiwa. Tukianza na hapa nyumbani mwanadada Lady Jaydee alifuta picha zake zote kwenye akaunti yake ya Instagram na kuposti picha moja tu ya Bobi Wine bila kuandika neno lolote lile.

 

Fid Q yeye aliandika; “Uganda” na kuweka alama ya ngumi. Mwanamuziki AY hakuwa nyuma, aliandika maneno haya; “Mganda wa kwanza kumjua kwenye maisha yangu” kisha akaweka alama za vidole viwili juu kama ile cha Chadema (Chama cha Maendeleo).

 

Wanamuziki wengine walioonyesha kuguswa na wakati mgumu anaopitia Bobi Wine ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini na Joseph Haule ‘Professor Jay’, Mbunge wa Mikumi.

Kwa upande wa Kenya, Prezzo yumo kwenye listi ya wanamuziki wanaompigania Bobi kupitia Instagram na kwa Uganda listi ndefu inaongozwa na mwanamuziki Juliana Kanyomozi ambaye ameposti mara kadhaa picha akiambatanisha ujumbe wa kumuombea kwa Mungu, Bobi Wine apite salama kwenye mtiti huu.

Mbali na hao, mastaa zaidi ya 80 Afrika wameonesha kuguswa na tukio hilo.

‘UBISHI’ WAKE WATAJWA KUMPONZA!

Mbali na sababu nyingi zinazotajwa kumfikisha kwenye masaibu haya Bobi Wine, ubishi wake pia unatajwa kumponza.

Bobi Wine ni mbishi kwelikweli hasa kwenye masuala anayoyaamini. Anaamini kwamba Waganda hawana uhuru na wanaishi enzi za utumwa.

 

Ukisikiliza wimbo wake uitwao Freedom utaelewa juu ya hili, namna alivyoichana Serikali yake katika nyanja mbalimbali. Kama haitoshi unaweza kusikiliza wimbo wake mwingine uitwao Situka ndiyo utamuelewa jamaa namna alivyo mbishi.

Lakini mbali na kutunishiana misuli kupitia muziki wake, Bobi Wine akiwa majukwaani amekuwa akimsema rais wake waziwazi katika masuala ambayo anahisi si sawa.

 

JUMUIYA YA MADOLA WATOA NENO

Kwa upande wa Jumuiya ya Madola, kupitia mwakilishi wake nchini Uganda wameonya kukamatwa kwa mara kwa mara kwa wanasiasa wa upinzani na kuongeza kwamba; “Kuna ongezeko kubwa la watu wanaoipinga Serikali, ambalo linaweza kusababisha machafuko ndani ya Uganda.”

 

MUSEVENI NAYE AIBUKA

Kwa upande wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, alikanusha taarifa za mateso za mwanamuziki huyo na alionya ‘media’ kuendelea kusambaza taarifa hizo.

Hata hivyo hadi Alhamisi iliyopita, Bobi Wine aliachiwa huru na Mahakama ya Kijeshi nchini humo baada ya kumuondolea mashtaka ya umiliki haramu wa silaha nchini kisha akakamatwa tena na kutakiwa kushtakiwa kwenye Mahakama ya Kiraia kwa kosa la uhaini pamoja na wabunge wengine waliokamatwa.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.