The House of Favourite Newspapers

 Bocco, Kagere Wapewa Maelekezo Maalum Lubumbashi

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, amefunguka kuwa amepanga kukaa na washambuliaji wake akiwemo Mnyarwanda, Meddie Kagere na John Bocco ili kuwapa mbinu za kupata mabao kwenye mechi yao ya ugenini dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

 

Simba imefuzu hatua ya robo fainali kwa rekodi ya kushinda mechi zake za nyumbani kutoka Kundi D huku ikifungwa mechi zote za ugenini bila kupata bao lolote katika mechi hizo.

 

Timu hiyo ilianza kufungwa na AS Vita ya DR Congo mabao 5-0 kisha ikafungwa tena kwa idadi hiyo na Al Ahly (5-0) kabla ya kufungwa na JS Saoura ya Algeria mabao 2-0. Simba inatarajiwa kucheza na TP Mazembe Aprili 5, mwaka huu katika mchezo wa kwanza utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kuelekea Lubumbashi nchini DR Congo kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa Aprili 12, mwaka huu.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems amekiri kukosa matokeo mazuri katika mechi za ugenini kwenye hatua ya makundi lakini amesisitiza kukaa na washambuliaji ili kutafuta dawa ya matokeo ya mechi za ugenini katika hatua ya robo fainali.

 

“Najua Mazembe ni timu kubwa lakini sasa ni mchezo wa KO, siyo kama tulivyokuwa kwenye makundi lazima tubadilike ili kuhakikisha tunafika sehemu nzuri kwa kuweza kupata matokeo ya ugenini jambo ambalo kwa sasa linahitaji maboresho.

 

“Lazima tukae na kuangalia pamoja na wachezaji na hasa washambuliaji kabla ya kwenda DR Congo katika mechi ya marudiano na kuona tumeufanyia kazi upungufu wote uliojitokeza kwenye mechi za makundi, hasa za ugenini ili kuona tunapiga hatua nyingine kubwa,” alisema Aussems.

IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam

Comments are closed.