The House of Favourite Newspapers

Bocco: Uturuki Kutatupa Kasi ya Ligi Kuu Bara

BAADA ya usiku wa kuamkia jana Jumapili, Simba kukwea pipa kuelekea nchini Uturuki kwa ajili ya kambi, nahodha wa kikosi hicho ambao ni mabingwa wa ligi kuu msimu uliopita, John Bocco ameweka wazi faida ya kambi hiyo.

 

Bocco alikuwa sehemu ya wachezaji ambao waliondoka na kikosi hicho cha Simba chini ya Kocha Patrick Aussems, raia wa Ubelgiji kuelekea Uturuki walipokwenda kuweka kambi ya wiki mbili kabla ya kurudi nchini Agosti 5, mwaka huu, kwa ajili ya Simba Day itakayofanyika, Agosti 8.

 

Mshambuliaji huyo ambaye ameibuka Mchezaji Bora wa Simba na Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2018/19 ameliambia Championi Jumatatu, kuwa kwake kama nahodha anafurahi kuona wanapata sehemu ya utulivu ya kuweka kambi ambayo itawajenga kisaikolojia kwa ajili ya kupambania kutwaa ubingwa wa ligi kwa msimu ujao.

 

“Msimu uliopita tulikuwa hapahapa Afrika na tukaenda Afrika Kusini kwa ajili ya kambi ya pre season, lakini kwa msimu huu tunaenda Ulaya katika nchi ya Uturuki, kwangu ni jambo zuri kwa sababu tunaenda kupata kitu kipya kabisa tofauti na kama tungebaki hapa nyumbani.

 

“Ninaamini hii itakuwa mwanzo mzuri kwetu kwa ajili ya kutetea ubingwa, unajua tukiwa huko tutapata nafasi zaidi ya kufikiria mazoezi na kuwa fiti zaidi kwa sababu tuko kwenye mazingira salama ambayo yanakufanya kama mchezaji kuwaza mazoezi pekee, hivyo hilo litakuwa jambo zuri kwetu kuelekea mapambano ya msimu ujao,” alisema Bocco.

Said Ally, Dar es Salaam

Comments are closed.