The House of Favourite Newspapers

Kipigo Cha Simba Kisiwapotezee Njia Yanga

Kikosi cha timu ya Yanga.

 

JUMAPILI iliyopita haikuwa siku nzuri kwa mashabiki, wachezaji, viongozi na wadau wa Yanga kutokana na kupoteza mchezo wa watani wao wa jadi, Simba kwa bao 1-0 katika Ligi Kuu Bara.

 

Hayakuwa matokeo mazuri kwa kuwa yalipunguza nguvu ya Yanga kuelekea mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo ambao kwa sasa unaonekana kuwa unaweza kutua mikononi mwa Simba.

 

Pamoja na hivyo, imekuwa kawaida mara nyingi kunapofanyika mchezo baina ya watani hao, inapotokea upande mmoja umepoteza mechi ni rahisi kuanza kusikia lawama na mwisho wake mara kadhaa zimesababisha kuibuka kwa migogoro.

Kikosi cha timu ya Simba

Kunapoibuka mgogoro hata kama ni mdogo ni rahisi kupoteza mwelekeo wa timu, kwa kuwa mara nyingi imekuwa ikiingia na kuathiri utendaji wa benchi la ufundi na wakati mwingine wachezaji.

 

 

Yanga bado inashiriki katika Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ni hatua kubwa na wao ndiyo wawakilishi pekee, hawatakiwi kugawanyika, ikitokea hivyo wajue kuwa ni mwanzo wa kujimaliza wenyewe.

 

Michuano hiyo ya kimataifa ina faida kubwa kwao kama klabu na hata katika nchi ya Tanzania kwa jumla, hawatakiwi kupoteza mwelekeo na kuzama kwenye migogoro ambayo haina faida, kufanya hivyo ni kutengeneza anguko baya hasa kipindi hiki ambapo timu yao ipo katika wakati mgumu kifedha.

 

Matokeo ya Simba yachukuliwe kama mchezo mwingine, changamoto zipo kila siku lakini hawatakiwi kupoteza ramani yao inayowapeleka sehemu nzuri.

Bodi ya Uhariri/ Maoni, Championi

Comments are closed.