Breaking News: Rais Bush wa Marekani Afariki Dunia

RAIS wa 41 wa Marekani, George Herbert Walker Bush,  amefariki dunia jana, Ijumaa, Novemba 30, 2018, majira ya saa 4:10 usiku mjini Houston akiwa na umri wa miaka 94, msemaji wake Jim McGrath amethibitisha kifo chake na kusema chanzo chake kimetokana na tatizo la mapafu (pneumonia) lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu.

 

Shujaa huyo wa Vita vya Pili vya Dunia ambaye alizaliwa Juni 12, 1924, ni rais aliyeongoza kwa awamu moja tu akiingia madarakani mwaka 1989 na kuondoka 1993 hivyo kubaki kama rais pekee aliyeiongoza Marekani kwa awamu moja.

 

Bush ambaye pia ni babaye rais wa 43 wa Marekani, George W Bush, amewahi kuwa rubani katika Jeshi la Marekani, Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Makamu wa Rais.

 

Mzee Bush amefariki ikiwa ni miezi saba tu tangu kifo cha aliyekuwa mkewe, Barbara Bush ambaye alifariki dunia Aprili 17, 2018, huko Huston akiwa na umri wa miaka 73.

 

Kwa upande wa siasa za nje, matukio makubwa yaliyofanyika duniani wakati wa utawala wake ni pamoja na kuanzishwa kwa Vita vya Ghuba, kuanguka kwa Ukuta wa Berlin (nchini Ujerumani) na kuvunjika kwa Muungano wa Kisoviet.

 

Mambo mengine yaliyofanyika nchini Marekani chini yake ni pamoja na kupigwa marufuku kwa uingizaji wa  bunduki za ‘semi-automatic’ nchini humo na kusainiwakwa  Sheria ya 1990 ya Wamarekani wenye Ulemevu na ya 1991 ya Haki za Kiraia.

 

Hata hivyo, pamoja na kusema wakati wa kampeni za kuchaguliwa kwake kwamba hapangekuwa na kodi mpya wakati wa utawala wake, jambo hilo hakulifanya.

 

Baba yake George, aliyeitwa Prescott, alikuwa seneta, na mwanaye mkubwa wa kiume, akawa rais wa 43 wa Marekani.

 

Ameacha watoto watano, wajukuu 17 na vitukuu wanane.  Pia alikuwa na binti aliyeitwa Robin ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka mitatu kutokana na kansa ya damu.

Toa comment