The House of Favourite Newspapers

Chirwa Awakosesha Wenzie Mamilioni

Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa.

PENALTI ya mwisho ya mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa ambaye mitaani wamempachika jina la Bwana Shamba, imewakosesha Sh10 milioni wachezaji wa timu hiyo walizoahidiwa na mabosi wao.

 

Yanga waliahidiwa fungu hilo endapo wangetwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.

Jumatano wiki hii, Yanga iliondolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa na URA ya Uganda kwa penalti 5-4 baada ya kutoka suluhu katika nusu fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

 

Katika penalti waliopata kwa upande wa Yanga ni Raphael Daudi, Gadiel Michael, Hassan Kessy na Papy Kabamba Tshishimbi, lakini Chirwa raia wa Zambia ambaye alichelewa kujiunga na timu huku akionekana akilima kwao, yeye alikosa.

 

Habari za uhakika ambazo Championi Jumamosi imezipata, mabosi hao wa Yanga walikutana na wachezaji kabla ya mchezo na kuwaahidi kuwapa fedha zote za zawadi ya ubingwa wa michuano hiyo ambayo ni Sh10 milioni.

Mabosi hao walitoa ahadi hiyo ya kuwapa wachezaji fedha hizo kwa ajili ya kuwaongezea morali ili wacheze kwa kujituma na kutwaa ubingwa huo.

 

Bosi mmoja alisema kikubwa wanachofurahia ni kiwango cha wachezaji walichoonyesha katika michuano hiyo wakiwemo Said Makapu na kipa chipukizi, Ramadhani Kabwili.

 

Alipotafutwa nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuthibitisha hilo alisema; “Mara nyingi tumekuwa tukipewa ahadi ya fedha katika mechi ngumu na muhimu kama hiyo dhidi ya URA.

 

“Ni kawaida yetu na nisingependa kusema ahadi ipi ya fedha tuliyoahidiwa, lakini kama wachezaji tuliahidiwa na hiyo yote ni katika kuleta morali ya timu.”

Stori: Wilbert Molandi

Comments are closed.