The House of Favourite Newspapers

DENTI ALIYEFIA SHULENI… UTATA MZITO WAIBUK A

INAUMA sana! Ndiyo maneno yanayoweza kukutoka kufuatia kuibuka kwa simulizi yenye utata mzito kuhusiana na kifo cha binti, Faith John Mutalemo, Mkazi wa Pugu-Mnadanai jijini Dar aliyefia shuleni.

Faith anadaiwa kujinyonga hadi kufa akiwa bwenini katika Shule ya Sekondari ya St. Anne Marie iliyopo Mbezi Kwa-Msuguri jijini Dar.

Akisimulia tukio hilo la lenye kukutoa machozi, shemeji wa marehemu aitwaye Ditrick ambaye ndiye mtu wa kwanza kupewa taarifa za kifo cha binti huyo alisema kuwa, ilikuwa usiku wa kuamkia Mei 2, mwaka huu, majira ya saa kumi za alfajiri ndipo alipopigiwa simu na mdogo wake aitwaye Octavian ambaye ni mwalimu katika shule hiyo, lakini tawi lingine.

TAARIFA ZA KUSHTUA

“Nilishtushwa na simu ya usiku namna ile, nikaipokea, nilipoanza kuzungumza na mdogo wangu, aliniambia kwamba mkuu wa shule anayosoma Faith, Gradius Dyetabula alimpigia simu na kumuuliza juu ya mahali anapoishi Faith.

“Mdogo wangu alisema alimuelekeza, lakini alibaki na wasiwasi kwamba alikuwa anarudishwa nyumbani pengine kuna jambo kubwa amefanya. Lakini tuliulizana hata kama kuna jambo kafanya inawezekanaje arudishwe usiku ule wakati ni mwanafunzi anayeishi bweni, si anaweza kulala halafu siku inayofuata akarudishwa?

“Au kama ni mgonjwa, kwa nini isingeelezwa wazi? Maswali yalikuwa ni mengi, lakini tuliamua kuvuta subira kwa sababu mkuu yule wa shule alimwambia angempigia tena,” alisimulia Ditrick.

Shemeji huyo aliendelea kusimulia kwamba, anafahamiana pia na mkuu wa shule hiyo, kwa hiyo majira ya saa 11:00 alfajiri mkuu huyo alimpigia simu na kumweleza kwamba Faith alikuwa amefariki dunia na alikutwa akiwa amejinyonga bwenini kwa kutumia neti.

“Nilimuuliza sababu za kujinyonga, akanieleza kwamba kabla ya tukio hilo mapema siku hiyo, alidaiwa kuiba ufunguo wa mwanafunzi mwenzake, lakini pia alimpiga mwanafunzi huyo kiasi kwamba alipelekwa kwenye Hospitali ya Bochi (Mbezi).

“Baada ya hapo alinieleza kwamba Faith alikataa kulala bwenini, ikabidi matroni ampigie simu yeye mkuu wa shule, akaongea na Faith na kumuomba alale kwa matroni na siku iliyofuata wangezungumza zaidi kilichotokea.

“Mkuu wa shule alinieleza kwamba walikubaliana na Faith, akaenda kulala kwa matroni aliyekuwa karibu na shule hiyo, lakini usiku alitoroka na kwenda kujinyonga bwenini.

“Nilimuuliza alitumia nini kujinyonga? Aliniambia alitumia neti aliyoichomeka kwenye tundu lililokuwa kwenye ‘siling boad.’ Kwa hiyo nikaamua kumpa taarifa baba wa Faith, tukakutana na kwenda shuleni.

WAKUTA MWILI UMEONDOLEWA

“Baada ya kufika shuleni, tulimkuta mlinzi aliyekuwepo usiku huo, matroni na mkuu wa shule. Tukauliza mwili upo wapi? Wakatuambia Polisi walifika na kuupeleka Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila.

“Kwa kuwa pale shuleni kuna ndugu kadhaa wa Faith akiwemo shemeji yake anayesoma kidato cha sita na ndugu yake mwingine anayesoma kidato cha tano, tukauliza kama waliitwa kumshuhudia ndugu yao, lakini mkuu wa shule alisema hawakuwaitwa.

“Tuliomba kupelekwa kwenye chumba ambacho Faith alijinyongea, lakini jambo la kushangaza hatukukuta siling boad kama tulivyoambiwa mwanzo wala tundu, tukaona huu ni utata.

“Juu kulikuwa na kenchi, tukaambiwa alijinyongea hapo!

“Tulikwenda hadi Kituo cha Polisi Mbezi-Luis, tukaomba maelezo, askari tuliowakuta walisema kweli waliutoa mwili wa marehemu na waliupeleka hospitali.

“Tukaomba picha za eneo la tukio, lakini polisi walisema hawakupiga kwani kulikuwa na giza!

“Kwetu jambo hili lilitushangaza kwa sababu mtu akijinyonga, utaratibu ni kwamba mwili ukiwa unatolewa ni sharti ndugu washuhudie au picha za eneo la tukio zipigwe.

Kama mtu alikuwa amekwikufa kulikuwa na uharaka gani wa kuutoa mwili? Huu ni utata mwingine!” Alisema shemeji huo.

Aliendelea kusimulia kwamba, walikwenda hadi hospitalini kuangalia mwili wa marehemu na walikuta kweli ni wa Faith. Baada ya siku tatu waliuchukua mwili na kwenda kuufanyia uchunguzi Muhimbili kisha kupanga siku kwa ajili ya mazishi.

SHULENI WAINGIA MITINI

“Siku ya mazishi tuliomba magari shuleni ya kutusaidia kwenye mazishi na tukamweleza mkuu wa shule awaeleze wanafunzi wenzake waje wahudhurie mazishi, lakini yalikuja magari matupu, hakuna hata mwanafunzi mmoja aliyefika. Hili lilitushangaza, wanafunzi pekee waliofika msibani ni kutoka shule aliyokuwa akisoma Faith awali ya High Mount kwani hapo St. Anne Marie alihamia akiwa kidato cha tatu.

“Baada ya mazishi tulikwenda shuleni kufuata vitu vya marehemu, lakini wakati vitu vinatolewa wanafunzi walikuwa wakishangaa na kuuliza kama Faith harudi, tukafahamu kwamba walikuwa hawafahamu na tulipowaeleza juu ya taarifa za kifo chake walianza kulia. Hili nalo lilitushangaza kwani vilio vilitawala shuleni.

“Ile ni shule ya bweni, majira ya kuanzia saa kumi watoto huamka kwa ajili ya kujisomea, kweli kama tukio lilikuwepo shuleni hapo, hakuna hata mtoto mmoja aliona? Wala kuona gari la polisi? Kuna utata kwenye msiba huu kwa kweli,” alisema Ditrick.

MSIKIE MAMA WA MAREHEMU

Kwa upande wa mama wa marehemu, Agness Shirima alipozungumza na Ijumaa Wikenda juu ya kifo hicho alisema kwamba mpaka sasa haelewi nini kilimpata mwanaye.

Mama huyo akizungumza kwa majonzi alitoa neno zito kwamba, taarifa za kifo zinaonekana kutonyooka na kwamba shule ilipaswa kuwapa ushirikiano wa kusema ukweli wa nini hasa kimetokea, kwani hata waliporudi tena polisi baada ya kituo kuhamishiwa Kiluvya, walisema kwamba hawana taarifa juu ya tukio hilo, jambo lililowashangaza.

“Kiukweli mwanangu ameondoka bado mdogo sana, kinachonisikitisha zaidi ni taarifa za kifo chake. Polisi wanasema hawana taarifa tena, majibu ya vipimo vya uchunguzi yapo Muhimbili na hakuna aliyeyafuatilia, kweli hapa kuna nini kimejificha kwenye kifo cha Faith?” Alihoji mama huyo.

MKUU WA SHULE

Ijumaa Wikenda lilimtafuta mkuu wa shule hiyo ambaye baada ya kuelezwa tukio zima alidai hafahamu lolote na kuna taarifa nyingi zinapikwa mitandao.

“Kiukweli sina taarifa zozote ninazofahamu, unajua kuna taarifa nyingi zinapikwa kwenye mitandao juu yetu, kwa hiyo sijui lolote,” alisema.

KAMANDA WA POLISI

Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP Jumanne Muliro hazikuzaa matunda hivyo zinaendelea ili kujua ukweli juu ya sakata la kifo cha Faith.

 

Stori: Boniphace Ngumije, Dar

Comments are closed.