DEREVA BAJAJ YAMFIKA MAZITO!

DEREVA wa Bajaj aliyefahamika kwa jina la Noel Razaro (30) kutoka Mtwara yamemfika mazito baada ya kupata ajali mbaya iliyomsababishia kupooza kuanzia kiunoni kwenda chini. 

 

Akizungumza na Gazeti la Uwazi hivi karibuni, Razaro alisema alipata ajali hiyo miaka mitano iliyopita wakati akiendesha Bajaji eneo linaloitwa Mkoani huko Mtwara Mjini. Akisimulia ajali hiyo ilivyokuwa, kijana huyo ambaye sasa hivi anaishi kwenye mateso makubwa alisema:

 

“Siku hiyo ilikuwa usiku, nikakutana na gari ambalo lilikuwa limewasha taa zote full, mazingira hayo yalinifanya nishindwe kuendesha na kusimama, gari hilo likanifikia na kunigonga. “Hapo hapo nilizimika na kuja kuzinduka nikiwa katika Hosptali ya Ligula.

 

Baada ya kuwepo hospitalini kwa siku 5, nikahamishiwa Hospitali ya Muhimbili ambako nilifanyiwa upasuaji na kuwekewa vyuma. “Nilikaa hospitalini hapo kwa mwezi moja kisha nikaruhusiwa kurudi nyumbani ila nikawa natakiwa niwe nakwenda kufanya mazoezi katika Hospitali ya Ligula lakini nilishindwa kutokana na kukosa pesa.

 

“Baada ya kuona ahueni kidogo, nikarudi Muhimbili na kutolewa vyuma ila kusema ukweli hali yangu haijakaa sawa, bado vidonda vinanisumbua na hata mipira ninayowekewa kwa ajili ya mkojo nashindwa kuibadilisha kwa wakati kutokana kukosa pesa.

 

“Baba yangu ni mzee, mama alishafariki sasa nakutana na hali ngumu kupita maelezo. Nalala tu mpaka vidonda vikubwa vimetoka makalioni. Yaani najiona nakufa hivi hivi kwa umasikini kwa maana hata chakula naweza kukaa siku mbili sijala chochote, nateseka sana jamani,” alisema kijana huyo huku akitokwa na machozi.

 

Mpenzi msomaji, Razaro yuko kwenye kipindi kigumu sana, anahitaji msaada hivyo kama umeguswa na ungependa kumsaidia kwa chochote, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba yake ya simu 0676299025. Kumbuka kutoa ni moyo na si utajiri.


Loading...

Toa comment