The House of Favourite Newspapers

Diamond Anavyotumia Fursa kwa Wapenzi Wake

Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’

AKILI ni nywele, kila mtu ana zake! Unaweza kuitumia methali hiyo kutokana na staa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kuwa na staili ya tofauti na mastaa wengine katika kazi zake, staili ambayo imekuwa ikimpa mafanikio kimuziki kwani hutumia fursa ya kuwashirikisha wapenzi wake zaidi.

 

Diamond, katika nyimbo na video zake nyingi amekuwa akiwatumia warembo ambao anatoka nao kimapenzi, yaani wapenzi wake ambao kwa wakati husika wanakuwa ni kivutio na gumzo kwa mashabiki wake wengi, hali ambayo humuongezea watu kibao wanaoshabikia kazi zake.

 

Hii naweza nikasema ni akili ya tofauti kwani kwa hapa Bongo msanii anayeongoza kwa kuwaimba au kuwashirikisha wapenzi wake kwenye kazi zake ni Diamond na staili hii ya tofauti imekuwa ikizidi kumwongezea umaarufu na kipato pia kwani kutokana na nyimbo hizo, hujikuta akipata shoo nyingi ndani na nje ya Bongo.

 

NINI SIRI?

Wajuzi wa mambo wanaeleza kwamba, Diamond amekuwa akiwashirikisha warembo hao kwenye nyimbo zake kwanza, ili nyimbo zake ‘zi-hit’ maana wengi wao ni maarufu. Pili ni wapenzi wake hivyo anawalipa fedha kidogo au hawalipi kabisa. Katika makala haya tunakuletea baadhi ya warembo ambao wamewahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Diamond na kujikuta wakishiriki kwenye kazi zake za kimuziki.

HAWA WA NITAREJEA

Huyu ni mwanamama ambaye alishiriki kwenye moja ya video za mwanzomwanzo kabisa za Diamond iliyokwenda kwa jina la Nitarejea. Hawa wa Nitarejea aliwahi kukiri kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Diamond, lakini baada ya kuwa maarufu alimsahau huku akiwa tayari ameshamtajirisha kimaisha na kimuziki.

NATASHA MOYO WANGU

Mwanamuziki Diamond alimtumia kama video queen kwenye Wimbo wa Moyo Wangu ambapo aliingia naye kwenye uhusiano. Natasha aliwahi kukiri kutoka kimapenzi na Diamond, lakini mwanamuziki huyo alichomoa na kusema siyo kweli.

WEMA SEPETU

Mrembo huyu anayefanya vizuri kwenye sanaa ya filamu Bongo, amewahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Diamond, lakini wakaachana.

Wakiwa kwenye uhusiano wa kimapenzi, Diamond alijiongeza kiakili na alitumia nafasi hiyo sawasawa baada ya kumuimba na ‘kumdis’ kwenye wimbo wake wa Nimpende Nani.

Kutokana na kumuimba huko, wimbo huo ulipata umaarufu kila kona na ulikuwa ukizungumziwa jinsi alivyomuimba vibaya aliyekuwa mpenzi wake huyo.

HAMISA MOBETO

Diamond alimtumia mwanamitindo huyu maarufu Bongo kwenye video ya Wimbo wa Salome na baada ya video hii ndiyo ilizaa matunda kwani mwanamama huyo alifanikiwa kupata ujauzito wa msanii huyo na kuzaa mtoto anayejulikana kwa jina la Abdul Nasibu ‘Dylan’.

Mpaka sasa wawili hawa wanaendelea kumlea mtoto wao ikiwa ni baada ya Mobeto kutinga mahakamani kudai fedha za matunzo kwa Diamond licha ya hivi karibuni kuzuka kwa sintofahamu baada ya familia kuonekana kwamba wanamtaka Zarinah Hassan ambaye pia ni mzazi mwenza wa Diamond.

ZARINAH HASSAN

Mwanamama huyo ambaye ni mjasiriamali kutoka nchini Uganda, amefanikiwa kupata watoto wawili na Diamond ambapo uhusiano wao wa kimapenzi ulipata umaarufu wa aina yake kabla ya baadaye kuvunjika kutokana na Mobeto kudaiwa kuingilia penzi lao hilo.

Wakati Diamond akiwa kwenye uhusiano na Zari aliweza kumshirikisha kwenye video ya Wimbo wa Iyena ambao ndiyo habari ya mjini kwa sasa.

 

Zari amenogesha sana kwenye video hii hali iliyosababisha kupata wafuasi wengi wanaoiangalia na kuipenda kwenye mitandao ya kijamii. Video hii imezua kizaazaa kwani familia imeibuka na kueleza kwamba wanamtaka Zari na meneja wa Diamond, Babu Tale aliamua kuchukua hatua ya kumfuata mwanamama huyo Sauz kwa ajili ya kumuomba msamaha ili arudiane na Diamond.

MAKALA: GLADNESS MALLYA, DAR

Comments are closed.