DJ Kidato cha Tatu Auawa kwa Kupiga Muziki ‘Mbaya’ Ukumbini

MCHEZESHAJI muziki nchini Uganda (DJ) amepatwa na mauti baada ya kuvamiwa na kundi la vijana waliompiga kwa kosa la kuweka wimbo ambao hawakuupenda walipokuwa wanacheza  kwenye ukumbi mmoja uliopo wilayani Nebbi, Mkoa wa Kaskazini, Uganda.

 

DJ Jerry Okirwoth ambaye alikuwa  mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Parombo, alikuwa ameshikilia kazi ya u-DJ kwa muda  usiku baada ya masomo yake ili kujipatia kipato cha kumudu mahitaji yake ya shule kufuatia DJ wa muziki huo kuwa likizo.

 

Kamishna wa Polisi wa Wilaya ya Nebbi, William Bob Labeja,  amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, ambapo amesema mwanafunzi huyo aliuawa siku ya Jumatano. Labeja ameulaumu uongozi wa ukumbi uliotumiwa na wauaji hao kwa kushindwa kumlinda marehemu kabla hajapatwa na mauti.

 

“Mimi kama Mkurugenzi Mkuu wa Usalama katika Wilaya hii, sitakubali disko zozote kufanyika usiku katika eneo hili, na yule atakayekiuka tutachukua hatua kali za sheria. Nazitaka kumbi zote zifungwe kwani zimekuwa hatari kwa maisha ya vijana,” amesema Bob Labeja.

 

Labeja pia alisema uchunguzi umeanzishwa ili kuwakamata waliohusika katika kumshambulia DJ huyo na kusababisha kifo chake.

 

Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa eneo hilo, Bosco Okwai,  amesema kuwa mwaka 2011 walitengeneza sheria inayozuia vibali vya kuendesha kumbi za muziki na amewataka viongozi wote wa mitaa kuhakikisha wanawapeleka mbele ya sheria watu wote watakaoipuuza sheria hiyo.

Loading...

Toa comment