‘Dudu la Yuyu’ Lampa Dili Baba Diamond

DAR ES SALAAM: AMA kweli Mungu akitaka kukupa hakuandikii barua! Baada tu ya kuuza sura kwenye wimbo wa Umeniteka ‘Dudu la Yuyu’ baba wa msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Abdul Juma ameanza kudaka madili chungu mbovu!

 

Wikiendi iliyopita Ijumaa Wikienda lilimtembelea baba Diamond nyumbani kwake Magomeni-Kagera jijini Dar ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia kuhusu madili mbalimbali yaliyojitokeza baada tu ya yeye kuonekana katika wimbo huo.

 

Alisema licha ya kuwa tayari yeye alikuwa maarufu kabla ya wimbo huo kutoka lakini amejikuta akiwa maarufu zaidi na kulamba madili ya hela na wengine wakitaka kufanya naye kazi.

“Kama unavyojua mimi ni maarufu kitambo hasa kutokana na mwanangu Diamond kufanya vizuri katika muziki kwa muda mrefu lakini kuna watu wameongezeka kunifuatilia baada ya tu ya kuonekana kwenye video,” alisema baba Diamond.

 

Baba Diamond alisema wimbo huo umemfanya agombewe hadi na wasanii wakubwa ambao hata yeye hakutegemea kama wanaweza kumuomba kolabo.

“Huwezi amini tayari mastaa wakubwa tu acha nisiwataje majina lakini wametaka kufanya kolabo na mimi, kuna wengine wamenipa mialiko ya shoo, kuna wengine wananihitaji kwa matangazo, siwezi kutaja gharama zangu ila anayetaka anaweza kunitafuta,” alisema.

 

Baba Diamond alisema anamshukuru Mungu kwa hatua aliyoifikia japo muziki haukuwa kwenye malengo yake lakini amegundua kwamba unaweza kumpa madili mengi hivyo ataendelea kuufanya.

Stori: Erick Evarist, Ijumaa Wikienda


Loading...

Toa comment