The House of Favourite Newspapers

DUH! HAMISA MOBETO MBISHI AISEE!

“HIVI huyu naye anaimba vitu gani? Wewe hujui kuimba bora utafute kazi nyingine ya kufanya!” Haya ni maneno yaliyozoeleka kwa andagraundi wengi wanaotafuta kutoka kwenye muziki huu wa Bongo Fleva yakilenga kuwakatisha tamaa.

“Nilishiriki BSS (Bongo Star Search) nikaambiwa sijui kuimba, lakini mimi moyoni mwangu nilikuwa nasema nina kitu fulani.

 

Sikukata tamaa. Nikaendelea kufanya muziki mzuri na kweli Mungu ameniona sasa hivi nimesikika,” anasema Harmonize ambaye ni staa mkubwa kwa sasa kwenye Bongo Fleva.

“Nilikw-enda na mama yangu kwa jamaa mmoja kumuomba anisimamie kwenye muziki, jamaa aliponisikiliza alisema sijui kuimba,” anasema staa mkuwa wa kimataifa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz.

 

“Baada ya kutoa Ngoma ya Nainai niliumiza sana kichwa nitatokaje na ngoma itakayoifikia au kuipita Nainai, nikarekodi Ngoma ya Baadaye, nilipokwenda pale THT (Tanzania House of Talent) na kuwasikilizisha washikaji, kila mtu aliniambia hakuna kitu na Ngoma ya Baadaye haitafanya poa. Namshukuru Mungu alitokea Ruge (Mutahaba enzi za uhai wake), nikamwambia bosi nina ngoma mpya naomba uisikilize, akaisikiliza, akaniambia ni bonge la ngoma na kweli Baadaye ikawa bonge la ngoma,” anasema Ommy Dimpoz, staa mwingine mkubwa wa Bongo Fleva.

 

“Nilikwenda na CD kwa Ruge, nikamsikilizisha wimbo wangu wa kwanza, nakumbuka aliivunjavunja ile CD, najua hakufanya kwa ubaya, lakini sikukata tamaa,” anasema Nandy, mmoja wa wanamuziki wa kike wa Bongo Fleva wanaofanya poa kwa sasa.

Mbali na hao wapo wasanii wengi kwenye muziki huu wa Bongo Fleva ambao nao walikatishwa mno tamaa kuwa hawajui kuimba, lakini hawakukata tamaa na leo wanasikika na kufanya poa. Wasanii kama Shilole, Gigy Money, Amber Lulu, Lulu Diva, Snura na wengine ni miongoni mwa wale walioambiwa hawawezi, lakini wakatoboa.

 

NI ZAMU YA MOBETO

Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia nguvu kubwa mno kumkatisha tamaa Hamisa Mobeto, ua jipya kwenye Bongo Fleva tangu alipoanza kuimba mwaka jana.

Tayari mkononi Mobeto ana ngoma kadhaa zikiwemo Madam Hero, Tunaendana, Sawa na My Love ambayo wiki iliyopita ilimfanya kujimilikisha Mtandao wa YouTube kwa saa kadhaa baada kushika namba moja. Mbali na muziki, Mobeto ni modo, fashenista, video queen na mwigizaji wa Bongo Movies.

 

Wanaombeza Mobeto wanasema hajui kuimba, hana sauti ya kuwaimbia watu, labda anajiimbie mwenyewe.

Wapo waliokwenda mbali zaidi na kumshauri Mobeto aache kufanya muziki kwani hajui kabisa kuimba, badala yake ajikite kwenye mitindo kwa kile wanachodai anafaa zaidi kufanya shughuli hizo kuliko muziki.

 

Wapo wanaomsisitiza kuwa wanaomsifia wanamdanganya kwa kupenda achoreke kwani anaimba kama yupo kwenye maombolezo na kama kweli anataka kuimba, basi afanye mazoezi ya kufa mtu.

Lakini Mobeto amekataa kusikiliza kelele hizo za kukatishwa tamaa. Ameamua kuwa mbishi kinoma aisee! Ameamua kuziba masikio na kujitafutia mashabiki wake wa muziki bila kujali watu wanasema nini.

 

Mobeto ameamua kuwa mbishi kwa sababu anajua Beyonce Knowles aliambiwa hajui kuimba. Leo ni mwimbaji tajiri anayeheshimika mno duniani.

Mobeto anajua Oprah Winfrey aliambiwa hafai kuwa mtangazaji kwenye televisheni, lakini ndiye mtangazaji wa televisheni mwenye mkwanja zaidi duniani.

 

Mobeto anakomaa kwa sababu anafahamu Steven Spielberg alikataliwa na chuo cha sanaa za uigizaji mara tatu kwa sababu ya ufaulu mdogo. Leo ni mmoja kati ya mada-irekta wenye tuzo nyingi na heshima kubwa duniani.

Mwana-mama Mobeto hataki kukubali kukata tamaa kwa sababu anajua Albert Einstein alia-mbiwa ni zuzu na yupo slow kwe-nye kujif-unza. Dunia inam-kumbuka kama binadamu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri kuwahi kuishi duniani.

 

Mbali na hao, Mobeto pia anajua Ludwig van Beethoven aliambiwa hakuna matumaini ya yeye kuja kuwa mtaalam za muziki, lakini anatambulika kama genius wa muziki kuwahi kutokea duniani.

Anachopaswa Mobeto kukijua ni kuendelea kukomaa hivyohivyo kwani dunia ina kawaida ya kulijaribu kusudio la mtu kama ni la kweli au la! Dunia inataka wabishi wanaokomaa na ndoto zao hadi wanatoboa.

 

Waliyoyapitia walioshinda kukatishwa tamaa yangetosha kuwarudisha nyuma wakaamua kufanya vitu vingine ila hapana, waliamini katika kile walichokitaka kiasi kwamba ilikuwa haiwezekani kuwarudisha nyuma hata katika nyakati ngumu.

Songa mbele Mobeto, amini unaweza, simama na unachokiamini. Go Mobeto!

MAKALA: Sifael Paul

Comments are closed.