Funga Mtaa, Mke Atumia Mdundiko Kumtoa Mumewe Kwa Mchepuko Wake

DAR ES SALAAM: MAISHA ya uswahilini raha sana jamani! Mambo yalikuwa burudani kwenye sherehe iliyofunga Mtaa wa Bi. Ndege uliopo maeneo ya Hananasif, Kinondoni jijini Dar iliyoandaliwa na mwanamke aitwaye Mama Abdul ikiwa ni staili aliyoitumia kumtoa na kumkaribisha mumewe aliyekuwa ‘ametekwa’ na mchepuko. 

 

Mwanamke huyo ambaye ni mke halali wa mwanaume aitwaye Hamis aliishi kwenye ndoa kwa raha mustarehe kwa miaka saba ambapo kuna wakati Hamis alitoweka kwa mkewe na kwenda ‘kufichwa’ na hawara aitwaye Joha anayeishi maeneo ya Kinondoni.

 

KISIKIE CHANZO KWANZA

Akizungumza na Amani hivi karibuni, mmoja wa mashosti wa mama Abdul aliyejitambulisha kwa jina la Salma alisema: “Rafiki yangu ameandaa bonge la sherehe pale Mtaa wa Bi. Ndege, ni baada ya kufanikiwa kumtoa muwewe kutoka kwa hawara ambako ameishi kwa mwaka mmoja na nusu.

 

“Baada ya kufanikisha zoezi hilo, ameita kigoma na muziki wa taarabu utafungwa siku hiyo hivyo kama vipi mje mchukue habari maana siku hiyo patakuwa hapatoshi,” alisema mtoa habari huyo.

SIKU YA TUKIO SASA

Juzikati paparazi wa Amani alikuwa mmoja wa watu waliotinga katika Mtaa wa Bi. Ndege na kushuhudia umati wa wanawake wakiwa wamevalia sare, wakirusha vijembe kwa mwanamke waliyemtaja kuwa ni mchepuko wa mume wa shoga yao aliyekuwa amemfungia ndani.

 

Wakati mambo yakizidi kupamba moto, ghafla walitokea wanaume wakipiga ngoma na matarumbeta hivyo kunogesha tukio hilo lililokuwa na lengo la kumpokea mume baada ya kurejea kutoka kwa hawara.

“Kiko wapiiiii, mume karudi kwa mkewe sasa, yule mchepuko aliyekuwa akitamba kwamba amemshika mume wa mtu na hawezi kuachika, kiko wapi sasa, warureeee,” alisikika akisema mmoja wa wanawake aliyejitambulisha kwa jina la Fauzia Mcharo huku akiungwa mkono na wenzake.

 

Hata hivyo baada ya mambo kunoga, wanawake hao wakiongozwa na mwenye mume walianza safari kuzunguka mitaa mbalimbali ya Kinondoni huku wakiendeleza vijembe, jambo  lililowashangaza wengi. Akizungumza na paparazi wetu, mke huyo, alisema: “Kwa kweli nimevumilia sana, mume wangu tulikuwa tunapendana, tumeishi muda mrefu lakini yule mwanamke sijui alimfanya nini, akamchukua na kwenda kuishi naye. Nikabaki na maumivu makali moyoni.

 

“Kilichoniumiza zaidi ni kwamba, huyu hawara alikuwa akija hapa ninapoishi na kunipa maneno ya shombo, eti yeye mzuri sana na mume wangu hawezi kumuacha, kuna wakati tulipigana mpaka kupelekana polisi.

 

“Cha kushukuru nilikuwa na moyo wa ustahimilivu, nikamuomba Mungu na hatimaye nimefanikiwa kumrudisha mume wangu, kwa kweli ninayo furaha kubwa sana na ndiyo maana nimeandaa sherehe hii. “Hapa tutakunywa, tukakula nyama choma pamoja na kucheza muziki na marafiki zangu maana haikuwa kazi rahisi.”

MUME NAYE AFUNGUKA

Akizungumzia kilichomfanya atoke kwa mkewe, Hamis alisema alihadaika tu, akajikuta ameshawishika kutoka nje ya ndoa, jambo ambalo analijutia.

“Kwa kweli siwezi kusema kwa nini nilimsaliti mke wangu lakini niseme tu kwamba, najutia kosa, nimerudi kwa mke wangu tumlee mtoto wetu. Huko nilikokuwa nimejifunza mengi, nimegundua nilikuwa nimepotea ila yote kwa yote nimerudi kwa mke wangu kipenzi,” alisema mwanaume huyo.

Loading...

Toa comment