
DAR: Kufuatia ajali ya ndege ndogo ya Shirika la Auric Air iliyotokea Jumatatu ya Septemba 23 na kusababisha vifo vya watu wawili, akiwemo Nelson Mabeyo ambaye ni mtoto wa Mkuu wa majeshi ya Ulinzi nchini (CDF) Venance Mabeyo, giza nene limetanda kutokana na mfululizo wa ajali za ndege ndogo zinazoendelea kutokea nchini.
Ajali iliyochukua uhai wa mtoto wa Mabeyo, Nelson aliyekuwa rubani wa ndege hiyo ndogo na mwenzake Nelson Orutu aliyekuwa katika mafunzo ya urubani, imetokea zikiwa zimepita wiki kadhaa tangu kutokea kwa ajali nyingine mbili, ambazo nazo zilihusisha ndege ndogo na kusababisha vifo vya raia wawili wa Afrika Kusini.
MAZINGIRA YA AJALI ILIYOMUUA NELSON
Ajali iliyogharimu maisha ya Nelson na mwenzake, imetokea katika uwanja mdogo wa ndege eneo la Seronera ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti majira ya saa 1:30 asubuhi, huku taarifa zikieleza kwamba ilikuwa ikiruka kutoka Serengeti kwenda Arusha baada ya kuwashusha watalii.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Kampuni ya Auric, Peter Kimaro, baada ya ndege hiyo kuhakikiwa na kuonekana ipo sawa, iliruhusiwa kupaa lakini baada ya kushika mwendo na kupaa, badala ya kunyooka ndege hiyo ilikata kona na kuanza kuyumba kabla ya kugonga paa la choo cha uwanja na kulipuka.
Kwa nyakati tofauti, Rais Dk. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, walifika nyumbani kwa CDF Mabeyo kwa ajili ya kuifariji familia hiyo iliyokumbwa na majonzi mazito kutokana na kifo cha Nelson.

KUMBUKUMBU MBAYA
Agosti 3, mwaka huu, watu wawili raia wa Afrika Kusini, walifariki dunia baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kupata ajali katika kata ya Igigwa, Sikonge mkoani Tabora.
Watu hao waliotambulika kwa majina ya Des Werner (58), pamoja na Werner Fredrick Fronaman (36), walikuwa kwenye ndege yenye namba za usajili 19-ZU-TAF mali ya Afrika Kusini.
Kabla ya ajali hiyo kutokea, walitua kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Tabora wakitokea Entebe, Uganda wakiwa njiani kuelekea Lilongwe, Malawi.
Taarifa zinaonesha kwamba chanzo cha ajali hiyo, ilikuwa ni kuzimika ghafla kwa injini ya ndege hiyo wakiwa angani. Taarifa zaidi zikaja kueleza kwamba ndege waliyokuwa wakiitumia, ilikuwa imetengenezwa kwa majaribio Cape Town nchini Afrika Kusini na kwamba walikuwa kwenye safari za majaribio, wakizunguka sehemu mbalimbali barani Afrika.
Siku tatu baadaye, Agosti 6, mwaka huu, ajali nyingine ya ndege ndogo ilitokea kisiwani Mafia, ikiihusisha ndege aina ya Cessna 208B Caravan mali ya Kampuni ya Tropical Air ambapo watu tisa walinusurika katika ajali hiyo.
Ndege hiyo ilikuwa ikitokea visiwani Zanzibar ambapo baadaye ilielekea jijini Dar es Salaam kabla ya kupata ajali ikiwa kisiwani Mafia.
Novemba 15, 2017 ilikuwa ni siku nyingine ya huzuni baada ya ndege ndogo ya Kampuni ya Coastal Aviation, kupata ajali Ngorongoro mkoani Arusha na kusababisha vifo vya watu 11 wakiwemo watalii waliokuwa wakipiga picha katika eneo la Kreta ya Imbakai ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Ajali hiyo ndiyo iliyoongoza kwa kusababisha vifo vingi katika ajali za ndege ndogo nchini.
Mwezi mmoja kabla ya ajali hiyo, Oktoba 25, 2017 ajali nyingine ikiihusisha ndege ya kampuni hiyohiyo ya Coastal Aviation, Cessna Grand Caravan ilitokea katika eneo la Lobo, ndani ya Hifadhi ya Serengeti na kusababisha watu wawili wajeruhiwe. Hakukuwa na vifo katika ajali hiyo.
Ajali hiyo pia ilitanguliwa na ajali nyingine iliyotokea Oktoba 8, 2018 wilayani Monduli, ikiihusisha ndege ndogo, Cessna 206 mali ya Kampuni ya Safari Air Link na kusababisha kifo cha abiria mmoja.
GUMZO MITANDAONI
Ajali ya juzi iliyokatisha maisha ya mtoto wa CDF Mabeyo, ni kama imekumbushia machungu yaliyosababishwa na ajali nyingine za ndege zilizotokea mwaka huu na mwaka uliopita, ambapo kwenye mitandao ya kijamii, wadau mbalimbali walianza kuchangia mada, wakihoji kwa nini ajali hizo zinatokea mfululizo?
#ChugaBarbie katika Mtandao wa Kijamii wa Twitter, aliandika: “Jamani hizi ajali za ndege ndogo mpaka lini? Kwa nini serikali haichukui hatua? Tumechoka kuwapoteza ndugu zetu.”
Isborn2017 katika Mtandao wa Kijamii wa Facebook yeye aliandika: “Mamlaka ya Usafiri wa Anga #TAA mbona mpo kimya? Siku hizi ndege zinaanguka kama daladala! Muwe mnazikagua na hizi, msiishie kwenye Bombadier pekee!” IamSumve kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliandika: “Pumzika kwa amani #NelsonMabeyo, mwendo umeumaliza kaka! Hizi ndege hizi, mbona zinatumaliza jamani?”
Maoni yaliyotolewa ni mengi lakini hoja zilizokuwa zinazungumziwa zaidi na wadau, ni usalama wa ndege ndogo zinazotumika kubeba abiria. Wapo waliohoji kama nazo huwa zinakaguliwa kabla ya kupaa na baada ya kutua kwa sababu nyingi hufanya safari zake kwenye maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kusafirisha watalii, ambako hakuna karakana za ukaguzi wa ndege.
Msisitizo uliwekwa kwenye mamlaka husika, kukaza uzi wa udhibiti kama ilivyo kwenye ndege kubwa ambapo ni nadra nchini kusikia zikipata ajali, kutokana na ukaguzi madhubuti unaofanyika kabla ya kuruka na baada ya kutua, huku pia zikifanyiwa ‘service’ kwenye karakana zilizopo kwenye viwanja mbalimbali vya ndege nchini.
CHANZO CHA AJALI ZA NDEGE NDOGO NI NINI?
Chanzo cha ajali iliyosababisha kifo cha mtoto wa Mabeyo, bado hakijafahamika na uchunguzi bado unaendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Kwa ajali iliyoua marubani wa Afrika Kusini mkoani Tabora, mbali na hitilafu za kiufundi zilizosababisha injini ya ndege hiyo kuzima angani, ilikuja kubainika pia kwamba marubani waliokuwa wakirusha ndege hiyo, walikuwa na leseni za daraja la kwanza ambazo kimsingi hazikuwaruhusu kupaa umbali mrefu angani.
Lakini pia, ndege hiyo ilikuwa imeundwa (assembled) nchini Afrika Kusini kwa majaribio kupitia mradi wa U- Dream, kwa hiyo haikuwa na uwezo wa kuruka umbali mrefu. Sababu hiyo ilisababisha ndege hiyo izuiwe kutua jijini Nairobi, Kenya kwa sababu haikuwa imekidhi vigezo vya usalama wa anga.

Lakini pia, marubani hao walikamatwa na kuzuiliwa kwa saa kadhaa jijini Cairo, Misri baada ya kubainika kwamba ndege yao ilikuwa na hitilafu kadhaa ambazo zilihatarisha usalama wao na wa watumiaji wengine wa huduma za usafiri wa anga, ingawa baadaye waliachiwa na kuendelea na safari yao kabla ya kufikwa na umauti.
Dk. Bwire Lufunjo aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT), katika mahojiano na gazeti moja la kila siku nchini, amewahi kunukuliwa akiizungumzia moja ya ajali hizo kuwa ni hitilafu katika mfumo wa umeme wa ndege uliosababisha mlipuko ulioenda kuzima injini.
Sababu nyingine zinazotajwa kuchochea ajali za ndege ndogo, ni hali ya hewa ambapo uchunguzi unaonesha kwamba ndege ndogo huwa hazina uwezo wa kuhimili mabadiliko makubwa ya hali ya hewa kama upepo mkali, mvua kubwa au nguvu za uvutano wa dunia (gravitational force) kwenye baadhi ya maeneo na kusababisha ajali za mara kwa mara.
KUTOKA KWA MHARIRI
Usafiri wa anga ndiyo unaotajwa kuwa salama zaidi duniani lakini usalama huo lazima uendane na ukaguzi wa ndege zinazofanya safari fupi au ndefu, bila kujali kama ni ndege ndogo au kubwa.
Ni wakati wa mamlaka husika, kuzitazama kwa jicho la tatu kampuni zinazotoa huduma za usafiri wa ndege za kukodi ili kuhakikisha zinakidhi vigezo vya usalama katika usafiri wa anga. Hii itasaidia kupunguza vifo vunavyosababishwa na ajali za aina hii.


Comments are closed.