The House of Favourite Newspapers

HADITHI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 4

0

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Nikiwa sielewi hili wala lile, nilimuona mmoja kati yao akirudi pale kwenye pikipiki, nikamuona akifungua kidumu kilichokuwa na kimiminika ndani yake ambacho kwa mbali sikuweza kugundua ni nini. Akarudi ndani kwa wenzake na kufumba na kufumbua, nilishtuka kuona moshi mwingi ukianza kutokea madirishani na pembeni ya paa.

 

SASA ENDELEA…

 

“Unanificha si ndiyo?”

 

“Snox, sina sababu ya kukuficha chochote ndugu yangu, ila labda Seba anaweza kuwa anajua chochote maana siku hizi ndiyo mtu wa karibu zaidi na mzee.”

 

“Nitampata wapi?”

 

“Lazima muda huu atakuwa anakula bata Trace Element, kule Masaki,” alisema Suma akitegemea kwamba baada ya maelezo hayo nitamuachia.

 

Kwa walichonifanyia, japokuwa sikuwa na nia ya kukatisha maisha ya mtu yeyote, lakini ilikuwa ni lazima niwashikishe adabu wote waliohusika halafu mwisho nitamalizia na huyo aliyewatuma, ambaye nilikuwa na hasira kali sana juu yake kwa alichonifanyia maishani mwangu.

 

Nilimsukuma Suma kwa nguvu, akakimbia na kusimama mbele hatua kadhaa mbele, akanigeukia haraka huku akiwa ameinua mikono juu maana alikuwa anajua ni nini ninachotaka kukifanya.

 

Mara nyingi kama mtu amekuteka na mkononi ana silaha ya moto, anapokwambia ukimbie, au anapokusukumia mbali na yeye, usidhani anafanya hivyo kwa sababu kweli amekusamehe, mara nyingi ni kwa sabahu anataka apate nafasi ya kukulenga vizuri ili akupige risasi.

Suma alilijua hilo na ndiyo maana alifikia hata hatua ya kunipigia magoti akiomba nisimfanyie chochote.

 

Sikutaka kusikiliza la muadhini wala mchota maji, nilifanya kile nilichoona kinafaa, mlio mkali wa bunduki ulisikika, na hasa ukizingatia kwamba ilikuwa imekatwa mtutu, mlio wake ulikuwa mkubwa na wa kutisha sana.

 

Sikupoteza muda, nilimruka pale chini alipokuwa ameangukia akitokwa na damu nyingi, nikachumpa kwenye ukuta na muda mfupi baadaye, nilikuwa nikiteremka upande wa pili wa ukuta. Nilijua kwa vyovyote lazima mlio huo utasikika kwa polisi waliokuwa doria ambao lazima watakuja eneo hilo kwa hiyo nilipita njia tofauti na niliyojia.

 

Wateja waliokuwa wakiendelea kuburudika mle ndani kwa vinywaji na muziki, walishtuka mno kusikia mlio wa bunduki, tena kutokea ndani kabisa ya ‘chimbo’ lao, kila mmoja akaanza kutimua mbio kuokoa maisha yake, wengine wakikanyagana hovyo na kusababisha madhara yawe makubwa.

 

Zile purukushani zilinisaidia hata mimi kuondoka eneo hilo kwa urahisi zaidi kwani nilijichanganya na kujifanya na mimi naogopa mlio wa risasi, nikawa nakimbia ‘mdogo-mdogo’.

 

Ungeniona wala usingeweza kuhisi kwamba mimi ndiyo nilikuwa chanzo cha mshike-mshike uliokuwa unaendelea.

 

Nilitokezea Sinza ya Mugabe baada ya kuwa nimekatiza sana vichochoro ili nisionekane na mtu yeyote. Nilisimama kando ya barabara na muda mfupi baadaye, bodaboda moja ilikuja, nikaipungia mkono na hatimaye ikasimama.

 

“Duh, baba umepiga pigo za kijambazi kabisa! Niuzie hilo koti,” alisema dereva wa bodaboda huku akichekacheka, nikanyamaza tu kwani ninapokuwa nimeivaa sura ya kazi huwa sipendi kucheka kwa sababu nimewahi kufundishwa kwamba unapocheka, unaondoa uzingativu wa akili.

 

“Nipeleke Trace Element.”

 

“Trace Element au Element?”

 

“Nimekwambia Trace Element,” nilisema kwa msisitizo, yule dereva wa bodaboda akanywea na nikamuona kama ananitazama kwa macho ya kuibia hivi.

 

Basi aliwasha pikipiki na tukaondoka huku kila mtu akiwa kimya kabisa. Njia nzima nilikuwa namsisitiza kuongeza kasi nadhani mpaka mwenyewe baadaye alikoma.

 

Basi baada ya kama dakika thelathini, tayari tulikuwa tumewasili Masaki, nikateremka kwenye bodaboda na kumlipa fedha zake kisha harakaharaka nikajichanganya na kuelekea kwenye chimbo lingine liitwalo Trace Element.

 

Unajua watu wengi wanapajua Club Element lakini hawajui kwamba kuna chimbo lingine la kijanja liitwalo Trace Element, ambalo ndani yake kuna watu wabaya wa kila aina.

 

Mara nyingi, wau wabaya huwa hawachangamani na watu wazuri mara kwa mara, hata wanapokunywa pombe, huwa wanatenga kujificha kwenye machimbo yao ambayo wanakutana wenyewe kwa wenyewe, hapo ndipo wanapokuwa na amani ndani ya mioyo yao kwani wakijichanganya na watu wasiowajua, kila anayemuona anahisi ni polisi au mpelelezi.

 

Kwa sababu mara kwa mara nilikuwa nakuja eneo hilo na wenzangu wakati nikiwa mwanachama kamili, nilikuwa nazijua njia nyepesi za kutoroka, hasa polisi wanapokuja kwa lengo al kufanya ukaguzi, niliamua kutumia njia hizohizo kuingilia kwa sababu nilikuwana uhakika pale getini nisingeruhusiwa kuingia.

 

Basi nilizunguka upande wa pili na kukwea juu ya mti uliokuwa jirani na fensi, nikatambaa na kujivuta juu kwa juu mpaka nilipopanda juu kabisa ya fensi, nikatafuta sehemu nzuri ya kurukia, nikadondokea ndani kimyakimya bila mtu yeyote kujua.

 

Unaweza kushangaa huu umahiri wa kuparamia kuta za watu, taha ndefu kiasi gani bila kushtukiwa na mtu yeyote nimeupata wapi? Katika kipindi chote nilichokuwa nafanya kazi za uhalifu, mimi ndiyo nilikuwa nategemewa zaidi kwenye masuala ya kuruka fensi na kwenda kufungua mageti kwa ndani.

 

Mara nyingi ili majambazi waingie ndani kwa urahisi, lazima mmoja atangulie ndani kupitia ukuta na akiingia, anaenda kufungua geti kwa ndani ili wote waliopo nje waingie na huko ndiko nilikopata ujuzi huo.

 

“Kumbe wakati napanda kwenye ule mti, mmoja kati ya walinzi wa eneo hilo, alikuwa ameshaniona na akawa anasubiri aone mwisho wangu.

 

Nikiwa pale chini, nilishtukia bomba la baridi likinigusa shingoni, likifuatiwa na sauti ya ‘tulia hivyohivyo kwa usalama wako’, nikajua nimepatikana.

 

Miongoni mwa vitu ambavyo Mungu amenijaalia, ni kutokuwa na hofu au woga ndani ya moyo wangu na pengine hiyo ndiyo sifa iliyokuwa inawafanya watu wote wanaonijua wawe wananiogopa au kuniheshimu, yaani kama huniheshimu basi uniogope kwani sikuwa na hata chembe ya woga.

 

Licha ya yule mtu kunigusisha bomba ambalo bila hata kuuliza nilijua lazima litakuwa ni mtutu wa bunduki, kwa jinsi ninavyowajua walinzi wengi wa Kibongo, huwa hawafanyi kazi kwa weledi.

 

Unaweza ukashangaa kwa nini nasema hivyo, lakini nikiri tu kwamba nimepitia mambo mengi sana hapa duniani, mengine makubwa na ya kutisha mno ambayo hata nikikusimulia, unaweza usiamini kwa haraka utakachokisikia.

 

Na miongoni mwa matukio mengi niliyoyafanya, yalikuwa yakiwahusu zaidi walinzi kwa hiyo nilikuwa najua jinsi walivyo wazembe.

 

Miongoni mwa sheria ambazo serikali inatakiwa kuzibadilisha mapema sana, ni hili suala la kampuni za ulinzi kukabidhiwa dhamana ya kulinda kwenye maeneo yenye mali za gharama, na kibaya zaidi kampuni hizi nyingi huwaajili wazee ambao hawawezi kupambana na majambazi wenye njaa, mwisho wanaishia kuuawa kama kuku.

 

Kwa hiyo nilichokifanya, nilijifanya kama nasalimu amri na kuinua mikono juu kisha kwa kasi ya kimbunga nikageuka na kumrukia yule mlinzi mwilini huku mikono yangu ikiwahi kuushika mtutu wa bunduki na kuugeuzia juu.

 

Kwa jinsi nilivyojirusha kwa nguvu, yule mlinzi hakutegemea kabisa kwa hiyo tukadondoka wote mpaka chini kama mizigo, tukawa tunagombea ile bunduki.

 

Katika zile purukushani, nilifanikiwa kumzidi nguvu, nikampiga na kitako cha bunduki yake mwenyewe, akapoteza fahamu.

 

Harakaharaka nilimburuta mpaka pembeni, nikamfunga mikono na miguu na kumjaza matambara mdomoni kisha nikaanza kuutafuta mlango wa kuingilia ndani.

 

Kwa nje kulikuwa na utulivu wa hali ya juu mno, usingeweza kuamini kwamba ndani kulikuwa na ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa.

 

Basi nilifanikiwa kufika kwenye mlango wa nyuma na kwa kuwa ulikuwa umefungwa kwa ndani, nilitumia mbinu ya kufyatua kitasa kwa kutumia sindano niliyokuwa natembea nayo.

 

Kwa watu waliowahi kushiriki kwenye haya mambo ya uhalifu, nadhani watakuwa wananielewa vizuri ninapozungumzia masuala ya sindano na vitasa.

 

Hakuna kitasa kinachoweza kufua dafu kwa mtumiaji mzuri wa sindano na mafuta ya breki.

 

Basi niliingia ndani kimyakimya na nikaiweka vizuri bunduki yangu, tayari kwa chochote.

Basi nilienda moja kwa moja mpaka kwenye vyoo vya uani, nikaingia kwenye moja kati ya vyoo hivyo na kujibanza humo, wakati nikitafakari nini cha kufanya.

 

Mara nilisikia vishindo vya mtu akija kule chooni, nikaikamata vizuri bunduki yangu, tayari kwa chochote.

 

Kwa bahati nzuri, aliingia kwenye choo cha pili, akajisaidia na muda mfupi baadaye, akawa anatoka.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

 

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply