HADITHI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 8
MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:
Ghafla niliinuka huku ‘bomba’ likiwa mkononi, kidole kikiwa kwenye ‘trigger’, nikazichekecha kwa mtindo wa kufagia kutoka kushoto kwenda kulia lakini ghafla nilihisi kitu kikipenya kwenye mwili wangu, damu zikaruka kama bomba lililopasuka, ghafla nikaanza kuhisi kama kizunguzungu.
SASA ENDELEA…
Sikuelewa tena kilichoendelea.
Nilikuja kuzinduka na kujikuta nikiwa nimefungwa kamba mikononi, huku vishindo vya mtu aliyekuwa akinisogelea vikisikika.
Nilikurupuka kwa hofu kubwa na kutaka kuinuka lakini kamba nilizokuwa nimefungwa mikononi na miguuni na kuunganishwa kwenye kitanda, na maumivu makali ya bega vilinifanya nishindwe kufanya nilichotaka kukifanya, nikawa natetemeka kuliko kawaida.
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kumbe tayari ilikuwa ni usiku lakini sikupata majibu hapo ni wapi na huyo mtu aliyekuwa akinisogelea ni nani.
Kabla sijapata majibu, nilishtukia nikimulikwa na mwanga mkali usoni.
“Umeamka?” sauti nzito ya yule mtu ilisikika ikinihoji huku akiwa bado ananimulika usoni, nikawa najaribu kujizuia lakini kwa kuwa mikono yangu ilikuwa imefungwa kwa nyuma, nilishindwa kufanya chochote kuuzuia mwanga ule, nikapata wazo la kufumba macho.
“Umefanya kazi nzuri sana leo,” alisema mwanaume huyo huku akizima ile tochi aliyokuwa ananimulika nayo, kisha akanisogelea pale kwenye kitanda nilipokuwa nimefungwa, akatoa kisu kidogo na kukata kamba nilizokuwa nimefungwa mikononi, akamalizia na miguuni.
Nilijaribu kuinuka huku nikiwa nimemkazia macho kwa sababu bado sikuwa najua yeye ni nani, nimefikaje hapo na kwa nini ananiambia maneno hayo.
Kumbukumbu za tukio la mwisho kabla sijapoteza fahamu zilinifanya niwe kama nimechanganyikiwa.
“Hebu tulia kwanza, utajitonesha kidonda chako bure,” alisema mwanaume huyo huku akinionesha kwa ishara kwenye bega langu la upande wa kushoto, nikajitazama na kushtuka kuona nimefungwa bandeji kubwa.
“Una bahati sana, ingeshuka chini kidogo ilikuwa inaenda kukupiga kwenye moyo, mshukuru sana Mungu kwamba iliingia kutokea mbele, ikapita katikati ya mfupa wa bega na kutokea upande wa pili,” alisema mwanaume huyo ambaye sasa niliweza kumuona vizuri uso wake.
Nilishtuka kutokana na maelezo aliyokuwa ananipa, harakaharaka nikakumbuka kuhusu tukio la kurushiana risasi lililotokea kabla ya baadaye kuhisi kitu cha baridi kikipenya na kuingia kwenye mwili wangu, na baadaye kupoteza fahamu kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Nini kilitokea na nimefikaje hapa?”
“Ina maana hujui ulichokifanya?” alisema mwanaume huyo huku akinitazama, tabasamu hafifu likiwa limechanua kwenye uso wake.
Nilihisi bado nipo kwenye hatari kubwa kwa sababu hata jinsi mwanaume huyo alivyokuwa akinitazama, ilionesha kama kuna kitu kinakaribia kutokea.
Nilichokifanya, japokuwa bado nilikuwa najisikia maumivu makali hasa pale kwenye mkono, nilianza kupiga hesabu za namna ya kumtoroka mwanaume yule.
“Unataka kutoroka si ndiyo?” aliniuliza, nikashtuka kugundua alijuaje kilichokuwa ndani ya kichwa changu? Nikawa natingisha kichwa kuonesha kwamba siyo kweli.
“Unatakiwa kuniamini, niliamua kukusaidia kuanzia kipindi ambacho hukuwa na fahamu, kama ningekuwa na nia mbaya na wewe si ningeshafanya ninachotaka kukifanya?”
“Wewe ni nani?”
“Hunijui mimi Snox? Ina maana umenisahau?” alinijibu kwa kunitaja jina langu, nikajikuta nikizidi kuchanganyikiwa.
Nikawa namtazama usoni huku nikijaribu kuvuta kumbukumbu zangu lakini bado sikuweza kumkumbuka kirahisi.
Nadhani na yeye aligundua kwamba sijamtambua kabisa, ikabidi avue mzula aliokuwa ameuvaa na kunisogelea.
Ni hapo ndipo nilipomtambua! Huyu alikuwa miongoni mwa vijana wa Bosi Mute na jina lake alikuwa akiitwa Siza, nakumbuka aliajiriwa siku za mwishomwisho kabla mimi sijaamua kuachana na kazi hiyo na kuamua kuwa raia mwema baada ya kuchoshwa na aina ya maisha niliyokuwa naishi.
“Umenikumbuka sasa!”
“Nakufahamu.”
“Uliyaokoa maisha yangvu siku ile Ubungo, na kiukweli nilibaki na deni kubwa ndani ya moyo wangu, nilihuzunika sana niliposikia umeondoka lakini nikamshukuru Mungu kwa kuamua kukubadilisha,” alisema Siza, kauli ambayo iliufariji sana moyo wangu.
“Najua upo kwenye wakati mgumu sana mdogo wangu, siku zote nimekuwa nikikuamini na naamini hata hili utalishinda kwa ujasiri mkubwa,” alisema huku safari hii akinipigapiga kwenye bega la kulia kama dalili ya kunifariji.
Nilikumbuka kuhusu tukio alilokuwa akilizungumzia na jinsi nilivyomuokoa! Nilijikuta nikisisimka sana mwili kwa sababu mwenyewe nilishasahau au pengine nilichukulia kama ni tukio la kawaida tu lakini kumbe bado Siza alikuwa akilikumbuka tukio hilo na kuamua kunilipa kwa wema.
Waliosema wema hauozi hawakukosea, unajua unaweza kutenda wema pengine hata kama mpo kwenye tukio baya ambalo ni chukizo mbele ya Mungu na wanadamu, lakini kama umelifanya kwa nia njema kabisa, basi ipo siku litakuja kukurudia, hata kama atakayekufanyia wema siyo yule ambaye wewe ulimfanyia, unaweza kurudishiwa wema wako kwa namna ya tofauti kabisa.
Nitakuja kuelezea kuhusu tukio hili la mimi na Siza baadaye lakini ni miongoni mwa matukio ya ujambazi yaliyowahi kuitingisha nchi na kuweka historia ya aina yake.
Wakati mwingine ni suala la kumshukuru Mungu tu kuona mpaka leo bado niko hai kwa sababu ama kwa hakika nimepitia mambo mengi sana kwenye hii dunia.
“Chuma changu kiko wapi?” nilimuuliza swali hilo ili niwe na uhakika na usalama wangu.
“Hiki hapa,” alisema huku akichukua bunduki yangu ambayo kumbe alikuwa ameihifadhi chini ya kile kitanda nilichokuwa nimelalia, akanipa kwa adabu, tena kwa kutumia mikono yote miwili. Nikainamisha kichwa kidogo kama ishara ya kumshukuru.
“Vipi kuhusu Saima?”
“Bado yuko chini ya mikono ya Bosi Mute.”
“Hapa ni wapi na nini kilichotokea?” nilimuuliza, akashusha pumzi ndefu na kunitazama, akanipigia saluti ambayo sikuelewa anamaanisha nini. Akaniambia yeye ndiye aliyekuwa zamu alfajiri ya asubuhi iliyopita na alishuhudia jinsi nilivyowapiga ‘ambush’ vijana wa Mute waliokuwa wakimuingiza Saima kwenye ngome hiyo.
“Mimi ndiye niliyekuwa getini na nilikuwa na taarifa tangu usiku kwamba kuna mzigo utafikishwa kambini alfajiri lakini sijui nini kikatokea wakachelewa kidogo.
“Wakiwa wamekaribia, niliwaona kutokea kwenye mnara wa mlinzi wa geti la nyuma, nikawa nawafuatilia wanavyosogea kama ilivyo kawaida ya kazi yetu,” alisema Siza na kuendelea kunieleza kwamba alifungua geti alipoona wamekaribia lakini ghafla akashtushwa na milio ya risasi zilizoanza kufyatuliwa kama mvua.
“Ilibidi nifunge geti na kufuatilia ni nini kilichokuwa kinaendelea lakini mpaka tunatoka nje,watu wote walikuwa chini, kila mmoja akiwa amechakazwa kwa risasi na cha ajabu, hakukuwa na mtu au watu waliofanya shambulio hilo baya, watu wote wakaamini kwamba lazima kuna watu wameshambulia na kukimbia lakini mimi nikawa mgumu kuamini kwa sababu aina ya upigaji wa risasi niliousikia ulikuwa tofauti.
“Kwa hiyo wakati wenzangu wanahangaika na wenzao ambao walikuwa na hali mbaya sana, wengine wakimkamata Saima na kumrudisha ndani, mimi niliamua kutoka na kulichunguza vizuri eneo la tukio na ndipo nilipokuona ukiwa umelala chini ya mti, damu nyingi zikiwa zimekutoka na kukufanya upoteze fahamu.
“Nikaamua kukubeba begani na kukimbia kuelekea porini kwa lengo la kutafuta nafasi nzuri ya kukusaidia bila mtu yeyote kujua chochote kinachoendelea na namshukuru Mungu nilifanikiwa na ndiyo maana leo upo hapa!
“Hapa ni Kibaha, Machinjioni na hatupo mbali sana na kambini,” alisema Siza, maelezo ambayo yalinifanya sasa nielewe ni nini kilichokuwa kimetokea.
“Vipi Mute anasemaje baada ya lile tukio?”
“Bado hajajua ni nani aliyehusika lakini amehisi kwamba ni wewe, ameagiza popote utakapoonekana upigwe risasi na kufa, anataka aione maito yako,” alisema Siza.
“Vipi kuhusu Saima wangu?”
“Yuko salama na bahati nzuri mimi na Teddy ndiyo tuliopewa jukumu la kumhudumia. Alikuja akiwa na hali mbaya lakini sasa hivi anaendelea vizuri, bado sijamwambia chochote kuhusu wewe ingawa mwenyewe anaonekana kama kuna kitu anakijua lakini hataki mtu yeyote ajue!
“Inaonesha alikuona ulivyokuwa unarushiana risasi pale getini na suala hilo limemchanganya sana kichwa chake. Kwani anajua kwamba wewe ni mzee wa bomba!”
“Mimi siyo mzee wa bomba Siza, wewe mwenyewe unajua kwamba hayo mambo nilishaachana nayo.”
“Anajua kwamba umewahi kupitia hii kazi?”
“Hajui chochote!”
“Ndiyo maana! Sasa nakushauri, utakapopata nafasi ya kuzungumza naye, mueleze ukweli awe anajua, pengine utamsaidia kumtuliza kichwa chake. Unajua kiumri mimi ni mkubwa kuliko wewe Snox, najua umuhimu wa hiki ninachokwambia.”
“Lakini mimi sifanyi tena hii kazi? Nimeshakuwa raia mwema hivi sasa.”
“Ungekuwa raia mwema usingefanya kile ulichokifanya pale getini! Ungewaacha wakupige risasi na kukuua! Ulichokifanya ni uthibitisho kwamba uwezo wako unazidi kuongezeka kila kukicha! Nani anayeweza kupambana kwa uwezo mkubwa kiasi kile na kuwaangusha watu wote? Wewe ni kamanda,” alisema huku akipiga tena saluti, nikaona kama ananichanganya kichwa.
“Namtaka Saima!”
“Unafikiri itakuwa rahisi kama unavyofikiria? Umefanya kazi na bosi Mute, unajua ni mtu wa aina gani.”
“Sijali chochote, namtaka Saima kwanza mengine yatafuatia.”
“Nenda kamchukue kama unaweza.”
“Ninaweza nandiyo maana nipo hapa,” nilimjibu kwa kujiamini, akanitazama usoni kisha akatingisha kichwa kama anayepingana na nilichokuwa nakisema.
“Mute ameshajua kwamba wewe ndiye uliyesababisha maafa makubwa kwa kuwapiga risasi vijana wake, unajua anawaza nini kuhusu wewe hivi sasa?”
“Sijali, ninachokitaka ni Saima wangu kwanza kisha mimi na yeye tutamalizana.”
“Huelewi ninavyokwambia kwamba ameagiza uuawe mahali popote utakapoonekana. Anasema mwanzo alijua unaweza kubadilika na kurudisha moyo wako nyuma lakini kwa kitendo kilichotokea, amebadilisha mawazo, anataka ufe.”
“Mimi pia nataka afe, na nitahakikisha namuua kwa mikono yangu.”
“Sikia Snox, usifanye maamuzi kwa hasira. Kwa hali uliyonayo hivi sasa, unatakiwa kwanza kukaa na kuuguza jeraha lako huku ukipanga mipango ya namna ya kurudi, utakapokuwa tayari mimi nipo tayari kukusaidia.”
Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:
www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.
Usisahau kulike, share na ku-subscribe.