Manara Atema Cheche Adai Wachezaji wa Kitanzania Hawajitambui – Video
MSEMAJI wa Klabu ya Yanga Haji Manara kupitia kipindi cha Krosi Dongo kinachorushwa na 255globalradio na Global TV amesema kumekuwa na tatizo la wachezaji wa kitanzania kutojitambua.
Manara amedai kuwa wachezaji wengi hasa wazawa wamekuwa hawajitambui kutokana na kutotambua thamani zao hasa linapokuja suala zima la kutumia ukubwa wa majina yao kujipatia kipato nje ya masuala ya michezo (Branding).
Lakini pia Manara hakuishia hapo amedai wachezaji hawa wazawa wamekuwa na changamoto ya kutokuwa na mawakala au mameneja wazuri wa kuwasimamia na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao ikiwa ni pamoja na kwenda kucheza soka la kulipwa katika vilabu vikubwa barani Afrika kama vile Al Ahly, Mamemlodi Sundown pamoja na Wydad Casablanca.
Pamoja na kuzungumzia mambo mengi, msemaji huyo anayesifika kwa mbwembwe na utani mwingi hasa kwa timu pinzani amemtaja mchezaji wa Simba Bernard Morrison kuwa ni mchezaji hatari na kwamba anaweza kuwa mwiba mkali kama asipochungwa vizuri na mabeki wa timu yake katika pambano la Ligi Kuu Bara linalotarajiwa kuchezwa Aprili 30, 2022 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.