The House of Favourite Newspapers

Harmo amemzidi Mondi kwa busara!

MOJA kati mahojiano bora ambayo Rajabu Abdul ‘Harmonize’ amewahi kuyafanya basi ni yale aliyoyafanya wiki iliyopita, ambapo alifu-nguka mambo mengi yahusuyo muziki wake likiwa suala la kuachana na uongozi uliomkuza kisanaa, Wasafi Classic Baby (WCB).

Muvi ya Harmonize kutaka kujitoa Wasafi ilianza muda mrefu kidogo, kila mtu alikuwa na mtazamo wake katika suala zima la yeye kujitoa. Kuna ambao walikuwa wanasema hataweza kusimama mwenyewe, kuna wengine walisema ataweza.

Lakini pia walikuwepo wengine ambao walisema pengine anahitaji muda kidogo kuweza kusimama mwenyewe. Kama hiyo haitoshi, kulikuwa na presha nyingine kutoka kwa watu wenye hofu ya kuzikabili fitna za kimuziki.

Harmonize anakwenda kuanzisha Konde Gang, ataweza kujidhibiti na fitna za Wasafi ambao wanaweza kumchezea rafu za kila aina ili mradi tu asiweze kusikika. Kumharibia ili kumdhihirishia kwamba bila wao, hakuna Harmonize.

Waliokuwa wanaijadili hoja hiyo, walikuwa na mifano yao kadha wa kadha ukiwemo ule wa Rich Mavoko. Kwamba alivimba kichwa, akadhani ataweza bila Wasafi matokeo yake mambo yanamuendea kombo. Ni kweli, kwenye gemu kuna fitna nyingi hivyo ili uweze kusimama, unahitaji roho ya kiaskari.

Watu wapo radhi kukufanyia kila aina ya jambo baya kwa gharama zozote ili tu kuthibitisha wao ni bora zaidi na huwezi kusimama bila wao. Mifano ipo mingi ya watu waliokuwa wakali wa kujimwambafai lakini kimsingi ukiwa imara, inawezekana kupita katikati yao na wakashangaa.

Tetesi za Harmo kujitoa Wasafi zilipokuwa zikishika kasi, pande zote mbili zilikuwa kimya. Wasafi walikuwa hawataki kuzungumza lakini pia uongozi mpya wa Harmo ulikuwa hautaki kutoa neno lolote hususan katika suala zima la msanii wao kujitoa Wasafi.

Meneja wa Harmo, Mjerumani alikuwa radhi kuzungumzia mambo mengine yote ya kimaendeleo ya kimuziki ya msanii wake ikiwemo ofisi mpya ambayo ina kila kitu kama ilivyokuwa Wasafi. Lakini ukimgusia kuhusu msanii wake kujitoa, hakuwa tayari kusema neno.

Hata Harmo mwenyewe hakuwa tayari kuzungumza lolote. Waandishi wa habari walikuwa na kibarua kizito kupambana na wingu zito ambalo lilikuwa limetanda kati ya pande hizo mbili. Viashiria vyote vya kwamba Harmo hayupo Wasafi, vilikuwepo lakini hakuna aliyethibitisha.

Wakati mambo yanakorogeka, Wasafi Festival ilikuwa ndiyo imeanza mikoani. Bosi kubwa Mondi alipohojiwa na vyombo vya habari baada ya kuulizwa Harmo atapafomu shoo hizo aliwataka wawe wavumilivu, atapanda kwenye majukwaa mengine sababu ni vigumu kuwa na Wasafi wote wakati pia wanakuwa na shoo za watu nyingine ambazo zilishalipiwa.

Mambo yakaenda hivyo, shoo kibao Harmo hakuonekana. Badala yake tukaanza kusikia vijembe kutoka kwa Mondi. Akiwa kule Iringa, Mondi alisikika akisema kwamba; Rais pekee ambaye wananchi wamemchagua, nishasalitiwa na Jeshi ila wakashindwa kunipindua.

Japo hakumtaja moja kwa moja Harmo lakini aliyekuwa anajiita JESHI ni Harmonize. Hiyo ilikuwa ni baada ya ahadi ya Diamond kuwa Harmo atatokea kwenye majukwaa hayo lakini hakutokea, ghafla tukasikia maneno hayo ya vijembe.

Mondi hakuishia hapo, kwenye majukwaa hayohayo ya Wasafi Festival, alisikika sasa live akimchana Harmonize akiwa jukwaani. Alichomekea hivi alipokuwa akiimba wimbo wa Baila; “ Si unajua wanamuziki vitabia vyao, wamejawa tamaa hasa wale kina Harmonize…”

Bwa’mdogo Harmo wakati huo alikuwa kimya, hivyo vijembe alivisikia lakini hakujibu chochote. Hii ndio tunaita busara, Waswahili wanasema mkubwa hakosei. Alijua kabisa kaka yake anamchana yeye ila hakuona sababu ya kumjibu. Alikaa kimya kabisa.

Lakini kuonesha sasa amekua kiakili, sikiliza mahojiano yake ya wiki iliyopita. Alifafanua vizuri kuhusu suala la yeye kuondoka, lakini ulimi wake ulikuwa makini sana katika kuzungumza. Hakutaka kabisa kuonesha dharau, hakutaka kuleta jeuri juu ya kule alikotoka.

Alikiri kwamba hawezi tena kuwa na mawasiliano na memba wa WCB kutokana na ile hofu ya kuonekana wasaliti lakini alisema anaamini Wasafi hawawezi kumuombea mabaya kama yeye ambavyo hawaombei mabaya.

Alieleza vizuri kuhusu suala la kuwalipa fedha za kuvunja mkataba, akaeleza jinsi ambavyo aliamua kulipa fedha hizo bila kelele sababu kufanya hivyo kungeweza kuleta mambo ya kupelekana mahakamani ambapo mwisho wa siku ingekuwa uadui ambao yeye hapendi kuona unatokea.

Alionesha kwamba ndoto yake ni kutaka kuona muziki unaendelea na hakuna bifu kati ya wasanii na wasanii au wasanii na vyombo vya habari, hiyo ndiyo busara. Hivi tunavyoongea sasa hivi, Mondi na wasanii wake wana mabifu na baadhi ya vyombo vya habari.

Harmo amesema yeye ndoto yake ni kuona wasanii wote wanashirikiana na vyombo vyote vya habari ili kuhakikisha muziki wa Bongo Fleva unafika mbali. Jambo hilo linashindikana kutokana na ubinafsi, chuki na roho mbaya baina ya msanii na msanii, wadau fulani na wadau wa mahali pengine.

Harmo anatamani sasa hivi nyimbo zake zichezwe na Wasafi FM au Wasafi TV jambo ambalo sidhani kama linawezekana. Nafsi zetu kidogo ni ngumu kukunjuka japo mdomoni twaweza kusema sina kinyongo na mtu fulani lakini kiuhalisia kinyongo kinakuwepo na hizo ndio fitna za Kitanzania.

HAKUNA ALIYETUROGA TUSHINDWE KUSHIRIKIANA, BALI TUNAJIROGA WENYEWE KWA ROHO ZETU!

Comments are closed.