The House of Favourite Newspapers

HATA WEWE DEGEDEGE INAWEZA KUKUPATA, SOMA HAPA!

DEGEDEGE ni hali ya ghafla ya kutingishika mwili mzima au mikono na miguu kunakosababishwa na kukakamaa kwa misuli ya mwili.  

 

Ugonjwa huu huwakumba zaidi watoto wadogo japokuwa hata mtu mzima anaweza kupatwa na maradhi haya. Huko nyuma watu waliamini kwamba degedege huwakumba watoto tu jambo ambalo sio sahihi.

 

Tatizo hili mara nyingi linatokana na magonjwa au hitilafu katika ubongo ambapo husababisha kutokea kwa upungufu wa vichocheo vya sukari kwenye damu, kitaalamu huitwa Hypoglycemia pamoja na upungufu wa hewa ya oksijeni kwenye damu, yaani Hypoxia.

 

Maradhi haya husababishwa na magonjwa mbalimbali na mara nyingi hujitokeza kwa watu ambao wana familia yenye historia ya ugonjwa huu, hivyo ni wa kurithi au huweza kuwa kiashiria cha kifafa. Watu wa rika zote wanaweza kuathiriwa na degedege, lakini watoto na vijana ndio huathirika zaidi na ugonjwa unapojirudia huitwa kifafa.

 

Imani za kuwa mtu mwenye degedege hachomwi sindano zimechangia kuongezeka kwa vifo au mtindio wa ubongo ambavyo hutokea iwapo maradhi haya hayakutibiwa kwa haraka na kwa ufasaha. Wakati mwingine si rahisi kubaini iwapo mtu amepatwa na degedege kutokana na baadhi ya watu hushikwa na bumbuwazi kwa muda mfupi hivyo kutojua kama amepatwa na degedege au la.

 

DALILI

Dalili za maradhi haya hutegemea sehemu ya ubongo ambayo imeathirika na hujitokeza kwa haraka ambapo husababisha mwili, miguu na mikono kuanza kukakamaa na mgonjwa kurudisha kichwa nyuma. Kushindwa kupumua na kutokwa na mapovu mdomoni, macho kugeukia nyuma na kuonekana kwa sehemu nyeupe ya jicho ni dalili kuu za ugonjwa huo wa degedege.

 

Kupoteza fahamu au kuzimia ikifuatiwa na kuchanganyikiwa (mgonjwa anapoteza kumbukumbu) pamoja na kushindwa kuzuia mkojo na haja kubwa ni dalili nyingine muhimu kuzijua. Hata hivyo, shambulio la degedege huisha baada ya muda mfupi mara nyingi chini ya dakika tano.

 

Baada ya shambulio mgonjwa hupitiwa na usingizi mzito kama takribani dakika 30 hadi saa nzima na azindukapo hushindwa kutambua kitu chochote kwa muda na huonekana kaduwaa.

 

CHANZO CHAKE

Degedege si ugonjwa bali ni maradhi yanayosababishwa na magonjwa mbalimbali, pia hutokana na kuvurugika kwa mfumo wa umeme katika ubongo.

Chanzo kikubwa cha degedege hutokana na maambukizi kwenye ubongo na uti wa mgongo. Kuumia ubongo kunakoweza kujitokeza wakati wa kujifungua, ugonjwa wa malaria, homa kali hasa kwa watoto, kifafa pamoja na kifafa cha mimba.

 

MATIBABU

Matibabu yake hutegemea chanzo cha maradhi hayo, mfano iwapo degedege imesababishwa na malaria au homa ya uti wa mgongo, mgonjwa anapaswa kutumia dawa za kutibu malaria na antibiotiki ya kuua bakteria. Pia mgonjwa huweza kutumia dawa zinazosaidia kudhibiti degedege.

 

MADHARA YA UGONJWA

Mwenye degedege asipopata tiba sahihi kwa wakati anaweza kupatwa na madhara yafuatayo: Kupata tatizo la kifafa, mtindio wa ubongo kwa watoto hali ambayo inaweza kuchangia uelewa duni katika masomo yake darasani. Mtoto anaweza kuwa na tatizo la ukuaji duni hasa kama degedege ikiwa itamtokea mara kwa mara kwani hatimaye mtoto kudumaa.

 

USHAURI

Inashauriwa na wataalamu wa afya kuwa pindi mtu apatapo degedege awahishwe haraka katika zahanati, kituo cha afya au hospitali ya karibu kwa matibabu zaidi ili kumwepusha na hatari ya kupata magonjwa ambayo yanaweza kumsababishia magonjwa ya kudumu katika maisha yake kama kifafa.

Comments are closed.