HATARI: ‘TANROADS WANASUBIRI ZIFIKIE AJALI NGAPI HAPA?’

GAZETI hili kwanza lina kila sababu ya kuipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli. Ndani ya kipindi cha miaka mitatu na miezi kadhaa, yamefanyika mambo mengi ya kimaendeleo ambayo kila mwananchi kutoka moyoni mwake anaweza kusema HONGERA JPM!  

 

Miongoni mwa mambo ambayo serikali hii imeyatilia mkazo ni pamoja na suala la barabara. Tumeshuhudia sehemu mbalimbali zikijengwa barabara za kisasa kabisa kiasi cha kurahisisha usafiri, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Watu wa takwimu wanaweza kujua mpaka sasa ni barabara ngapi, zenye ukubwa gani zimejengwa nchini lakini itoshe tu kusema kwamba, kwenye hili la miundombinu imefanyika kazi kubwa.

 

Hata hivyo, katika jitihada za kuleta maendeleo, changamoto haziwezi kukosekana na ndiyo maana katika pitapita ya waandishi wetu wamekutana na kero kubwa sana katika barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami inayotoka Goba hadi Makongo Juu jijini Dar. Siku za nyuma kidogo, barabara hiyo ilikuwa ya vumbi, mara kadhaa limekuwa likipitishwa greda na kuifanya ipitike kwa siku chache lakini baada ya muda hasa ikitokea mvua ikanyesha, mashimo yalikuwa yakirejea na kuifanya kupitika kwa shida, hasa kwa wale wenye magari madogo.

 

Baada ya adha ya muda mrefu, hatimaye serikali ilisikia kilio cha wananchi, ikaamua kujenga barabara hiyo lakini sasa, shida iliyojitokeza ni kuwepo kwa baadhi ya watu waliokuwa wamejenga pembeni mwa barabara hiyo ambao walitakiwa kubomoa ili kupisha ujenzi.

 

Taarifa iliyopo ni kwamba, wote waliokuwa wamejenga pembeni mwa barabara hiyo wamelipwa fidia na walitakiwa kubomoa nyumba zao. Lakini gazeti hili limebaini kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawakutii agizo hilo na matokeo yake sasa, kuna maeneo ambayo nyumba zilibaki na hata wakala wa barabara nchini, Tanroads walipoanza ujenzi wao, walilazimika kuzikwepa, huenda ni katika kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

 

Ila sasa, uamuzi huo umeleta usumbufu mkubwa sana kwa watu wanaotumia barabara hiyo kwani kuna eneo lililopo katikati ya Goba na Makongo Juu ambapo kuna sehemu yenye mlima kisha pembeni yake kuna vijumba kadhaa vimechwa vikiwa vinaning’inia, yaani vimekaa kihatari sana.

Walichokifanya Tanroads ni kujenga barabara moja eneo hilo na kwa sababu kuna mlima, ajali nyingi zimekuwa zikitokea. Wananchi wa eneo hilo walipokuwa wakizungumza na Uwazi walisema kuwa, wameshangazwa na hatua hiyo ya kuviacha vijumba hivyo vilivyokaa juu ya gemo ambavyo hata mvua ikinyesha kuna uwezekano wa kuanguka na kuziba barabara.

 

“Hili ni eneo hatari sana, ajali zinatokea kila siku kutokana na jinsi palivyokaa. Inawezekana kweli nyumba hizo ziliachwa kwa kuwa wamiliki walikuwa hawajalipwa fidia, lakini sasa si wamelipwa? Mbona wamebomoa upande na kuliacha eneo hilo liendelee kuwa korofi?

 

“Hawa Tanroads wanasubiri zitokee ajali ngapi ndipo wapashughulikie? Maana pale kwa sasa hata kama wasiweke lami, ni suala la kupitisha greda na kuwezesha magari kupishana vizuri kama ilivyo sehemu nyingine,” alisema Hamis Salimu wa Goba eneo la Mtipesa.

 

Katika kujua ni kwa nini eneo hilo hatari limeachwa liendelee kuwa hatarishi kwa watumiaji wa barabara hiyo, waandishi wetu walifika kwenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kibululu iliyopo karibu kabisa na eneo hilo ambapo walifanikiwa kuonana na Afisa Mtendaji aliyefahamika kwa jina la……, akasema:

 

“Hilo eneo tunalijua vizuri, awali kulikuwa na zoezi la kuwalipa fidia wale waliojenga pembeni mwa barabara hiyo, wameshalipwa na sasa hivi kazi inaendelea.

Uwazi: Lakini eneo lile linaonekana kuwa hatari sana, ajali zinatokea kila siku, kwa nini zisifanyike hata jitihada za kuliondoa lile gemo na kufanya magari yapishane vizuri?

Ofisa: Ni kweli pale ni hatari lakini watu wa Tanroads wako kazini, siku si nyingi ile adha itaondoka.

Uwazi: Inashindikana nini hata leo kuondoa lile gemo tu ili magari yapite vizuri wakati Tanroads wakijipanga kuziunga zile barabara kwa lami?

Ofisa: Unajua pale juu pia kuna nguzo za umeme ambao unatumika eneo kubwa, kwa hiyo hata Tanesco pia wanaweza kuwa wanachangia zoezi lile kutofanyika haraka lakini nakuhakikishia siku si nyingi mambo yatakuwa mazuri.

Itaendelea wiki ijayo.

Loading...

Toa comment