The House of Favourite Newspapers
gunners X

Haya Ndiyo Niliyoyaona Baharini-11

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
Ghafla nilifikicha macho kwani kama niliona kitu mbele yangu.
“Vipi tena?” aliniuliza Nurdin baada ya kuniona nimetumbulia macho mahali.
“Kama nimemwona.”
“Nani?”
“Bi. Sheila.”
Na yeye aliangalia kule ninakoangalia mimi.
“Ni wasiwasi tu hakuna lolote bwana Tolu.”
SASA ENDELEA…

Nilifikicha macho tena.
“Nurdin, yule mwanamke yumo ndani ya nyumba muda huu,” nilimsogelea sikioni Nurdin na kumwambia habari hizo.
Ghafla naye akataharuki, nilimwona akisimama huku akisema:
“Ondokeni humu ndani haraka sana,” huku akiwa ametumbulia macho mahali. Nikajua na yeye amemwona wa kwake.
“Baada ya dakika kama tatu, Nurdin akiwa anahema sana akasema:
“Hawa viumbe wanatutafuta kwa kutufuata mpaka huku majini lakini mimi sikubaliani nao hata kidogo.”
“Sasa tutaponaje Nurdin?”
“Usiwe na wasiwasi bwana Tolu. Kinga tunayo ya kutosha na ndiyo maana wameshindwa kutugusa sehemu yoyote ya mwili. Unajua majini wana uwezo wa kukugusa moja kwa moja na kukudhuru.”
“Kweli Nurdin?”
“Kweli. Na kudhuru kwao ni kukubwa sana kupita kawaida. Ndiyo maana walio wengi wakikutana macho na majini wanakufa au wanapata magonjwa ya mshtuko lakini sisi si umeona hapa tuko poa sana.”
Meli ilikata maji, utulivu wa baharini ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba hakuna aliyekumbuka yaliyopita kule Papua New Guinea.

Usiku ulianza kuingia hali ambayo nilianza kuifikiria kwamba haiwezi kupita salama.

Kwa kawaida ndani ya meli tulikuwa na vyakula kwa maana kwamba mtu anaweza kula akiwa mlemle ndani. Hivyo, muda wa kula kila mmoja alikula alivyopenda kwani tuliweka utaratibu wa kuwa na chakula cha pamoja kasoro nahodha wetu.
Huyu nahodha alikuwa bingwa sana wa kuvuta bangi. Alikuwa akivuta bangi mpaka anakuwa kama gaidi kwani anaweza kukusukumia hata majini. Hali hii iliwafanya baadhi ya wafanyakazi kusema iko siku watamchoma kisu. Nurdin na baadhi ya wengine ndiyo waliokuwa wakituliza hali ya hewa mara kwa mara.

Wakati giza linaingia, kila mmoja alikuwa akiona uzito wa hali ya hewa kwani ilibidi taa ziwashwe ili kuiruhusu meli kutambulika. Kuna ule mnara wa juu wa meli ambao unatakiwa uwe unawaka taa nyekundu kunapokuwa na giza ili vifaa vinavyotembea angani, kama ndege iwe rahisi rubani wake kuiona na kuikwepa.
Ndiyo maana hata mijini, ile minara ya simu ikishakuwa mirefu kiasi cha kupita maghorofa lazima iwe na taa nyekundu ili kumrahisishia rubani wa ndege kazi ya kujua wapi kuna minara.

Basi, tulikuwa katikati ya giza nene, mbele hakuna nyumba, kulia hakuna nyumba, kushoto na nyuma vilevile. Hapo sasa ndiyo katikati ya bahari. Nurdin aliniangalia, akanisogelea na kusema:
“Bwana Tolu, hivi unajua kwamba ukitaka kujua dunia ni duara bahari ndiyo kigezo cha kwanza?”
“Kivipi Nurdin?” nilimuuliza.

“Meli inapokuwa katikati ya bahari halafu huoni chochote pande zote ujue upo eneo ambao ni mduara. Ndiyo maana meli ikiwa inakuja mbele yako. Kitu cha kwanza kinachoweza kuonekana ni mnara ambao ndiyo sehemu ya juu sana ya meli.
“Lakini kadiri meli inavyozidi kusogea, unaanza kuiona meli yenyewe kwa juu mpaka usawa wa majini. Hii hali ndiyo inayokwambia kuwa, dunia ni duara na meli inapokuja inakuwa inapanda mlima.”
Ghafla meli yetu ilizima. Ikawa haisikiki kutoa mlio wowote ule. Nikaanza kuogopa kwani meli kuzima ni hatari.
Niliwaona wafanyakazi wote wakipanda juu ya meli huku wakipiga kelele na kusemasema kila mtu maneno anayoyajua mwenyewe.

“Nurdin nini tena?” nilimuuliza maana na yeye alikuwa akiekekea juu.
“Njoo huku bwana Tolu.”
Niliwafuata mpaka juu kabisa ambako walikuwa wamesimama wakiangalia juu na chini mara nyingine kwenye maji ya bahari.

“Jamani kuna nini kwani?” niliwauliza.
“Tunaweza kuzama Tolu,” waliniambia wengine lakini Nurdin hakufanya hivyo.
“Ni kweli Nurdin?” nilimuuliza, hakunijibu.
Lakini akasema: “Jitahidini kumwomba Mungu.”
Nilianza kulia nikiamini ni mwisho wa maisha yangu. Nilisema ni mwisho wa maisha yangu kwani meli ilianza kuelea maana hata sisi kusimama kwetu melini kulikuwa kunasukwasukwa huku na kule.
“Nurdin niambie jambo la maana.”
“La maana ni hili bwana Tolu, mjue Mungu wako kwenye matatizo kama haya.”
Mara, nahodha alikuja juu ya meli huku akiwa anapiga kelele. Lakini cha ajabu akaanza kutupiga mmoja baada ya mwingine akisema anatuua.

Sisi tukahisi alizima injini kwa makusudi na ndiyo maana amefikia hatua ya kutupiga. Mimi nilijiuliza kwa nini alikuwa akitupiga? Tulimkosea nini kikubwa ambacho kilimfanya achukue hatua ile!
Aliponisogelea nilimwachia ngumi moja, akaanguka. Maana mimi nilikuwa mrefu kwake na nilikuwa nina mwili kuliko yeye. Kwanza yeye alikuwa mnywaji sana wa pombe kali.
Akakimbia kushuka chini na baada ya dakika moja tu, injini zikawaka na meli kuanza kukata maji. Kwangu sikujua kama ilikuwa kawaida au la!
“Kwani inawezekana Nurdin?” nilimuuliza.
“Kuhusu nini bwana Tolu?”
“Meli kuwakia ndani ya maji na kuanza safari?”

Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma mkasa huu kesho kwenye Gazeti la Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply