HUKU JPM AKIIBUA ISHU YA MO MKURUGENZI DAR ATEKWA SAA 5,700

INATISHA! Wale watu wasiojulikana wanadaiwa kumteka mkurugenzi na mmoja wa wamiliki wa kampuni maarufu ya kusambaza vifaa tiba jijini Dar ya Immunolabs Medical Supplies Ltd anayejulikana kwa jina la Kepha Peter Mwiti (62), mkazi wa Ununio jijini Dar, Amani lina mkasa mzima.

 

ZAIDI YA SAA 5700

Kwa mujibu wa mzazi mwenza wa Mwiti aitwaye Grace Urassa (42), mkazi wa Bunju A jijini Dar, tangu kutekwa kwa tajiri huyo Julai, mwaka jana, sasa yapata miezi nane ambayo ni zaidi ya saa 5,700 bila kuonekana.

 

GRACE NA AMANI

Akisimulia mkasa huo, Grace aliliambia Gazeti la Amani, mapema wiki hii kuwa, mumewe huyo alitekwa kwenye ofisi za kampuni hiyo zilizopo Mtaa wa Majimaji, Mikocheni jijini Dar. Alisema taarifa za Mwiti ambaye amezaa naye watoto wawili, Audrey Kepha Mwiti (5) na Kennedy Kepha Mwiti (3) kutekwa, alizipata kutoka kwa karani wa kampuni hiyo aitwaye Lucas Mpali. “Mimi na Mwiti ni wamiliki na wakurugenzi wa Kampuni ya Immunolabs iliyosajiliwa Brela kwa namba 51630.”

 

ALIPATAJE TAARIFA?

“Mnamo Julai 9, mwaka jana nilipokea taarifa kwa karani wa kampuni yetu (Lucas Mpali) ambaye yeye alipokea simu kutoka kwa mfanyakazi mwenzake ambaye  naye alipigiwa simu na mtoto mkubwa wa Mwiti (Ayubu Peter ambaye ni mtoto wa mke mkubwa wa Mwiti).

 

ALIMWAMBIA MWANAYE AMETEKWA

“Ayubu ndiye aliyetaarifu kuwa alipigiwa simu na baba kwa kutumia WhatsApp na kumwambia kuwa ametekwa huku akisikia akipewa mateso na baada ya hapo simu haikupatikana tena.

 

“Baada ya kupokea ujumbe huo mzito, nilimpigia simu mzazi mwenzangu (Mwiti) bila mafanikio ndipo nikawatafuta kaka yake (David Msangi) na dada yake (Irene Kilumanga) kutaka kujua kama wana taarifa juu ya kutekwa kwa ndugu yao.

 

Lakini cha ajabu, wote walisema hawana taarifa. “Nilimpigia simu mwanasheria wa kampuni yetu (Walter Goodlucky) kumuuliza kama na yeye ana taarifa, akaniambia ndiyo anayo na alijulishwa na Ayubu (mtoto wa Mwiti).

 

KAKA MTU AHAKIKISHA

“Baadaye kaka wa Mwiti (David Msangi) alinipigia na kunihakikishia kuwa ni kweli baba watoto wangu kapotea katika mazingira ya kutatanisha. Aliniambia yeye alihakikishiwa na mke mkubwa wa Mwiti (Grace Mfinanga),” alisema Grace huku akitokwa na machozi kwa uchungu kisha aliendelea: “Nilianza kufuatilia kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay maana niliambiwa ndiko Ayubu alipokwenda kuripoti.

 

“Kabla ya kufika kituoni Oysterbay, nilipita kwa rafiki wa karibu wa Mwiti anayefanya kazi maeneo ya Oysterbay ambaye aliniambia hana taarifa za rafiki yake kutekwa. “Lakini rafiki huyo alimpigia simu Ayubu ambaye alimhakikishia kuwa ni kweli baba yake amepotea na kwamba alisharipoti kituoni Oysterbay.”

 

SAFARI YA OYSTERBAY

“Rafiki huyo alinishauri niende Oysterbay nikajue kinachoendelea na kwa taarifa zaidi nimuone mpelelezi na mkuu wa kituo.

 

“Nilifanya hivyo, lakini ilibainika kuwa hakuna maelezo yaliyokuwa yametolewa na mtoto wa Mwiti kama alivyodaiwa, hivyo nilichukuliwa maelezo. Baada ya hapo nikampigia simu Ayubu kumuuliza mbona taarifa za baba yake kupotea hazipo kituoni akaniambia anakwenda kufungua jalada na kweli alifanya hivyo.

 

POLISI WAMKAMATA GRACE

“Kitu ambacho kilinishangaza ni kwamba baada ya taarifa kufunguliwa polisi walikuja kunikamata mimi na kuniweka ndani kwa siku tano bila kunieleza kosa langu.

 

“Walinikamata, wakachukua simu zangu wakasema wanapeleleza tukio, wakaenda kwangu kusachi lakini pia hawakuniambia walikuta nini, lakini baadaye waliniachia. “Toka hapo nimekuwa kila nikifuatilia uchunguzi nazungushwa bila kupewa majibu mazuri.

 

“Lakini wakati huohuo kuna watu wananitishia kuwa nikiendelea kumtafuta Mwiti na mimi nitapotea kama yeye, taarifa hizi polisi wanazifahamu lakini napo sioni msaada,” alisema Grace huku akifuta machozi.

 

HADI KWA DCI

“Katika kumtafuta Kepha, nilifika hadi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka na Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, nilikaa naye na kumweleza shida yangu, alinisikiliza na kuahidi kunisaidia, lakini nako msaada sikuuona mpaka leo hii.

 

“Nilipoona hakuna mafanikio ya kumpata baba watoto wangu, kiukweli roho ilizidi kuniuma nikaona bora nimwandikie barua nzito Rais John Pombe Magufuli (JPM) nikaipeleka ikulu (Magogoni). Nashukuru nilipokelewa vizuri, lakini mpaka sasa sijapata majibu.

 

KILIO KWA JPM

“Namuomba Rais Magufuli, baba yangu, nina imani kubwa sana na yeye, anisaidie kwani watoto wananiuliza baba yupo wapi mama? Kiukweli naumia sana.”

Grace alisema kuwa shauri la kupotea kwa Mwiti lipo katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay likiwa na jalada la kesi namba DSM/KIN/CID/PE/175/2018- UCHUNGUZI. Alipoulizwa kama baba watoto wake huyo alikuwa na tatizo au mgogoro na mtu, Grace alisema: “Hakuwa na tatizo na mtu wala sijawahi kusikia akigombana na mtu.” Gazeti la Amani lilimtafuta DCI Boaz bila mafanikio kufuatia simu yake kuita bila kupokelewa.

 

KAMANDA KINONDONI

Alipotafutwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni ambapo ndipo kilipo Kituo cha Polisi cha Oysterbay, ACP Mussa Taibu aliomba kupewa muda afuatilie kwani wakati tukio hilo linaripotiwa hakuwa kwenye nafasi hiyo ya Kamanda wa Polisi wa Kinondoni.

 

“Naomba unipe muda nifuatilie. Wakati huo sikuwa kwenye nafasi hii,” alisema Kamanda Taibu. Gazeti hili linaahidi kulifuatilia sakata hilo ili kujua uchunguzi wake umefikia wapi na nini hatma ya Mwiti.

Kwa upande wake mtoto mkubwa wa Mwiti, Ayubu aliyefungua faili la uchunguzi wa kutekwa kwa baba yake na ndiye anayetoka taarifa hiyo kwa ndugu alipotafutwa kwa njia ya simu hakupatikana kutokana na kuwa ‘bize’ wakati wote.

 

Mke mkubwa wa Mwiti alipopigiwa simu ili kuulizwa kinachoendelea kutokana na tukio la mumewe kupotea katika mazingira tatanishi naye hakupatikana, huku kaka wa Mwiti, David simu yake ilita wakati wote bila kupokelewa.

Kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko mwingi gazeti hili linaendelea kuifuatilia habari hii kwa undani na kile kitakachokuwa kikipatikana kitatolewa kwenye vyombo vyetu vya habari siku zijazo.

Toa comment