The House of Favourite Newspapers

INATISHA Kifaranga Chatumika Mauaji ya Wanawake 3

INATISHA! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kifaranga cha kuku kudaiwa kutumika kama ramli chonganishi iliyosababisha mauaji ya wanawake watatu waliokutwa wametelekezwa vichakani katika Kata ya Salawe, Shinyanga Vijijini.

 

 

Mmoja wa wanakijiji hicho ambaye aliomba hifadhi ya jina, aliliambia Uwazi kuwa, hivi karibuni, miili ya wanawake watatu kwa nyakati tofauti ilikutwa vichakani ikiwa imejeruhiwa na mapanga na ndipo wanakijiji kwa kushirikiana na jeshi la polisi waliposhirikiana kutafuta kiini cha mauaji hayo.

“Wanakijiji walifanya uchunguzi na kumshuku mganga wa kienyeji aitwaye Itawa Ming’hwa kuwa anahusika kwani ndiye anayewafanyia watu ushirikina kwa kutumia ramli mbalimbali ikiwemo hiyo ya kifaranga cha kuku kisha kuwaambia wakawatoe wanawake kafara.

KISA NI UTAJIRI

“Wengi wanaokwenda kwa mganga huyo huwa wanahitaji utajiri hivyo wanapofanyiwa ramli na kuambiwa wanatakiwa wawatoe wanawake kafara, huwa hawajiulizi mara mbili. Wanakwenda kutekeleza unyama huo na ndiyo maana hata miili ya wanawake watatu iliyokutwa kichakani hivi karibuni, imehusishwa na mganga huyo,” alisema mwanakijiji huyo.

 

Baada ya wanakijiji kufanya uchunguzi wao na kumbaini mganga huyo, walilishirikisha jeshi la polisi ambalo lilifika haraka na kumkamata mganga huyo wa kienyeji sambamba na wenzake wanne kwa tuhuma ya kujihusisha na mauaji ya kukata mapanga wanawake kwa imani za kishirikina.

 

 

KAMANDA AZUNGUMZA

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo kwenye mikutano ya hadhara miwili iliyofanyika katika Kijiji cha Mwenge na Songambele baada ya kuongoza kufanya msako mkali kusaka wauaji.

AWATAJA WANAWAKE WALIOUAWA

Kamanda huyo amewataja wanawake watatu ambao wameshauawa kwenye imani hizo za kishirikina kuwa ni Mwalu Misri (24), Salome Paschal (24) Kabunga Linonelwa(10), ambao waliuawa kwa nyakati tofauti kuanzia kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu baada ya kuviziwa kwenye vichaka na kisha kuuawa.

 

 

WATUHUMIWA

Amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuhusika na mauaji hayo kuwa ni Stephano Maduka (20), Nihinga Lendele (57), Reuben Mafura (30), Amosi Itawa (21) pamoja na mganga wa kienyeji, Itawa Ming’hwa (47) ambapo wote wapo chini ya ulinzi wa jeshi hilo na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

 

MAKOROKORO WALIYOYAKUTA

Kamanda Haule aliongoza ufuatiliaji wa wanaodaiwa kufanya unyama huo na akasema kuwa walipofanya upekuzi nyumbani kwa mganga huyo wa kienyeji alikutwa akiwa na mkia wa mnyama adhaniwaye kuwa ni nyati, ngozi ya kenge, kipande cha ngozi ya fisi, pembe nne za wanyama mbalimbali, shuka tano nyeusi za kaniki, karatasi nakala tatu zenye maandishi yanayohimiza kuua watu na kifaranga cha kuku kinachotumika kupigia ramli chonganishi.

 

 

NGUO YA NDANI PIA IMO

Ametaja vitu vingine kuwa ni nguo ya ndani moja ya kike, mafungu mbalimbali ya mchanga, mawe yadhaniwayo kuwa ni madini ambayo yanatumika kupigia ramli chonganishi, pamoja na karatasi ikiwa na majina ya wanawake tisa ambao wamepangwa kuuawa ili kukamilisha ushirikina huo. “Baada ya kuwahoji watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na mauaji haya kwa madai kuwa waliagizwa na waganga wa kienyeji kwa kutoa kafara za wanawake tisa ili dawa zipate kufanya kazi na kupata utajiri,” amesema Kamanda Haule.

 

 

ATOA ONYO

Katika hatua nyingine Kamanda Haule ametoa wito kwa wananchi hasa vijana kuacha kutafuta mali kwa njia za ushirikina bali wajiunge kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze kukopesheka na kufanya kazi halali ambazo zitawaingizia kipato na kuinuka kiuchumi.

 

 

 

 

Nao baadhi ya wanawake waliohudhuria kwenye mikutano hiyo ya hadhara, Neema Paulo na Happynes Jeremia wameiomba serikali kukomesha kabisa matukio hayo ya mauaji dhidi yao ambayo yamekuwa yakiwafanya kushindwa kwenda kufanya shughuli za kiuchumi.“Tunashindwa kwenda mashambani kwa kuhofia kuuawa kwa kukatwakatwa mapanga kama walivyofanyiwa wenzetu, tunakuomba mkuu wa polisi hili lidhibitiwe,” alisema Neema.

STORI: MWANDISHI WETU, SHINYANGA

Comments are closed.