Watoto Wafariki kwa Kuzama Kwenye Dimbwi Wakifua, Wazazi Wasimulia – Video
Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Isengwa kilichopo Kata ya Lagangabilili wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu, limeopoa miili ya watoto wanne wote wa kike baada ya kuzama kwenye dimbwi lenye kina kirefu na maji mengi kijijini hapo.
Akitoa taarifa ya tukio hilo mbele ya waandishi wa Habari, Kaimu Kamanda wa Zimamoto Mkoa Faustine Mtitu, alisema kuwa tukio hilo limepelekea kufikisha vifo vya watu saba katika mkoa huo ambao wamezama kwenye madimbi, visima, mabwawa ndani ya Desemba.
Alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 11:00 Jioni, ambapo watoto hao wanaotoka katika familia tatu tofauti walifika kwenye dimbwi hilo kwa ajili ya kufua nguo zao.
Alisema kuwa watoto hao ambao watatu kati yao, walikuwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Lagangabilili, walizama kwenye Dimbi hilo wakati wakiendelea na shughuli ya kufua nguo zao.
Alisema kuwa mmoja kati ya watoto ambaye alianza kuzama, alitelekeza wakati akichota maji kwenye dimbwi hilo, ndipo mtoto wa pili baada ya kuona mwenzake amezama akaingia kwenye dimbwi hilo ili kumuokoa mwenzake aliyetangulia.