
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi amesema ishu ya Fomu ya polisi ya kuthibitisha Matibabu (PF3) isiwe kipingamizi cha mwananchi aliyepata ajali kushindwa kupata huduma ya dharura kwa sababu ya fomu hiyo.
Prof. Makubi amesema hayo leo ikiwa ni siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hasaan kutoa mapendekezo ya kubadilisha utaratibu kwa waliojeruhiwa kwa ajali mbalimbali kulazimika kupata PF3 ndipo watibiwe jambo ambalo linasababisha baadhi yao kupoteza maisha kwa kukosa huduma kisa hawana PF3.
“Kuanzia sasa vituo vyote vya kutolea huduma nisije nikasikia mtu anakosa huduma aliyepata ajali kwa sababu ya PF3, naomba tulitekeleze hili, utaratibu wa PF3 naomba uandaliwe wakati mtu akiwa anapata huduma,”
Prof. Abel Makubi.

Aidha, Prof. Makubi ameziagiza Hospitali zote za Rufaa nchini kuhakikisha wazee wote wanaoenda katika Hospitali hizo kutibiwa , wanapatiwa huduma bora kuanzia anapowasili hospitalini hapo, kwenye Vipimo hadi kwenye kupatiwa dawa.
“Wazee wetu ni lazima wapate huduma bora, kuanzia kumpokea, kumpeleka eneo la kupata huduma, kwenye vipimo, hadi kwenye dawa au kama anaenda kulazwa hadi anapotoka, kwa hiyo kwa wazee naomba tusicheze nao, haya ni maelekezo na lazima yatekelezeke,” amesema Prof. Makubi.

